AFYA YA ‘MTOTO WA BOKSI’ YABADILIKA GHAFLA, KULETWA DAR LEO

Morogoro. Hali ya mtoto Nasra Rashid (4) aliyekuwa amefichwa kwenye boksi kwa miaka minne, imebadilika ghafla juzi na jana kuwalazimu madaktari kumweka katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.(Martha Magessa)
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rita Lyamuya alisema jana kuwa tatizo kubwa la mtoto huyo ni kubadilika ghafla kwa upumuaji wake na utaratibu unafanyika ili leo asafirishwe kupelekwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
"Tunatarajia kumpeleka Muhimbili mapema asubuhi kwa gari maalumu la wagonjwa ili kupata matibabu zaidi," alisema Dk Lyamuya.
Alisema juzi Nasra alikuwa mwenye furaha na mchangamfu lakini jioni yake hali ilibadilika katika mfumo wake wa kupumua.
Alisema kwa msingi huo, uongozi wa hospitali ya mkoa umeamua kumsafirisha kwenda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.
Uchunguzi wa awali wa afya ya Nasra ulibaini kuwa mtoto huyo alikuwa na maradhi ya nimonia (kichomi), mifupa ya miguu na mikono kuvunjika pamoja na utapiamlo.
Watuhumiwa kortini
Katika hatua nyingine, watu watatu akiwamo baba mzazi wa Nasra, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Morogoro kujibu mashtaka ya kula njama na kufanya ukatili dhidi ya mtoto huyo.
Baba wa mtoto huyo Rashid Mvungi (47), mama mlezi wa Nasra, Mariamu Said (38) na mumewe Mtonga Omar (30), walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mary Moyo jana na kusomewa mashtaka hayo.
Wakili wa Serikali, Sunday Hyera alidai kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Desemba, 2010 na Mei mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege, mjini Morogoro.
Alidai kuwa katika kipindi hicho walimfanyia ukatili wa kumtelekeza na kumpa malezi akiwa ndani ya boksi na hivyo kumsababishia magonjwa.
Alitaja maradhi yaliyomkumba akiwa ndani ya boksi ni utapiamlo, kichomi na mvunjiko wa mifupa.
CHANZO:MWANANCHI


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...