Uharibifu wa barabara uliotokana na mvua zinazoendelea
kunyesha, umeendelea kuwatesa wakazi wa Dar es Salaam na mikoa
mbalimbali nchini hasa baada ya mabasi ya mikoani kuzuiwa kufanya safari
zake jana.
Amri ya kuzuia mabasi hayo ilitolewa jana ikiagiza mabasi
yote yasiondoke katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo hadi
itakapotangazwa vinginevyo, kutokana na uharibifu wa Barabara za Kilwa,
Morogoro na Bagamoyo ambako madaraja yamevunjika.
Dereva wa Basi la Adventure liendalo Kigoma, Joseph Luciano
alisema walitangaziwa na Sumatra na trafiki kuwa wasubiri mpaka hapo
watakapojulishwa kuondoka.
“Hatuwezi kuondoka mpaka Serikali itakapotangaza ili kuepuka
faini ambayo wenzetu, wale wanaopakia nje, wametozwa,” aliongeza huku
ikielezwa kuwa baadhi ya mabasi yalitozwa faini kwa kukiuka amri hiyo.
Abiria anayesafiri kwenda Kibondo, Kigoma, Lydia Lutakinikwa
alisema: “Nilikuja kuchukua mzigo wa duka langu tangu Ijumaa na nimekuwa
nikilala gesti. Nimeishiwa hela hivyo nalazimika kuendelea kuwapo
kwenye hili basi kwa kuwa sina tena pesa ya kwenda kulipia malazi.”
Kondakta wa Basi la Taqwa liendalo Nairobi, Yahaya Maulid
alisema wameruhusu kubadilishwa tiketi za abiria wao, kama
walivyoelekezwa na mamlaka husika ili kutoa nafasi kwao kujipanga upya.
Mkuu wa Usalama Barabarani Ubungo, Inspekta wa Polisi, Yusuf
Kamutta alisema zaidi ya mabasi 400 yameathiriwa na uamuzi huo…
“Tumezuia mawakala wasitoe tiketi mpya kwa sababu abiria wa leo (jana)
ndiyo wanaotarajiwa kusafiri kesho, hivyo wanaweza kuuza tiketi za
kuanzia keshokutwa.”
Msururu wa magari Pwani
Kutokana na kuharibika kwa baadhi ya madaraja katika Mkoa wa
Pwani, magari yaliyokuwa yakisafiri kutoka maeneo mbalimbali yalikwama
katika maeneo tofauti. Baadhi yalikwama Visiga na mengine Mlandizi
jirani na Kituo cha Polisi katika misururu mirefu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei aliwataka
wamiliki wa magari makubwa ya mizigo wanaotumia barabara hiyo kusitisha
safari zao kwa kipindi hiki hadi hapo hali itakapotengamaa.
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Pwani na uongozi wa
Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ililazimika kuweka kambi kwa siku
nzima eneo la Mlandizi jirani na daraja la Ruvu kusimamia shughuli ya
ukarabati wa daraja dogo lililokuwa na hitilafu.
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Pwani, Tumaini Sarakikya alisema
hadi jana mchana magari yalikuwa yameanza kupita upande mmoja, lakini
baadaye jioni yangeanza kupita bila wasiwasi.
Waliokufa Dar wafikia 13
Mafuriko yaliyotokana na mvua hizo yamesababisha vifo vya
watu 13 mkoani Dar es Salaam hadi jana, huku Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili (MNH) pekee ikipokea maiti tisa.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema maiti
mbili zilipatikana Wilaya ya Temeke na nyingine moja ilikutwa eneo la
Jangwani, Ilala na miili hiyo imehifadhiwa MNH na Hospitali ya Temeke.
Alisema jitihada zinaendelea kubaini iwapo kuna miili zaidi
katika mito na mabonde ambayo yalikumbwa na mafuriko hayo na ameomba
mwananchi kutoa ushirikiano.
Ofisa Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema hadi jana
hospitali hiyo ilikuwa imepokea maiti tisa zote zikiwa za wanaume na
kati ya hizo, mbili zimetambuliwa na ndugu zao.
Kwa upande mwingine, Kamanda wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi wa
Kinondoni, Mark Njela alisema maiti moja ya mwanamume ilikutwa jana
kwenye Mto wa Mabibo nyuma ya Kampuni ya Ami.
MWANANCHI