Biashara ya muziki Tanzania imeendelea kupanuka kwa kiasi kikubwa, na
wasanii wenye hits, majina, connection, bahati na sababu zingine
wameendelea kuingiza fedha nyingi kutokana na muziki wao.
Njia kubwa na za uhakika zinazowapatia mapato wasanii ni pamoja na
malipo ya show, malipo ya ringtones, endorsements (mfano kuwa mabalozi
wa brands mbalimbali na kufanya matangazo) na wengine kupata kipato
kupitia biashara walizozianzisha.
Kama njia kubwa zingine mbili za kuwaingizia kipata wasanii wengi
duniani zingefanikiwa nchini, wasanii wetu wangekuwa mbali zaidi. Njia
hizo ni mauzo ya albam za muziki na malipo ya mirahaba kutokana na
matumizi ya nyimbo zao kwenye kumbi za starehe na kwenye vituo vya radio
au TV.
Licha ya kuwepo kasoro hizo, bado Bongo Flava imebadilisha maisha ya wasanii wengi.
Bongo5 imejitahidi kukusanya kadri iwezavyo, data za uhakika kutoka kwa
watu walio karibu na wasanii kadhaa wa Tanzania kutaka kufahamu, kiasi
walichoingiza, malipo waliyoyapata mwaka huu na data zingine zingine,
kuandaa orodha hii ya wasanii 10 walioingiza fedha nyingi zaidi mwaka
2013.
Wafuatao ni 10 waliongiza fedha nyingi zaidi mwaka 2013.
1. Diamond Platnumz
1. Diamond Platnumz
Hakuna ubishi kuwa, mwaka 2013 Diamond Platnumz ndiye msanii aliyeingiza
fedha nyingi zaidi. Pesa nyingi ya Diamond imetokana na malipo ya show
zake za ndani na nje ya nchi. Kwa uhakika, mwaka huu pekee, Diamond
amefanikiwa kuingiza takriban shilingi bilioni 1.
Kwa show za ndani peke yake, Diamond hutoza si chini ya shilingi milioni
10 ama 15 na kila wiki hufanya show zaidi ya 2. Hivyo tangu mwaka
uanze, Diamond amekuwa akiingiza shilingi milioni 40 kila wiki. Tour za
nje alizofanya mwaka huu ni pamoja na zile za Uingereza ambako alifanya
show kwenye miji mitatu, show ya Burundi na Congo, show mbili za Kenya
(Nairobi na Mombasa), show ya nchini Comoro ambako alilipwa si chini ya
dola 30,000 na show ya Malaysia wiki iliyopita.
Kwa upande wa show za hapa nyumbani ambazo ni nyingi mno zisizo na
idadi, ukiachana na zile za kawaida, Diamond aliingiza shilingi milioni
40 kwenye show 4 za Kili Music Tour ambapo kila show alilipwa shilingi
milioni 10. Ndiye msanii aliyelipwa fedha nyingi zaidi kwenye ziara
hiyo.
Pia amefanya show kadhaa za Fiesta 2013, show za promotion za Tigo na
makampuni mengine, Tamasha la Matumaini, show ya Tulizana Tuko Wangapi
ya Leaders Club, show yake na Nay wa Mitego (Dar Live na Maisha Club).
Mwezi February 16 mwaka huu, Diamond alifanya show jijini Arusha ambayo
kiingilio chake kilikuwa ni shilingi 150,000 ndani ya Club Safari na
ukumbi kufurika.
Miezi kadhaa iliyopita pia hitmaker huyo wa ‘Number 1’ ameshaalikiwa
kwenye show corporate kuburudisha wafanyakazi wa benki na taasisi
zingine pamoja na watu binafsi na zote hizo zimemuingizia fedha nyingi.
Pamoja na show, Diamond amekuwa akiingiza fedha nyingi zaidi kwenye
malipo ya ringtones ambapo kila baada ya miezi mitatu amekuwa akiingiza
si chini ya shilingi milioni 20. Kwa mujibu wa Push Mobile, akaunti ya
Diamond kwenye kampuni hiyo ndio inayoingiza fedha nyingi kuliko msanii
mwingine yeyote wa Bongo Flava.
