Fainali
za Kombe la Dunia ni uwanja mpana. Ni mahali ambapo vipaji na vipaji
vya wanasoka duniani huonekana. Madalali wa kuvumbua na kununua
wachezaji [scouts] hufurika kwenye mashindano kama haya wakijua wazi
kabisa kwamba pale ndipo watakapoona “lulu” kwa ajili ya vilabu vyao.
Kwa maana hiyo kuna kila aina ya harakati za kimichezo na kuonyesha na
kuonyeshana vipaji. Hii sio kumaanisha kwamba wachezaji wote mahiri hapa
duniani walicheza katika fainali za Kombe la Dunia.La. Wapo wasakata
kabumbu kadhaa ambao hawakuwahi kugusa fainali hizi.Mfano ni George
Opong Weah na watu kama kina George West nk.
Lakini
wakati wengine wakionyesha vipaji ili wang’amuliwe na kubadilisha
maisha yao ya kisoka,wapo wale ambao wanashuka dimbani tayari wakiwa na
majina [superstars] na ambao dunia tayari inakuwa ikiwaangalia kwa
makini kutaka kujua na kuona kile watakachokifanya. Kila timu huwa na
mchezaji ambaye hutizamwa zaidi. Kwa umombo unaweza kumuita Key Player.
Kila timu,kwa kupenda au kutopenda,huwa ina star player. Hii haimanishi
kwamba katika timu hakuna wachezaji wengine wenye majina au wanaoweza
pia kuwa stars.La. Ni sheria ya mmoja mmoja inayozingatiwa hapa.
Kwa mujibu wa wataalamu
mbalimbali wa soka,wachezaji hawa 32 [mmoja kutoka katika kila timu
inayoshiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka huu] ndio watarajiwa
kuchomoza zaidi huko Brazil. Mpangilio huu hapa ni kutokana na makundi
ya FIFA World Cup 2014. NB: Orodha hii inaweza kubadilika kwani
imeandikwa kabla timu zote hazijathibitisha wachezaji wake 23
iliyowachagua mwisho. Wengine wanaweza kuumia katika siku hizi za mwisho
na hivyo kutokwenda Brazil.Zingatia.
Neymar-Brazil.
Hakuna
ubishi kwamba Neymar anayechezea soka la kulipwa Barcelona nchini Spain
ndio gumzo kubwa kwa timu ya Brazil. Anatarajiwa kuongoza mashambulizi
ya The Kings Of Samba[Brazil]
Oribe Peralta-Mexico
Ingawa
wachezaji wengine wa Mexico kama Chicharito na Giovani dos Santos
wanatajwa kama ma-star,Oribe Peralta ambaye anacheza katika ligi ya
nyumbani katika club ya Santos Laguna, ndiye anaaminika hivi sasa kuwa
star zaidi
Luka Modric-Croatia
Hakuna
shaka kwamba Luka Modric ndiye mchezaji star zaidi hivi sasa katika timu
ya Croatia. Kiungo huyu ambaye hivi sasa anachezea timu ya Real Madrid
nchini Spain ameonekana wazi kuwa tegemeo sio tu katika club bali nchi
yake Croatia.
Charles Itandje-Cameroon
Ingawa
ungetegemea mchezaji kama Samuel E’too kuendelea kuwa star na tegemeo
zaidi katika timu ya Cameroon, golikipa Charles Itandje ndio tegemeo na
ambaye wengi watapenda kumuona akiokoa mikwaji. Charles ambaye anachezea
timu ya Konyaspor nchini Uturuki[kwa mkopo kutoka PAOK FC ya Ugiriki]
aling’ara vilivyo katika mchezo dhidi ya Tunisia wakati wa kuwania
nafasi ya kwenda Brazil.Google utaona alichofanya.
