Utangulizi
Ndugu wananchi;
Naomba
nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia
uzima na kutuwezesha kwa mara nyingine tena kuzungumza na taifa juu ya
masuala muhimu yanayohusu nchi yetu. Mwezi wa Saba tunaoumaliza leo
ulikuwa na matukio mengi baadhi yakiwa makubwa na kushtusha na mengine
yalikuwa matukio ya kawaida.
Mashambulio ya Mabomu
Ndugu Wananchi;
Tarehe
3 Julai, 2014 na tarehe 07 Julai, 2014 kulitokea mashambulizi ya mabomu
nyumbani kwa Sheikh Sudi Ally Sudi na katika mgahawa wa Vama kwa
mfuatano huo. Kabla ya hapo, kulikuwa na matukio mengine matatu: Kanisa
la Olasiti tarehe 5 Mei, 2012, Mkutano wa Kampeni wa CHADEMA tarehe 15
Juni, 2013 na Baa ya Arusha Night Park tarehe 13 Aprili, 2014. Hali
kadhalika, tarehe 13 Juni, 2014 kulitokea shambulizi la mabomu katika
eneo la Darajani, Zanzibar.
Kila
lilipotokea shambulizi uchunguzi ulifanyika na watuhumiwa kukamatwa.
Lakini, watuhumiwa waliokamatwa safari hii wanaelekea kutoa sura nzuri
zaidi ya mtandao wa watu wanaofanya vitendo hivi vya kikatili pale
Arusha na kwingineko nchini. Watu 38 wameishafikishwa Mahakamani,
wengine 8 watafikishwa Mahakamani kesho na uchunguzi na msako unaendelea
kote nchini kuwapata watuhumiwa wengine.
Napenda
kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa vyombo vyetu vya ulinzi
na usalama kwa kazi kubwa na nzuri iliyotufikisha hapa tulipo sasa.
Tunawaomba waongeze bidii, maarifa na ushirikiano mpaka wote waliohusika
wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Aidha,
natoa pongezi na shukrani maalum kwa wananchi wema waliotoa taarifa
zilizowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa. Napenda kutumia nafasi hii
kuwasihi wananchi wenye taarifa kuhusu wanaotafutwa au ye yote
anayejihusisha na vitendo hivi viovu watoe taarifa kwenye vyombo vya
usalama ili hatua zipasazo zichukuliwe.
Kutupwa Viungo vya Binadamu
Ndugu Wananchi;
Tarehe
22 Julai, 2014, katika Bonde la Mto Mpiji lililopo eneo la Bunju Wilaya
ya Kinondoni, Dar es Salaam, viligunduliwa viungo vya binadamu na
baadhi ya vitendea kazi vya madaktari vikiwemo aprons na gloves. Viungo
hivyo vilivyokutwa vimekakamaa na kuhifadhiwa katika mifuko
myeusi 85, vilikuwa vimetupwa jana yake tarehe 21 Julai, 2014. Tukio
hilo lilileta taharuki na hofu kubwa katika Jiji la Dar es Salaam na
nchini kwa ujumla.
Uchunguzi
uliofanywa uligundua kuwa viungo hivyo vilikuwa vinatumika kufundishia
wanafunzi wa udaktari katika Chuo Kikuu cha Tiba kilichoko Mbezi Beach
maarufu kwa jina la IMTU. Ni utaratibu wa kawaida kwa vyuo vikuu vya
udaktari nchini na kote duniani kutumia miili ya wanadamu waliofariki
kufundishia. Hata hivyo, pale viungo hivyo vinapokuwa havihitajiki tena
kwa shughuli hiyo, zipo taratibu zake za kuvisitiri ambazo hazikufuatwa.
Bahati nzuri mamlaka husika zimeona kasoro hiyo na hatua zimeanza
kuchukulikuwa.
Tuziachie mamlaka hizo kuchukua hatua zipasazo kwa mujibu wa madaraka
yao na kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zinazotawala shughuli za namna
hiyo. Ni matumaini yangu kuwa yaliyofanywa na IMTU hayatafanywa tena na
Chuo hicho wala chuo kingine cho chote hapa nchini.
Ziara Yangu Mikoani
Ndugu Wananchi;
Katika
mwezi huu wa Julai, nimefanya ziara katika ya mikoa ya Tanga na Ruvuma.
Nimefurahishwa sana na hatua kubwa ya maendeleo waliyopiga wananchi wa
mikoa hiyo. Pamoja na mchango wa Serikali, ari na mwamko mkubwa wa
kujiletea maendeleo walionao viongozi na wananchi wa mikoa hiyo
vimechangia sana katika kuongeza kasi ya maendeleo na mafanikio
yanayoendelea kupatikana. Katika ziara hizo, nilizindua miradi
iliyokamilika na kuweka mawe ya msingi ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya
maendeleo ikiwemo ile ya barabara, umeme,maji, afya, elimu, majengo ya
Serikali, nyumba na kadhalika.