Mkataba exclusive alioingia na kampuni ya simu ya Vodacom kuuza wimbo
wake mpya My Number One kama muito wa simu, umezidi kumpandisha juu na
ikidaiwa kuwa mkataba huo ni wa mamilioni ya shilingi.
Ikumbukwe pia, Diamond ni balozi wa Cocacola. Mkataba huo ambao
haijajulikana umemuingizia shilingi ngapi, lakini ni fedha inayoweza
kuwa si chini ya shilingi milioni 100.
Diamond ni miongoni mwa wasanii wengine 23 wa Afrika akiwemo Lady Jaydee kwenye mradi mkubwa wa Cocacola wa Coke Studio Africa.
2. Lady Jaydee
Huwezi amini, vuguvugu la Anaconda limemsaidia Jaydee si tu kukusanya
mashabiki wengi zaidi, bali pia limempa fedha nyingi mno. Zaidi ya
tiketi 3,500 zilinunuliwa kwenye show yake ya mwezi June ya Miaka 13 ya
Muziki na kuingiza takribani shilingi milioni 100. Haikuishia hapo,
albam yake Nothing But The Truth ilinunuliwa kwa kiasi kikubwa na
kumfanya kuwa msanii pekee wa Bongo Flava anayeendelea kufurahia mauzo
ya albam zake.
Hits zake mbili, Joto Hasira na Yahaya kutoka kwenye albam yake hiyo,
zimebadilisha maisha yake na kumfanya kuwa mwanamuziki mwenye show
nyingi zaidi pia. Lady Jaydee ametumbuiza kwenye karibu show zote za
Kili Music Tour ambako ameingiza shilingi milioni 25.
Mwaka huu pia Lady Jaydee amefanya show nyingi kubwa ikiwemo ile ya
uzinduzi wa filamu ya Lulu, Foolish Age, show yake kwenye Miss Tanzania
2013, Family Day Show ya Arusha iliyofanyika Eid Pili, Anaconda Show
iliyofanyika Triple A na nyingine iliyofanyika Snow View Hotel. Akiwa
Arusha pia, Lady Jaydee aliuza kopi za albam yake kama njugu pamoja na
tiketi za Anaconda zilizouzwa kwa shilingi 15,000 kila moja.
June mwaka huu pia, Lady Jaydee alitumbuiza kwenye semina ya kuwezesha
wanawake kuondokana na njaa na umaskini, iliyofanyika chini ya mfuko wa
fursa sawa kwa wote chini ya mama Anna Mkapa. Biashara yake ya Nyumbani
Lounge, imeendelea kufanya vizuri pia kwa kupata wateja wengi wanaoenda
kupata chakula, vinywaji na burudani kutoka kwa bendi yake ya Machozi.
Bado anaingiza fedha kupitia udhamini wa Airtel kwenye show yake ya TV
ya Diary of Lady Jaydee. Msanii huyo ambaye jina lake ni Judith Wambura
pia miongoni mwa wasanii 24 wa bara la Afrika waliochukuliwa kwenye
mradi wa Coke Studio Africa wa kampuni ya Cocacola unaoendelea jijini
Nairobi Kenya.
Coke Studio Africa – the new, exciting music show featuring incredible live performances by the very best in Africa
3. AY
Humsikii sana rapper huyu kwenye show za Tanzania. Tofauti na wasanii
wengine, fedha anazoingiza AY zinatokana zaidi na endorsements na
biashara zake anazofanya. Pesa nyingi alizoingiza zimetokana na mkataba
wa mwaka mmoja na Airtel wa ubalozi uliokamilika mwezi May mwaka huu.