Diego Costa-Spain
Ingawa
bado kuna utata kuhusu hali yake na kama atakuwa fit kabla ya kuanza kwa
fainali za Kombe la Dunia huko Brazil,Diego Costa mshambuliaji mahiri
wa timu ya Atletico Madrid anatarajiwa kuwa nyota wa Spain. Lakini pia
huenda akawa ndiye mchezaji atakayezomewa zaidi huko Brazil kwani Diego
ni mzaliwa wa Brazil na angeweza kabisa kuchezea Brazil mwaka huu kama
asingeamua kuchezea Spain[pia ni raia wa Spain].Wabrazil hawajaipenda
hiyo.
Arjen Robben-Holland[The Netherlands]
Robben,mshambuliaji
mahiri ambaye hivi sasa anaendelea kuwika na timu ya Bayern Munich
nchini Ujerumani,ndiye mchezaji ambaye ni star zaidi na ambaye
ameonyesha kuwa na kile kiwango kinachoitwa “cha dunia”. Ana miaka 30
hivi sasa.
Arturo Vidal-Chile
Arturo
ambaye anachezea club ya Juventus nchini Italia ni mchezaji “kiraka” wa
Chile ambaye endapo Chile itaushangaza ulimwengu wa soka huko
Brazil,bila shaka mchango wake utakuwa mkubwa.
Tim Cahill-Australia
Tim
Cahill anayechezea timu ya New York Red Bulls katika ligi ya soka ya
Marekani na Canada[Thiery Henry alipitia hapo baada ya Ulaya] ndiye
nyota kwa upande wa Australia.
James Rodriguez “Hames”-Colombia
Kwa
upande wa Colombia Ramadel Falcao, ndio mchezaji nyota zaidi.Lakini kuna
kila aina ya dalili kwamba mwaka huu hatoweza kucheza kutokana na
kusumbuliwa na maumivu ya goti.Hapo ndipo James Rodriguez anapochukua
nafasi. Rodriguez au Hames kama anavyoitwa na mashabiki wa soka huko
Colombia, anachezea AS Monaco ya Ufaransa.
Yaya Toure-Ivory Coast
Kama yupo
mchezaji kutoka barani Afrika[bila kujali timu] ambaye sio tu anapendwa
na mashabiki wengi barani Afrika hivi na ambaye yupo kwenye kiwango cha
juu,basi bila shaka ni Yaya Toure. Hata wachezaji wenzake wa Ivory
Coast kama vile mkongwe Didier Drogba,wote wanamtaja Yaya kuwa kiongozi
na mhimili wa timu yao. Yaya anachezea mabingwa wa Ligi Kuu ya
Uingereza, EPL Champions, Manchester City
Kostas Mitroglou-Greece
Ingawa
mashabiki wa Ligi Kuu ya Uingereza bado hawajapata nafasi ya kuona
vizuri makeke ya Kostas ambaye anacheza katika klabu ya Fulham, ni wazi
kwamba yeye ndio tegemeo kubwa la timu ya Ugiriki katika mashindano ya
mwaka huu.
Keisuke Honda-Japan
Ingawa
Japan wanao mastar wengine kama vile Shinji Kagawa anayechezea
Manchester United,hakuna ubishi kwamba Keisuke Honda ndiye mhimili mkuu
kwa sasa. Anachezea AC Milan nchini Italy.
Wayne Rooney-England
Ingawa
msimu wa ligi kwa upande wa timu yake ya Manchester United haukuwa wa
kuvutia sana, Wayne Rooney au ukipenda unaweza kumuita Wazza anabakia
kuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo zaidi kwa upande wa timu ya taifa ya
Uingereza. Hana historia nzuri sana na mashindano ya Kombe La Dunia
lakini endapo kelele za waingereza[na wana kelele kweli] zitakuwepo,basi
Wazza anaweza kuwa chanzo.
Mario Balotelli-Italy
Miaka
kadhaa iliyopita[na hata hivi sasa miongoni mwa watu] ni vigumu kuamini
kwamba mtu mweusi ndio key player kwa timu ya taifa ya Italy. Muda
umebadilika na mchezaji huyu mwenye mbwembwe,hasira na kila aina ya
vituko ndiye ataangaliwa zaidi pindi timu yake ya Azzurii itakapoteremka
dimbani huko Brazil.