Nimepata
faraja kubwa kupata taarifa kuwa ahadi zangu nyingi na zile zilizomo
kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi zimekamilika na zingine ziko katika
hatua mbalimbali za utekelezaji. Ndoto ya miaka mingi, kabla na baada ya
Uhuru, ya wananchi wa Mikoa ya Kusini ya kutaka Mikoa yao ifunguke na
kuunganishwa na mikoa mingine kwa barabara za lami sasa kuna uhakika wa
kukamilika. Barabara ya kutoka Mbinga, Songea hadi Namtumbo iliyojengwa
kwa msaada wa Serikali ya Marekani imekamilika na tuliizindua. Tuliweka
mawe ya msingi ya kujenga barabara ya lami kutoka Namtumbo, Tunduru,
Mangaka hadi Mtambaswala kwenye Daraja la Umoja linalounganisha Tanzania
na Msumbiji kwa msaada wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na Serikali ya
Japan. Barabara ya kutoka Mangaka hadi Masasi iliyojengwa kwa msaada wa
Serikali ya Japan imekamilika na tuliizindua. Katika barabara ya kutoka
Mtwara hadi Mbamba Bay kimebaki kipande cha kilometa 66 kutoka Mbinga
kwenda Mbamba Bay ambacho hakikuwa na mpango wo wote wa kuwekewa lami
kwa sasa. Bahati nzuri, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
(ADB), Bibi Tonia Kandiero alitangaza pale Namtumbo kuwa Benki yake
itafadhili ujenzi wa barabara hiyo. Mambo sasa yamekamilika.
Kule
Masasi mkoani Mtwara na Nachingwea mkoani Lindi tulizindua kukamilika
kwa mradi mkubwa wa maji wa Mbwinji unaomaliza tatizo kubwa la maji kwa
miji hiyo kwa miaka mingi ijayo.
Nyumba za Bei Nafuu
Ndugu Wananchi;
Nikiwa
wilayani Mkinga na katika Manispaa ya Songea nilizindua nyumba za
gharama nafuu zilizojengwa na Shirila la Nyumba la Taifa (NHC). Nyumba
hizo za vyumba viwili na vitatu zinauzwa kwa bei ya shilingi milioni
31 hadi 42. Wenzetu wa NHC walinieleza utayari wa kujenga nyumba zaidi
endapo watapatiwa maeneo na Halmashauri za Wilaya na Miji.
Walinilalamikia kuwa hawapati ushirikiano wa kutosha kutoka mamlaka
husika. Nilipokuwa Mkinga na Songea niliagiza Halmashauri hizo na
nyinginezo nchini kutenga maeneo kwa ajili ya NHC na Mifuko ya Hifadhi
za Jamii yote ili waweze kujenga nyumba za bei nafuu kwa ajili ya
wafanyakazi na wananchi kwa ujumla.
Hii
ni fursa ya aina yake kwa wananchi wa kipato cha chini na cha kati
kuweza kujipatia nyumba kwa urahisi. Halmashauri zisiwe kikwazo wakati
ardhi imejaa tele na kila wakati wanapima viwanja vipya. Jambo lingine
zuri waliloniambia viongozi wa NHC ni kwamba zipo Benki ambazo
wanashirikiana nazo kutoa mikopo kwa watu wanaonunua nyumba zao. Ni
matarajio yangu kwamba uongozi wa Halmashauri zote nchini utaitikia
maelekezo yangu na kwamba utatenga maeneo kwa ajili ya mashirika yetu
hayo.
Matibabu kwa Wazee
Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa
wilaya ya Kilindi nilifurahishwa sana na utaratibu wa kuwapatia wazee
huduma ya matibabu. Kama mjuavyo Sera ya Afya inataka wazee na watoto wa
chini ya miaka mitano watibiwe bure katika hospitali za Serikali.
Bahati mbaya vitambulisho wanavyopata wazee vimekuwa havithaminiwi ya
kutosha. Kwa sababu hiyo, nafuu wanayostahili kupata imekuwa haipatikani
kwa urahisi na wengine huikosa kabisa.
Katika
Wilaya ya Kilindi, Halmashauri ya wilaya imeamua kuwakatia wazee hao
Bima ya Afya inayotolewa na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na hivyo
kuondoa kabisa migogoro inayohusiana na vitambulisho vya wazee
vilivyokuwepo kabla. Kwa kuzingatia malalamiko ya mara kwa mara
ninayoyapata kutoka kwa wazee kuhusu matibabu, nashauri Halmashauri zote
nchini ziige mfano wa Wilaya ya Kilindi. Kama Kilindi wameweza kwa nini
wengine washindwe.