Katika ubalozi huo wa Airtel Africa, AY aliungana na wasanii wengine
watatu wa Afrika ambao ni pamoja na Papa Wemba, Tuface na Daddy Owen wa
Kenya. Katika mkataba huo AY alilipwa dola za Kimarekani 80,000 ambazo
ni zaidi ya shilingi milioni 129.
Rapper huyo wa ‘Machoni Kama Watu’ ni balozi pia wa bia ya Peroni ya
Italia na kupitia mkataba huo, AY ameingiza mkwanja mwingi. AY pia ni
mwanzilishi mwenza wa kipindi cha Mkasi kinachoendeshwa na Salama Jabir.
Kipindi hicho kina wadhamini wawili, Cocacola na Airtel na hivyo
kupitia mgawanyo wa mapato, AY amekuwa akiingiza pia fedha ya kutosha.
AY ni CEO wa kampuni ya Unity Entertainment inayojihusisha na kuandaa
show, matangazo, kuleta wasanii wa nje na mambo mengine. Mwaka huu
pekee, ikishirikiana na kampuni ya SK Entertainment, kampuni yake
imeandaa show kibao zikiwemo zile zilizofanyika Elements Lounge ambapo
Avril, Prezzo, Huddah Monroe na J-Martins wamewahi kuhudhuria.
Maisha ya kawaida ya rapper huyu ndio yanayowafanya watu wengi wasijue
ukubwa wa kile anachokiingiza. Macho yake ameyaelekeza zaidi kwenye
uwekezaji na anawekeza haswaa. Kuna tetesi kuwa, AY anajenga ghorofa
lake maeneo ya Kigamboni jijini Dar es Salaam. Anasemekana kuwekeza pia
mkoani Mtwara alikonunua ardhi ya kutosha. Mungu ndio anajua ni wapi
alikowekeza tena.
4. Ommy Dimpoz
Ommy Dimpoz ambaye kwa sasa yupo kwenye ziara ya muziki nchini Marekani
ameingiza fedha zake nyingi kupitia show alizofanya. Ziara zake za Ulaya
na Marekani pekee zimemuingizia dola 50,000 ambazo ni sawa shilingi
milioni 81.
Tangu aachie wimbo wake mpya Tupogo, tayari Ommy ameshaingiza shilingi
milioni 50. Kwenye show yake ya hivi karibuni ya Tupogo Night
iliyofanyika Club Billicanas, Ommy alipeleka nyumbani shilingi milioni
10 baada ya kukata gharama zote. Watu 1,770 walihudhuria show hiyo.
Show yake ya Burundi ya mwanzoni mwa mwezi uliopita ilimuingizia staa
huyo shilingi milioni 30. Ommy hutoza si chini ya shilingi milioni 7 kwa
show na kwa mwezi, amekuwa na uhakika wa kufanya show tatu ama nne za
ndani bila kusahau show za Kili Music Tour.
Hivi karibuni kwenye segment ya Tell it All ya Bongo5, Ommy alifunguka
kuwa makampuni mengi yamekuwa yakimfuata kumpa endorsements lakini
msimamo wake wa kutaka kulipwa fedha ya uhakika imemfanya azikatae
nyingi lakini yupo mbioni kupata deal kubwa. Mpaka sasa Ommy anajenga
nyumba mbili kwa mpigo zenye thamani ya shilingi milioni 250 hadi
zilipofikia. Tayari ana viwanja vingine viwili anavyotaka kuangusha
mijengo mingine. Hivi karibuni pia atakuja na clothing line yake ya PKP.
5. Madee
Hii inaweza kuwa surprise kwa wengi lakini Madee ni mfano tosha wa jinsi
single moja inavyoweza kubadilisha maisha ya msanii. Tangu atoe single
yake, Sio Mimi, Madee ameshaingiza si chini ya shilingi milioni 200.
Mwaka huu ameshafanya show 10 za kampeni ya Tigo ambapo kila moja
alilipwa shilingi milioni 3, show 15 za Airtel kwa kiwango hicho hicho.
