MFUKO
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeazimia kuongeza wanachama wake
ambao kwa sasa ni asilimia 7.4 ya Wananchi wote kwa kuvisajili vikundi
mbalimbali vya wajasiriamali na ushirika katika huduma za Mfuko kwa
kupitia uchangiaji wa mtu mmoja mmoja.
Hayo yamo katika hotuba ya Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii iliyosomwa Bungeni jana.
Waziri
wa wizara hiyo Dk Seif Rashid alisema katika utaratibu huo, uongozi wa
vikundi ndiyo utakuwa wadhamini na pia ndiyo utakaokuwa wakala wa Mfuko
katika ukusanyaji wa michango na ufuatiliaji wa upatikanaji wa huduma.
Mkakati
huoumelenga kuongeza wigo wa wanufaika wa huduma za bima ya afya nchini
kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2015. Kwa sasa huduma hiyo imefikia
asilimia 19.2.
Vilevile, alisema Mfuko utafanya tathmini ya nne ya Mfuko ili kuangalia uhai wa Mfuko na huduma zake kwa wanachama.
Akizungumzia utaratibu
wa kugharimia huduma za afya kwa kuchangia Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF)
kwa ajili ya sekta isiyo rasmi na wananchi waishio vijijini, Waziri
huyo wa Afya alisema hadi kufikia mwezi Machi, 2013 Watanzania 4,010,844
sawa na asilimia 9.2 walikuwa wamejiunga na Mfuko huo.
Aidha
Dk Rashid alisema kutokana na tathmini iliyofanywa, Mfuko wa Afya wa
Jamii kwa sehemu za mjini umeanza kutumika katika mkoa wa Dar es Salaam
kwa kuhusisha vikundi vya uzalishaji.
Alisema
katika hotuba yake kwamba katika mwaka 2014/15 utaratibu huo
unaojulikana kama Tiba kwa Kadi (TIKA) unatarajiwa kuenezwa katika mikoa
ya Mwanza, Singida, Ruvuma, Pwani, Tanga, Lindi na Kilimanjaro.
"Naomba
nichukue nafasi hii kuwashauri Waheshimiwa Wabunge wote kujiunga na
Mfuko huo ili kuwa mfano na kutoa elimu ya Mfuko huo katika maeneo yenu
ili wananchi wengi waweze kujiunga. Mimi binafsi nimejiunga na Mfuko huu
na nimeona faida zake hivyo nawaomba wananchi wote nchini wajiunge na
Mfuko huo" alisema Waziri Rashid.
Aidha
alisema Wizara imekamilisha na kuzindua Mpango Mkakati wa Matumizi ya
TEHAMA katika sekta ya afya wa mwaka 2013 - 2018, ikiwa ni utekelezaji
wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, inayoelekeza matumizi ya mfumo endelevu
wa habari na mawasiliano katika shughuli za sekta ya afya.
Akifafanua
zaidi amesema Wizara yake pia imeboresha huduma za tiba kwa njia ya
mtandao - telemedicine, na kuwa hadi sasa huduma hiyo inajumuisha
hospitali ya rufaa ya kanda Mbeya, Temeke, Bagamoyo, Mwananyamala,
Amana, Tumbi na Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili.
Katika
mwaka huu wa fedha Wizara itaunganisha Hospitali za Rufaa za Kanda
(Bugando na KCMC), na Hospitali maalumu (Mirembe, Ocean Road na MOI)
katika mfumo wa telemedicine ili kuboresha huduma za ushauri na tiba
katika mtandao na kupunguza rufaa zisizo za lazima.
Akizungumzia
vyanzo vya kugharamia huduma za afya, Dk Rashid alisema Bima za afya
imekuwa moja ya vyanzo muhimu sana katika vituo vya kutolea huduma za
afya na kupunguza pengo la mahitaji ya raslimali fedha kwa kiwango
kikubwa.
Alisema
kutokana na Ripoti ya Mapitio ya Matumizi ya Fedha za Umma (Public
Expenditure Review – PER, 2012) inaonesha kwamba vyanzo mbadala
vinachangia wastani wa asilimia 5 ya mapato yote ya Halmashauri kwa
sekta ya afya.
"
Hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2014 Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
uliwalipa watoa huduma za matibabu kiasi cha Sh. bilioni 77.7. " alisema
na kuongeza kuwa:Mfuko umeanza kutekeleza utaratibu wa kuwaunganisha
watoa huduma katika mtandao wa kompyuta ili wawe wanaandaa na
kuwasilisha madai kwa njia ya kielektroniki.
Alisema
hatua hiyo imekusuduia kupunguza muda wa malipo na kuharakisha
utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa e-Health ambao Wizara iliuzindua
Oktoba mwaka jana.
Nayo
Kamati ya Bunge ya afya imesema ipo haja ya Huduma za bima ya afya
ziwafikie wananchi wote ikijumuisha wazee, watoto, watu wenye ulemavu,
yatima, wajawazito na wasio na kipato kama haki yao ya msingi.
Aidha
imeitaka Serikali ibuni njia mbadala ya kupata fedha kutekeleza mradi
wa ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Kanda ya Kusini inayotakiwa kuejengwa
Mtwara.
Kuhusu
ujenzi na karabati wa vituo vya kutoa huduma , kamati hiyo ya kudumu ya
bunge imetaka kuandaliwa kwa mikakati maalumu ili kupunguza utegemezi
kwa kushirikisha wadau wa ndani
Nayo
kambi ya upinzani katika hotuba yake imetaka Mifuko inayogharamia
huduma za Afya (NHIF, CHF/TIKA, CBHI, NSSF-SHIB) iwekewe utaratibu wa
kufanyakazi kwa pamoja.
Aidha
wametaka mapendekezo ya Mfumo wa ugharamiaji huduma za afya kwa wote
yawasilishwe kwa Wadau wakiwemo waheshimiwa Wabunge na waelimishwe
kuhusu dhana hiyo.
Usimamizi wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) uimarishwe hususani katika eneo la fedha zinazochangwa na wananchi.