Ndugu Wananchi;
Katika
mikoa hii miwili nilipokea taarifa za kutia moyo kuhusu juhudi za
wananchi na Serikali katika kupanua fursa za elimu. Vijana wengi wenye
umri wa kujiunga na shule za msingi wanafanya hivyo na wale wote
wanaofaulu mtihani wa darasa la saba wanapata fursa ya kwenda sekondari.
Hatuna tena tatizo la fursa. Pamoja na mafanikio hayo mazuri, taarifa
za wanafunzi wengi kushindwa kumaliza elimu ya msingi na sekondari,
zimenishtua na kunisikitisha sana.
Katika
Mkoa wa Tanga kwa mfano, kati ya wanafunzi 50,921 walioanza darasa la
kwanza mwaka 2007 , ni wanafunzi 41,017 tu ndiyo waliofanya mtihani
mwaka 2013. Hivyo basi, wanafunzi 9,904 ambao ni sawa na asilimia
19.4 hawakumaliza elimu ya msingi. Kwa upande wa sekondari, katika mkoa
wa Ruvuma, kwa mfano, kati ya wanafunzi 18,892 walioanza kidato cha
kwanza mwaka 2010 ni wanafunzi 9,968 sawa na asilimia 52.76 ndiyo
waliofanya mtihani wa kidato cha nne. Hivyo basi, wanafunzi 8,924 sawa
na asilimia 47.2 hawakumaliza elimu ya sekondari. Taarifa za namna hii
nilizipata pia katika ziara zangu ya Mikoa ya Kagera, Geita na Simiyu.
Nina kila sababu ya kuamini kuwa hali ni hiyo hiyo kwa Mikoa mingine
mingi nchini. Kwa kweli kiwango hiki cha wanafunzi wanaoshindwa kumaliza
elimu ya msingi na sekondari ni kikubwa mno. Kinanisikitisha sana,
hakikubaliki na hakiwezi kuachwa kiendelee.
Ndugu Wananchi;
Kwa
maoni yangu wazazi, walimu na viongozi wanao wajibu maalumu wa
kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanahudhuria masomo shuleni tangu
wanapoanza mpaka wanapomaliza masomo yao. Huu ni wajibu wa lazima na
siyo hiari. Ni wajibu wa kisheria. Kwa hiyo, nimeagiza kwamba, wazazi,
walimu, Maafisa Elimu wa Wilaya wa Msingi na Sekondari na Kamati husika
katika Halmashauri zote nchini ziwajibike ipasavyo kuhakikisha kuwa
utoro mashuleni unakomeshwa. Ajenda ya mahudhurio shuleni iwe ni ya
kudumu katika vikao vyote vya Halmashauri.
Kuanzia
sasa Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule ni lazima watoe taarifa za
mahudhurio ya wanafunzi kwa Maafisa Elimu wa Wilaya kila miezi mitatu.
Maafisa Elimu wa Wilaya nao watalazimika kutoa taarifa kwenye vikao vya
Halmashauri mwezi mmoja baada ya kupokea taarifa hizo. Halmashauri
hazina budi kuchukua hatua stahiki za kijamii na kisheria kuhakikisha
kuwa watoro wanarudi shuleni. Wazazi wa watoto hao au mtu ye yote
atakayebainika kuhusika na utoro huo abanwe ipasavyo.
Sheria
ya Elimu ya 1978 ipo, itumieni kwa ukamilifu kulitatua tatizo hili.
Haipendezi kusubiri mpaka miaka saba kwa wanafunzi wa shule ya msingi au
miaka minne kwa wanafunzi wa sekondari ipite ndipo taarifa za utoro kwa
wanafunzi zitolewe au zijulikane. Lazima ufuatiliaji wa mahudhurio uwe
wa mara kwa mara ili hatua za kuzuia ziweze kuchukuliwa mapema.
Ninawataka viongozi wa TAMISEMI, Mikoa na Wilaya kuchukua hatua stahiki
kudhibiti tatizo hili la utoro na watoto wengi kutokumaliza masomo.
Litarudisha nyuma maendeleo ya taifa.
Umeme Vijijini
Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa
mkoani Ruvuma nimezindua ujenzi wa miradi mingi ya umeme vijijini. Kwa
mujibu wa miradi hiyo vijiji 309 vitapatiwa umeme kati ya vijiji 509 vya
Mkoa huo vinavyohitaji umeme. Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi
za dhati kwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospiter Muhongo na
viongozi wenzake, viongozi na wafanyakazi wa Wakala wa Umeme Vijijini
(REA) pamoja na TANESCO kwa kazi kubwa na nzuri waifanyayo ya kufikisha
umeme vijijini. Kwa kweli ni mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu
suala la umeme vijijini kupewa msukumo mkubwa kiasi hiki, kwani
kinachofanyika Ruvuma kipo nchi nzima. Nawaomba wananchi wanaofikishiwa
umeme wautumie. Hata gharama za kuunganisha umeme zimepunguzwa makusudi,
ili watu wengi waweze kumudu kuingiza umeme majumbani na kwenye
shughuli za kichumi na huduma.