Luis Suarez-Uruguay
Kama
ilivyo kwa Balotelli hapo juu,Luis Suarez ni mchezaji mwingine ambaye
ana kila aina ya vioja. Pamoja na hayo ni mfungaji hodari na ndio
tegemeo kubwa la Uruguay huko Brazil.Kwa bahati nzuri au mbaya,Uruguay
wapo kundi moja England na hivyo lazima watapimana joto. Upinzani kutoka
Liverpool utaendelea?Tutaona.
Keylor Navas-Costa Rica
Sio mara
nyingi sana kuwemo kwenye Kombe la Dunia na kisha kutamba kwamba
mchezaji wenu mhimili ni kipa.Costa Rica wao wanaweza kusema hivyo kwani
Keylor Navas anayechezea timu ya Levante nchini Spain ndio mhimili na
ambaye anategemewa kulinda mlango na kuongoza wenzake.
Franck Ribery-France
Ukisema
Franck Ribery wa Bayern Munich basi bila shaka itabidi pia useme Franck
Ribery wa Ufaransa. Ndio tegemeo. Mwaka huu alikuwepo katika wachezaji
watatu wa juu waliokuwa wanawania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa
FIFA.
Xherdan Shaqiri-Switzerland
Endapo
Switzerland itakuwa na mafanikio makubwa huko Brazil,basi Xherdan ndio
atakuwa mpishi mkuu.Anachezea Bayern Munich pembeni ya Ribery na Arjen
Robben.
Antonio Valencia-Equador
Winga
huyu ambaye anachezea Manchester United ndio tegemeo kubwa la Equador
katika mashindano ya mwaka huu.Wenzake wanamuita “kiongozi”.
Emilio Izaguirre-Honduras
Emilio
anachezea Celtic FC kule Uskochi. Kwa upande wa Honduras ndiye tegemeo
kubwa hususani kwa upande wa ulinzi na kusukuma mbele mashambulizi.
Lionel Messi-Argentina
Hakuna
ubishi kwamba Messi ni miongoni mwa wachezaji mahiri kabisa waliowahi
kuucheza mchezo wa soka hapa duniani.Hata hivyo, ana kasoro moja kwa
mujibu wa wachambuzi wa soka na hususani wasiompenda;hajawahi kushinda
Kombe La Dunia. Kwa maana hiyo,kama unadhani Neymar wa Brazil ana presha
ya kuipa Brazil kombe,Messi pia anayo na zaidi.Argentina na ulimwengu
unasubiri…ataiwezesha kushinda Kombe La Dunia mwaka huu?
Edin Dzeko-Bosnia & Herzegovina
Bosnia
& Herzegovina ni wageni katika fainali za Kombe La Dunia.Hii ndio
mara yao ya kwanza. Pamoja na hayo,wanaye Edin Dzeko mshambuliaji
anayechezea mabingwa wa Uingereza,Manchester City. Ndiye atagemewa
kuwaongoza wenzake kufanya “muujiza” huko Brazil.
Ashkan Dejagah-Iran
Iran
wanasema hawaendi Brazil “kutalii”.Bila shaka wanasema hivyo wakiangalia
wachezaji wao kama Ashkan Dejagah ambaye anacheza soka ya kulipwa
nchini Uingereza. Huyu bwana anao pia uraia wa Ujerumani na alipokuwa
mdogo aliwahi kuchezea timu ya vijana ya Ujerumani akiwa na Mesut Ozil.
Emmanuel Emenike-Nigeria
Ingawa
ligi anayochezea[Uturuki] haina umaarufu sana, hakuna ambaye anatilia
shaka uwezo wa Emmanuel Emenike katika soka. Ni mshambuliaji mahiri na
makini. Anatarajiwa kuongoza mashambulizi ya Nigeria[Super Eagles] timu
ambayo inatarajiwa kufanya vizuri huko Brazil.
Phillip Lahm-Germany
Miongoni
mwa wachezaji wa timu ya Ujerumani ambao ni vigumu sana kwa kocha wa
Ujerumani,Joachim Low, kupata mtu wa kuziba pengo lake[endapo itatokea
akaumia au vinginevyo] ni Kapteni Phillip Lahm. Mchezaji huyu ambaye
anachezea Bayern Munich ni muhimu na ndiye anaongoza Ujerumani huko
Brazil ikitarajiwa kwamba mwaka huu watafanya vyema zaidi.
