WAKATI Rais
Dkt. Jakaya Kikwete anataraji kuwa mgeni rasmi wa kilele cha siku ya
maadhimisho ya mazingira duniani yanayoadhimishwa kitaifa Juni 5 mwaka
huu mkoani Mwanza, uchafuzi wa mazingira mto Mirogo umeongezeka jijini
hapa.
Imebainika
kuwa, Kaya 75 jijini humo zinatirilisha vinyesi na majitaka ndani ya
Mto Mirongo unaomwaga maji machafu Ziwa Victoria hali ambayo imedaiwa
kuongezaka kwa kasi ya uchafuzi wa mazingira na uharibifu wa mto huo
hivyo kuhatarisha afya watumiaji wa maji ikiwemo wanyama, mimea na
viumbe hai waishio majini.
Hali
hiyo pia ilijitokeza na kushuhudiwa na baadhi ya wadau wa mazingira
kutoka Menejimenti ya Ofisi za Maji Bonde la Ziwa Victoria, Maafisa Afya
wa Jiji la Mwanza na Jumuia ya waumiaji wa maji na mazingira walipokuwa
wakifanya zoezi la kufafisha mto Mirongo hii leo ikiwa ni sehemu ya
maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yanayofanyika jijini humo.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika eneo la daraja la Mabatini linalopitiwa
na mto huo baada ya kubaini kuwepo kwa Kaya hizo, Kaimu Afisa wa Maji
kutoka Bonde la Ziwa Victoria Godfrey Kajanja alisema kwamba, Ofisi yake
na Halmashauri ya Jiji zitakutana kuchukua hatua za kisheria kwa Kaya
hizo na watu walio na tabia ya kuchafua maji ya mito.
Kajanja
alisema kwamba, hali hiyo ikiachwa kuendelea bila kudhibitiwa
kutawezesha kuibuka magonjwa ya tumbo endapo Mamlaka ya Majisafi na
Mazingira ya jijini humo haitachukua hatua za kuongeza kiasi kikubwa cha
dawa ya kutibu maji kabla ya kusambazwa kwa watumiaji.
“Lazima
sasa tushirikiane kuzitekeleza sheria zilizopo za Mipango miji kwa
upande wa Jiji la Mwanza, pamoja na ofisi yetu ya Bonde kutumia sheria
ya usimamizi wa rasilimali ya maji Na. 11/2009 na sheria ya usimamizi wa
mazingira Na. 24/2004 ambazo zinaoanisha adhabu ya fedha na kifungo kwa
watu watakaokaidi na kukutwa na makosa,” alisema.
Kwa
upande wake Mhandisi wa Maji toka ofisi za Bonde la Ziwa Victoria
Mhandisi Jane John alieleza kwamba, hatua hivyo inatakiwa kukomeshwa
mara moja na jamii iliyo kandokando ya maeneo unapipita mto Miringo na
maeneo ya vyanzo vya maji ili kusaidia kulinda na tabia ya uchafuzi wa
mazingira ikiwemo udhibiti jambo ambalo litaepusha uharibifu na
uchafuzi.
“Tumeshuhudia
mabomba ya vinyesi na maji machafu yakimwaga mtoni wakati tukifanya
usafi wa pamoja kwenye mto Mirongo na wadau mbalimbali walioko kwenye
maadhimisho ya siku ya mazingira kitaifa hili ni jambo ambalo linahitaji
hatua za haraka kulikomesha na kuwachukulia hatua wanaofanya uchafuzi
huu,”alisisitiza.
Naye
Mwenyekiti wa NGO ya Jumuiya ya watumiaji maji na mazingira Adam Shija
ya Kata ya Mbugani Wilayani Nyamagana mkoani hapa alisema kwamba,
tumekuwa na changamoto kubwa wakati wa usafishaji wa mto huo na
wamebaini kuwepo kwa baadhi ya Kaya 75 ambazo zimekuwa zikitirilisha
uchafu wa vinyesi na majimachafu ndani ya mabomba yaliyoelekezwa mtoni
humo.
Shija
alifafanua walipotembelea kandokando yam to huo kwenye maeneo ya
unapoanzia na kupitia kasha kumwaga maji ziwani Victoria katika Kata za
Nyakato walibaini kaya 16, Mahina kaya 8, Mbugani kaya 24, Mirongo kaya
17, Nyamagana kaya 6 na Pamba kaya 4 na tayari orodha hiyo imetokana na
ukaguzi wa Jumuiya hiyo hivi karibuni.
Wito
wangu kwa Serikali na Idara zenye jukumla la kusimamia rasilimali ya
maji na mito, mabwawa na ziwa Victoria kutekeleza sheria kwa vitendo ili
kukomesha tabia hiyo ya uchafuzi wa maji na uharibifu wa mazingira
unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya wananchi bila kujali kama
husababisha madhala kwa watumiaji wa maji na kuhatarisha uhai wa viumbe
hai majini.