Mchakato wa Katiba Mpya
Ndugu Wananchi;
Kama
tujuavyo, Bunge Maalum la Katiba lililoahirishwa tarehe 25 Aprili, 2014
kupisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la
Wawakilishi kushughulikia bajeti za Serikali husika, litakutana tena
tarehe 5 Agosti, 2014 kuendelea na kazi yake ya kutunga Katiba Mpya. Kwa
vile Bunge Maalumu la Katiba halikuweza kumaliza kazi yake ndani ya
siku 70 zilizotengwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
nimeliongezea Bunge hilo siku 60 kwa ajili ya kukamilisha kazi yake.
Nimefanya hivyo kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na Sheria hiyo hiyo.
Hatua Iliyofikiwa Kabla ya Kuahirishwa kwa Bunge
Ndugu Wananchi;
Itakumbukwa
pia kuwa, tarehe 16 Aprili, 2014, baadhi ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba hasa kutoka vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi walisusia
mjadala uliokuwa unaendelea Bungeni na kutoka nje. Wakati wanatoka
Bungeni, kazi kubwa ilikuwa imefanyika. Tayari Kamati zote 12 za Bunge
hilo zilikuwa zimekamilisha kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita za Rasimu
ya Tume. Sura hizo zinazungumzia utambulisho wa nchi na muundo wa
muungano. Kamati zote zilipiga kura ya kupitisha uamuzi wao kuhusu sura
hizo mbili. Kamati kadhaa ziliweza kupata theluthi mbili ya kura kwa
Wajumbe wa pande zote mbili za Muungano, jambo lililoonyesha dalili
njema kwamba Katiba mpya inaweza kupatikana.
Baada
ya hapo, taarifa ya kila Kamati iliwasilishwa kwenye Bunge zima. Kwa
mujibu wa Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, maoni ya wachache nayo
yaliwasilishwa. Kazi iliyokuwa inafuatia, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge
ni kwa Kamati ya Uandishi kukamilisha taarifa yake na kuiwasilisha
kwenye Bunge zima kwa ajili ya kujadiliwa. Baada ya Wajumbe kujadili
taarifa hiyo itafuatia kupiga kura ili kuamua kuhusu Sura hizo mbili.
Kama yalivyo masharti ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, uamuzi
utafanywa kwa theluthi mbili ya kura za kila upande wa Muungano wetu.
Sababu za Baadhi ya Wajumbe Kususia Bunge Maalumu la Katiba
Ndugu Wananchi;
Sote
tumewasikia Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba waliosusia vikao vya
Bunge hilo wakielezea sababu zilizowafanya watoke Bungeni. Walitoa
matamko kwenye vyombo vya habari na pia katika mikutano ya hadhara
waliyoiitisha na kuhutubia sehemu mbalimbali nchini. Sababu walizotoa
zimekuwa zikiongezeka na kubadilika kadri siku zinavyosonga mbele na
upepo wa kisiasa unavyokwenda.
Hivi
sasa wanazungumzia mambo mawili. Kwanza, kwamba Bunge Maalumu halina
mamlaka ya kuifanyia mabadiliko yo yote Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa
na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa maoni yao, kazi ya Bunge Maalumu
la Katiba ni kujadili na kupitisha tu Rasimu ya Katiba ya Tume na siyo
kubadili cho chote. Pili, wametoa sharti la wao kurudi Bungeni ni
kuhakikishiwa kwamba, kitakachojadiliwa Bungeni ni Rasimu ya Tume. Bila
ya sharti hilo kukubaliwa, wamesisitiza kutorudi Bungeni.
Mamlaka ya Bunge Maalum la Katiba
Ndugu Wananchi;
Mimi
nimehusika katika kubuni wazo la kuwa na mchakato wa kuandika Katiba
Mpya, na katika maandalizi ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ya
kuongoza na kuendesha mchakato huo. Kwa kweli sikumbuki wakati wo wote
katika vikao vya Baraza la Mawaziri kujadili Rasimu ya Muswada wa Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba tulipozungumzia Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba kuwa haiwezi kufanyiwa marekebisho na Bunge Maalumu la Katiba.