Majeed Waris-Ghana
Ghana au
Black Star ni miongoni mwa timu kutoka Africa ambazo zinatarajiwa
kufanya vyema nchini Brazil. Kama utakumbuka,Ghana katika fainali za
Afrika Kusini mwaka 2010 walibakia almanusura kutoboa na kufika nusu
fainali. Majeed Waris anayechezea soka la kulipwa FC Valenticiennes huko
Ufaransa anajua vyema wakati gani apige,akimbie nk.Ni mchezaji ambaye
anatarajiwa kuipa forwardline ya Ghana uhai mkubwa na kushirikiana vyema
na Asamoah Gyan.
Clint Dempsey- USA
Hakuna
ubishi kwamba mchezaji wa US ambaye alikuwa anatizamwa na wengi kuongoza
timu ya nchi hiyo ni London Donovan. Kwa bahati mbaya kocha mjerumani
Jurgen Klinsman, hakuona hivyo. Donovan katemwa. Badala yake mchezaji
Clint Dempsey ndiye ambaye anatarajiwa kuongoza jahali za USA.
Christiano Ronaldo-Portugal
Hivi sasa
ndiye anashikilia taji la FIFA La Mchezaji Bora wa Dunia. Timu
anayochezea,Real Madrid ndio mabingwa wa Ulaya na yeye akiwa na rekodi
ya magoli 17 ya Ligi ya Mabingwa. Hakuna ubishi kwamba Portugal
wanakwenda Brazil kutokana na mchango wake mkubwa hususani katika ile
mechi iliyowaweka pembeni Sweden. Ronaldo au CR7 ndiye mhimili mkubwa wa
Ureno.
Eden Hazard-Belgium
Swahiba
wangu wa karibu,Esmail Manambi,majuzi alinikumbusha kwamba
Ubelgiji,ingawa sio miongoni mwa timu zinazotajwa sana linapozungumziwa
suala la Ubingwa wa Dunia, wanaweza kuushangaza ulimwengu. Nakubaliana
naye kabisa. Ubelgiji ya mwaka huu imejaa wachezaji wenye vipaji na
majina. Kuna kila Kompany,Lukaku,Fellaini nk. Wote,hata
hivyo,wanaangalia zaidi kwa Eden Hazard ambaye mwaka jana Chelsea
walikohoa paundi Milioni 32 kumnunua.
Roman Shirokov-Russia
Kama
utakumbuka wakati wa fainali za South Africa kocha wa Uingereza wakati
huo,Fabio Capello kidogo apate wazimu.Ule utulivu wake uliisha ghafla.
Wanasema kelele za Vuvuzela zilizingua sana. Hivi sasa Capello ndio
kocha wa Urusi. Na kama kuna mchezaji ambaye anaweza kusaidia
kutorudisha ule mzimu wa Capello South Africa basi mchezaji huyo ni
Roman Shirokov anayechezea Krasnodar.Ndiye Kapteni wa Urusi.
Ki Sung-Yueng-South Korea
Ingawa
Korea Kusini inapewa nafasi ndogo zaidi kunako Ubelgiji na Urusi katika
kundi lao, endapo watasonga mbele basi bila shaka mchango wa Ki Sung
Yueng anayechezea Sunderland kwa mkopo kutoka Swansea,hautokuwa
mdogo.Ndiye tegemeo kubwa la Korea ya Kusini.
Madjid Bougherra-Algeria
Algeria
ni timu nyingine kutoka Afrika mwaka huu.Nchi hii ina uzoefu zaidi wa
Kombe la Dunia. Kapteni wao Madjid Bougherra anayecheza soka lake la
kulipwa nchini Qatar na timu ya Lekhwiya, ndiye anayetarajiwa kuongoza
jahazi.Ameshachezea nchi yake katika zaidi ya mechi 60.