Alifanya show mbili za kampeni za Coca Cola, ile ya uzinduzi wa Coke
Zero na Cocacola Bonanza Mlimani City. Bado ameendelea kufanya show za
Fiesta 2013. Madee pia alikuwa miongoni mwa wasanii waliotumbuiza kwenye
show ya Fuse ODG iliyofanyika September 7 kwenye viwanya vya ustawi wa
jamii jijini Dar es Salaam.
6. Mwana FA
Mwanzoni mwa mwaka huu, Hamis Mwinjuma aka Mwana FA alikuwa msanii wa
tatu miongoni mwa wasanii waliongiza fedha nyingi kupitia malipo ya
miito ya simu, RBT ambapo aliingiza shilingi milioni 18. Alifanya show
mbili kwenye Kili Music Tour ambapo aliingiza si chini ya shilingi
milioni 7 pamoja na show kadhaa za Fiesta 2013.
Show yake ya The Finest ilimuingizia shilingi milioni 19. Hivi karibuni
alichukuliwa na kampuni ya Vodacom kuzunguka baadhi ya mikoa kwenye
kampeni yao na CCBRT kuhusiana na kukuza uelewa wa tatizo la Fistula na
kulipwa mkwanja kama balozi wa kampeni hiyo.
Mwaka huu FA amefanya matangazo kadhaa ya Vodacom. Hivi karibuni pia
aliingia kile kilichoonekana mkataba kama balozi wa simu za Samsung
Galaxy Tanzania japo haijulikani kama ulikuwa mkataba wa ubalozi kama
ilivyo mingine.
Mwana FA pia amefanya show za nje zikiwemo za Kenya na Afrika Kusini
aliyofanya siku ya Eid mwezi uliopita. Kama wasanii wengine pia, FA
ameingiza fedha nyingi kwa show za kawaida za hapa nyumbani na zile za
promotion.
7. Chege
Mwaka huu Chege peke yake alifanya show sita nje ya nchi ambazo kila
show alilipwa shilingi milioni 4. Akiwa na Temba ambao kwa pamoja hutoza
shilingi milioni 6, Chege amefanya show zaidi ya 30 zikiwemo zile za
Fiesta, za promotion mbalimbali na zile za kawaida.
Mwezi ujao yeye na Temba wataanza tour ya miezi mitatu barani Ulaya
ambapo show ya kwanza itakuwa nchini Sweden, October 5. Pamoja na hivyo,
Chege ana biashara ya salon.
8. Profesa Jay
Profesa Jay aliingiza shilingi milioni 20 za Kili Music Tour, alifanya
show kubwa ya Jose Chameleone April mwaka huu, show kibao za promotion
za makampuni, show ya kampuni ya IPP kwaajili ya Walemavu, Diamond
Jubilee mwezi January, na show zingine za kawaida za Dar na mikoani. Pia
nguli huyo wa rap ya Tanzania ameingiza fedha nyingi kupitia show
nyingi za Lady Jaydee.
Prof J amewekeza kwenye biashara ya salon ambayo tayari inafanya vizuri
na ameshafungua studio ya kurekodi muziki iliyopo kwenye hatua za mwisho
kuanza kazi. Jize aliingiza pia fedha kupitia kampeni ya magazeti ya
Mwananchi kwa kufanya matangazo na show za mikoani.
9. Nay wa Mitego
Tangu mwaka uanze, Nay wa Mitego ameshafanya show zaidi 20
zilizomuingizia si chini ya shilingi milioni 60. Show hizo ni pamoja na
zile za promotion za makampuni ya simu, show mbili za Muziki Gani, show
ya Kili Music Tour, show za Fiesta na zile za kawaida. Pia ana biashara
zake ambazo kwa pamoja humuingizia si chini ya shilingi milioni 4 kwa
mwezi.
10. Temba
Fedha nyingi alizoingiza Temba mwaka huu zimetokana na show walizofanya
pamoja na Chege. Ukitoa muziki, Temba pia ni mfanyabiashara na anamiliki
duka la vifaa vya ujenzi.
Credit: Bongo5