Mimi
siyo Mwanasheria na hivyo nakiri kwamba naweza kuwa na upungufu katika
kuelewa maana ya baadhi ya maneno ya kisheria. Hata hivyo, sikumbuki
kuwepo kwa kifungu cho chote katika Sheria kinachosema kuwa Bunge
Maalumu la Katiba halina mamlaka hayo. Tangu tulipoyasikia maneno hayo
yakisemwa nimeuliza nithibitishiwe ukweli wa madai hayo bado sijaambiwa
vinginevyo. Kama ukweli huo upo naomba anisaidie. Badala yake naambiwa
kuwa maneno yaliyotumika katika Sheria haiakisi dhana inayotolewa kuwa
kazi ya Bunge Maalum la Katiba ni kubariki Rasimu na siyo kufanya
vinginevyo. Nimeambiwa kuwa sheria inasemaTume itaanda Rasimu ya Katiba
na Bunge Maalum la Katiba litatunga Katiba iliyopendekezwa.
Ndugu Wananchi;
Tarehe
30 Desemba, 2010, nilipozungumzia dhamira yangu ya kuanzisha mchakato
wa kuandika Katiba Mpya nilieleza wazi nia ya kuwepo kwa uwakilishi
mpana wa Watanzania katika mchakato huo. Ndiyo maana katika Sheria
tukaweka ngazi nnekatika mchakato wa kutunga Katiba. Ngazi ya kwanza
ikiwa ya wananchi kutoa maoni yao juu ya kila wanachotaka kijumuishwe
katika Katiba ya nchi yao. Ngazi ya pili, ni ya wananchi kupitia
wawakilishi wao katika Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na Mabaraza ya
Kitaasisi kutoa maoni yao kuhusu Rasimu ya kwanza ya Katiba
iliyotayarishwa na Tume.
Ngazi
ya tatu inajumuisha wawakilishi wa wananchi waliopo kwenye Mabaraza ya
Kutunga Sheria ya Sehemu zetu mbili za Muungano, yaani Bunge la Jamhuri
ya Muungano na Baraza la Wawakilishi, wakichanganyika na Wawakilishi wa
makundi mbalimbali ya jamii ya Watanzania kutoka pande zote mbili za
Muungano. Hawa ndio wanaounda Bunge Maalumu la Katiba, lenye jukumu la
kutunga Katiba inayopendekezwa.
Mamlaka
ya kutunga Katiba kwa mila na desturi za Mabaraza ya Kutunga Sheria ni
uwezo wa kurekebisha, kubadili, kufuta na hata kuongeza
kilichopendekezwa. Ingekuwa kilichokusudiwa ni kubariki tu lisingetumiwa
neno la kutunga Katiba. Hali kadhalika, lisingewepo sharti la kupiga
kura na msisitizo wa kupata theluthi mbili kwa kila upande wa Muungano.
Aidha, kama ingekuwa jukumu la Bunge Maalumu ni kubariki tu Rasimu
lisingepewa siku 70 za kazi na Rais kupewa mamlaka ya kuongeza siku
zaidi kadri aonavyo yeye inafaa.
Ngazi
ya nne na ya mwisho, tuliweka kura ya maoni ya wananchi kukubali au
kukataa Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba. Kama ingekuwa
Rasimu ya Tume haiwezi kubadilishwa hata nukta kwa nini basi tuweke
kura ya maoni ya kuwahusisha wananchi wote?
Ndugu Wananchi;
Tulizibuni
ngazi hizi nne kwa dhana kwamba kile ambacho hakikuonekana au
hakikuwekwa sawa katika ngazi moja kitaonekana na kurekebishwa katika
ngazi inayofuata katika ngazi zile tatu za mwanzo. Na, iwapo Katiba
iliyotungwa haitawaridhisha wananchi wanayo haki ya kuikataa. Kwa
kufanya hivyo, wananchi ndiyo waliopewa turufu ya mwisho.
Ndugu wananchi;
Kwa
kweli, napata shida kuelewa mkanganyiko unatoka wapi na hasa wale
wanaoongoza kuhoji mamlaka ya Bunge Maalumu kuwa ni wale wale waliotunga
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba tena hatua kwa hatua. Nashangazwa zaidi
ninapoona wale wale waliotunga Kanuni za Bunge Maalumu ndiyo wanaoongoza
kuhoji uhalali wa kile walichokitunga.
Kanuni
za Bunge Maalumu la Katiba, Ibara ya 33 (8) inasema: Nanukuu: “Wakati
wa mjadala, Mjumbe yoyote anaweza kutoa mapendekezo ya marekebisho,
maboresho au mabadiliko yaliyomo katika Sura za Rasimu ya Katiba
zinazojadiliwa kwa utaratibu ufuatao: (a) Ikiwa ni marekebisho,
maboresho au mabadiliko yanayobadilisha jambo la msingi, au
yanayobadilisha maudhui ya Ibara, mapendekezo ya marekebisho yatapelekwa
kwa maandishi kwa Katibu siku moja kabla ya mjadala wa Ibara husika.
(b) Ikiwa ni marekebisho madogo, ambayo hayabadili msingi au maana,
mapendekezo ya marekebisho yatawasilishwa na mjumbe wakati wa mjadala
baada ya kupata ruhusa ya Mwenyekiti”. Mwisho wa kunukuu.
Kanuni
hii ilipotungwa, Wajumbe wote wa Bunge Maalumu pamoja na wale ambao
baadae walisusia vikao vya Bunge walikuwepo Bungeni na walishiriki
kuipitisha. Tena basi, baadhi yao walikuwa Wajumbe wa Kamati ya Kanuni
iliyopendekeza Kanuni hizo. Unapowaona watu wale wale sasa wanakuwa
vinara wa kuhoji mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba, unajiuliza maswali
mengi kuhusu watu hao bila ya kupata majibu yaliyo sahihi na kutosheleza
akili na ufahamu wetu.
Ndugu Wananchi,
Unaposoma
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kanuni za Bunge Maalumu, hii ni
dhahiri kwamba wote walikuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mamlaka ya Bunge
Maalumu ya kujadili Rasimu iliyoandaliwa na Tume na kutunga Katiba
inayopendekezwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura.
Kinachojadiliwa Bungeni ni Rasimu ya Tume
Ndugu Wananchi;
Yapo
madai yanayotolewa na kuenezwa na Wajumbe waliosusia Bunge Maalumu la
Katiba kwamba kinachojadiliwa Bungeni siyo Rasimu ya Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, ndiyo maana basi wanaweka sharti la kujadiliwa Rasimu ya Tume
ya Jaji Warioba ndipo warudi Bungeni. Madai haya nayo yananipa taabu
kuyaelewa. Ndugu zetu hawa walishiriki siku zote 19 za Kamati 12
zilipokutana kujadili Sura yaKwanza na ya Sita za Rasimu ya Tume.
Halikadhalika. walikuwepo na kushiriki kwa ukamilifu wakati taarifa za
Kamati, tangu ya Kwanza mpaka ya 12,zilipowasilishwa kwenye Bunge zima.
Aidha, na wao walishiriki kutoa maoni ya wachache kwa dakika 20 na kutoa
ufafanuzi kwa muda wa dakika 30 kwa kila Kamati. Haya maneno ya sasa
kwamba kinachojadiliwa Bungeni siyo Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba bali
nyingine kabisa ambayo wanadai eti ni ya CCM yanatoka wapi.
Mimi
nadhani kuwa huenda katika Kamati kumefanyika marekebisho kwenye Rasimu
ambayo hayakuwapendeza. Kama hivyo ndivyo, wawe wakweli kuhusu jambo
hilo kuliko kusema mambo yasiyowakilisha ukweli halisi wa Rasimu
inayojadiliwa. Matokeo yake ni kuwafanya wafuasi wao na wapenzi wao na
hata watu wengine waamini kuwa kinachojadiliwa siyo Rasimu ya Tume ya
Jaji Warioba bali nyingine tena ni ya CCM. Jambo hilo si kweli na
wenyewe wanajua kwamba si kweli ila sijui kwa nini wameamua kupotosha
ukweli.
Ndugu Wananchi;
Kinachonishangaza,
zaidi ni kwamba, kama hawakuridhishwa na yaliyofanyika, kwa nini
wasingetumia mifumo waliyojitengenezea wenyewe kwenye Kanuni kumaliza
tofauti zao? Kanuni zinaelekeza kuwa mambo wasiyoridhika nayo yajadiliwe
kwenye Kamati ya Mashauriano na Maridhiano. Ukiacha mifumo ya
maridhiano ndani ya Bunge ukaenda nje kwa wananchi au vyombo vya habari
na mitandao si jawabu la tatizo.
Ndugu Wananchi;
Ndiyo
maana nashawishika kuunga mkono wale wote wanaowasihi Wajumbe wa
CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na wengine warejee Bungeni. Watumie mifumo
maalum ya Bunge iliyowekwa na Kanuni kutafuta maridhiano. Hali
kadhalika, wasichoke kuwa na mawasiliano na vyama vingine vya siasa na
hasa CCM kutafuta maelewano. Mimi niko tayari kusaidia pale watakapoona
inafaa kufanya hivyo kama ambavyo nimekuwa nikifanya ziku za nyuma.
Nililolisema
mwanzoni kabisa mwa mchakato na nalirudia tena leo kwamba, ili tuweze
kufanikiwa kupata Katiba Mpya ambayo sote tunaitaka, maelewano baina ya
wadau wakuu wa kisiasa ni jambo lisilokuwa na badala yake. Vinginevyo
kupata theluthi mbili kwa pande zote mbili za Muungano haitawezekana.
Ndiyo maana nampongeza sana Msajili wa Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Jaji
Francis Mutungi, kwa uamuzi wa kuvikutanisha vyama vinne vikuu vya siasa
kujadili namna ya kuondoa mtihani uliopo sasa katika mchakato wa
Katiba.
Ombi
langu kwa viongozi wa vyama hivyo ni kuitumia vyema fursa ya
majadiliano kuukwamua mchakato kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake.
Hali kadhalika nampongeza sana Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba,
Mheshimiwa Samwel Sitta, kwa kuitisha kikao cha Kamati ya Mashauriano na
Maridhiano. Bahati mbaya ni kwamba Wajumbe wa vyama vilivyosusia Bunge
Maalumu hawakushiriki. Ni matumaini yangu kuwa Mheshimiwa Sitta hatokata
tamaa kuendeleza juhudi za mashauriano na kwamba katika vikao vijavyo
na wenzetu hawa watashiriki.
Ndugu Wananchi;
Hivi
karibuni kumekuwepo pia madai yanayoelekeza lawama kwangu. Kwanza
nalaumiwa eti kuwa mambo yalikuwa yanaenda vizuri mpaka pale nilipotoa
hotuba ya ufunguzi wa Bunge Maalumu ndipo yalipoharibika. Pili nalaumiwa
kwamba nawezaje kuikana Rasimu ya Katiba ambayo na mimi ni mmoja wa
watu waliotia sahihi katika Rasimu hiyo.
Niruhusuni
nianze na hili la pili. Nadhani ndugu zetu wanaotoa madai haya
yameitafsiri isivyo sahihi yangu katika Gazeti la Serikali lililotangaza
rasmi Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa
mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba baada ya Tume kumaliza kazi
yake ya kuandika Rasimu ya Katiba, Rais wa Jamhuri ya Muungano amepewa
kazi tatu kufanya. Kwanza, kupokea Rasimu hiyo na Taarifa ya Tume kutoka
kwa Mwenyekiti jambo ambalo lilifanywa tarehe 30 Desemba, 2013. Pili,
amepewa kazi ya kuitangaza rasmi Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume kwa
watu wote kuiona na kuisoma ndani ya siku 30. Alipewa sharti la
kuitangaza katika Gazeti la Serikali na vyombo vingine vya habari. Hili
nalo lilifanywa hivyo tarehe 22 Januari, 2014.
Ndugu Wananchi;
Katika
kutangaza katika Gazeti la Serikali sharti linamtaka anayetangaza
ajitambulishe kuwa yeye ni nani na atie sahihi yake. Kwa kufanya hivyo,
hakumfanyi yeye kuwa naye ni mhusika na maudhui ya kila
kinachopendekezwa na Tume. Sahihi zilizomo ndani ya Rasimu na Taarifa ya
Tume ni za Wajumbe wa Tume, kamwe sahihi ya Rais haimo hivyo hawezi
kulaumiwa kuwa anaikana sahihi yake. Yeye ametimiza wajibu wake wa
kutangaza, akaiweka hadharini kwa umma wa Watanzania kuiona na kusoma
Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume vilivyotayarishwa na kutiwa sahihi
na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kazi ya tatu ni kuitisha
Bunge Maalumu ambayo nayo imekamilika tangu tarehe 18 Februari, 2014.
Ndugu Wananchi,
Jambo
lingine linalofanana na hilo ni yale madai kwamba nilikuwa napata
taarifa ya maendeleo ya mchakato ndani ya Tume mara kwa mara, iweje leo
nitoe maoni tofauti kama niliyoyatoa katika hotuba yangu kwenye Bunge
Maalumu. Ni kweli kabisa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba, Makamu wake, Mheshimiwa Jaji Agustino
Ramadhani na Mheshimiwa Dkt. Salim Ahmed Salim wamekutana na mimi kwa
nyakati mbalimbali kuzungumzia mwenendo wa mchakato. Lakini, hayakuwa
mazungumzo ya kina kuhusu nini kiwe vipi katika maudhui na mapendekezo
ya Tume. Ukweli ni kwamba Rasimu zote mbili nilizipata mara ya kwanza
nilipokabidhiwa rasmi, tena kwa uwazi. Napenda watu wasijenge dhana kuwa
nilipewa Rasimu na kuisoma kabla ya kukamilika na hivyo nilitoa maoni
yangu. Tume hii ilikuwa huru na niliiacha iwe hivyo. Sikuiingilia kwa
namna yo yote ile kupenyeza mambo ninayotaka yawemo. Kuthibitisha
dhamira yangu ya kutaka Tume iwe huru katika kufanya kazi zao hata pale
waliponitaka nitoe maoni niliwaomba tusifanye hivyo ili nisiwakwaze
katika kufanya kazi zao, wakapata taabu ya kuwianisha wanayofikiria na
mawazo yangu.
Ndugu Wananchi;
Kuhusu
madai kwamba mambo yalikuwa yanakwenda vizuri na kwamba hotuba yangu
iliyavuruga, napenda kusema wazi kuwa lawama hizo hazina ukweli wo wote.
Ni madai yasiyokuwa na msingi. Kwani mimi hasa siku ile nilifanya lipi
la ajabu. Ukweli ni kwamba nilisema yale yale ambayo Tume yenyewe
imeyasema katika Rasimu ya Katiba na Taarifa za Tume. Niliyoyasema
kuhusu malalamiko ya watu wa pande zetu za Muungano na uzuri na
changamoto za miundo ya Serikali mbili na Serikali tatu ni yale yale
yaliyomo kwenye taarifa za Tume. Nimetumia takwimu zile zile za Tume.
Pengine kilichoonekana kuwa kibaya ni jinsi nilivyozifasiri taarifa hizo
na mapendekezo ya Tume.
Jambo
lingine ambalo nimelifanya ni kutoa maoni yangu kuhusu baadhi ya
vipengele vya Rasimu hususan uandishi na dhana mbalimbali zilizokuwamo.
Silioni kosa langu kwa kufanya hivyo, kwani Rasimu imetolewa hadharani
kwa watu kuijadili. Na mimi kama raia ninayo haki ya kufanya hivyo kama
wafanyavyo wengine. Kwa nini nilaumiwe kwa kutumia haki yangu hiyo.
Lakini,
pia mimi ndiye Rais wa nchi yetu, ninayo dhamana ya uongozi na ulezi wa
taifa letu. Itakuwaje kwa jambo kubwa la hatma ya nchi yetu
nilinyamazie kimya. Watanzania wangeshangaa na wangekuwa na haki ya
kuhoji Rais wao ana maoni gani. Bahati nzuri nilitoa maoni yangu mahali
penyewe hasa, na kwa uwazi, kwenye Bunge Maalumu la Katiba. Hata hivyo,
ni muhimu kusisitiza kuwa namna nilvyotoa maoni yangu sikuwa natoa
maagizo wala kushurutisha, ndiyo maana kila wakati niliwakumbusha
Wajumbe kuwa mamlaka ya uamuzi ni yao. Yangu yalikuwa maoni tu
wanahiyari ya kuyakubali au kuyakataa. Niliwataka Wajumbe wasome na
kuielewa vyema Rasimu. Nilisema wasome sura kwa sura, mstari kwa mstari
na neno kwa neno. Niliwaomba wajiridhishe kuhusu uandishi na dhana
mbalimbali. Nilitoa mifano ya mambo yahusuyo uandishi ambayo ni vyema
wayatazame. Pia nilitoa mifano ya dhana ambazo niliwasihi wajiridhishe
juu ya kufaa kwake kuwepo.
Kuhusu
muundo wa Serikali tatu, nilieleza wazi kuwa sina tatizo nao kama ndiyo
matakwa ya Watanzania. Lakini, nilieleza hofu yangu kuhusu mapendekezo
ya Tume na kuwataka Wajumbe wafanye kazi ya ziada kuondosha udhaifu
iwapo wataukubali muundo unaopendekezwa. Nilieleza nia yangu ya kutaka
tuwe na Serikali ya Muungano yenye ukuu unaoonekana, yenye nguvu ya
kuweza kusimama yenyewe, inayoweza kuwa tegemeo kwa nchi Washirika,
Serikali isiyokuwa tegemezi wala egemezi kwa nchi washirika na ambayo
inavyo vyanzo vya uhakika vya mapato. Hivi kwa kutoa ushauri huo kwa
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba inageuka kuwa nongwa. Kwa kweli
sielewi lawama ni ya nini?.
Naamini
sistahili lawama bali pongezi kwa kuwa muwazi na kutoa ushauri wa
msingi ambao utasaidia nchi kupata Katiba nzuri inayojali maslahi ya
watu wa nchi yetu na ya nchi zetu mbili zilizoungana miaka 50
iliyopita.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Mwisho,
ni maoni yangu ya dhati kuwa mgogoro uliopo sasa katika mchakato wa
Katiba hauna sababu ya kuendelea kuwepo. Naamini hayo yote ambayo
Wajumbe wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi wanayalalamikia yanaweza
kushughulikiwa kwa ukamilifu katika mifumo ya Bunge Maalumu la Katiba
iliyotengenezwa na Wajumbe wote na wao wakiwemo. Nawasihi waitumie. Hali
kadhalika, kwa kupitia mazungumzo wanayofanya na wenzao wa Chama cha
Mapinduzi wanaweza kutengeneza nguvu ya pamoja kutatua changamoto za
sasa na zitakazojitokeza baadaye. Kilicho muhimu ni kwa pande zote kuwa
na dhamira ya dhati ya kutoka hapa tulipo sasa. Kama utashi wa kisiasa
upo kwa kila mmoja wetu, hilo ni jambo linalowezekana kabisa. Narudia
kuahidi utayari wangu wa kusaidia kadri inavyowezekana tusonge mbele.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni sana kwa kunisikiliza.