Wakati vyombo vya usalama vya Kenya vikitangaza kulidhibiti jengo lote la Westgate lililovamiwa na magaidi wanaodaiwa kuwa wa kundi la Al-Shabaab, baadhi ya watu waliojitoa muhanga na kufanikiwa kuokoa maisha ya wengine, wanaendelea kuibuka.
Hivi karibuni gazeti hili lilichapisha habari juu
ya askari wa Kikosi Maalumu cha Anga (SAS) cha Uingereza, aliyeweza
kuokoa zaidi ya watu 100 ndani ya jengo hilo.
Hivi karibu, baadhi ya vyombo vya habari vya Kenya
vimemnukuu pia Abdul Haji (38) ambaye ni raia wa kawaida aliyeweza
kufika ndani ya jingo hilo na kuokoa watu waliokuwa wametekwa na
wanamgambo hao wanaodaiwa kuwa wa Al Shabaab.
Gazeti la Daily Nation, limemnukuu kijana
huyo akisema alipata ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (SMS) kutoka kwa
kaka yake ukisomeka kuwa “Nimekwamba Westgate, nadhani kuna magaidi
wamevamia hapa, niombee”.
Kijana huyo ambaye asili yake ni Msomali, alisema
alipata sana hofu kutokana na ujumbe huo wa kaka yake kwani ilikuwa ni
wiki mbili tu tangu televisheni moja ya nchi hiyo kumtaja kaka yake huyo
kama mmoja wa watu anaowasaidia magaidi hao wa Al Shabaab.
Kijana huyo ambaye ni mtoto wa Seneta, Yusuf Haji
alisema hali hiyo ilimpa wasiwasi zaidi kwani tayari walishaanza kupata
vitisho kutoka kwa baadhi ya watu wakiamini kuwa kweli familia yake
wanawasaidia Al Shabaab.
Anasema baada ya ujumbe huo alikimbia mara moja na
kwenda katika jengo hilo la Westgate, na muda mfupi tu tangu magaidi
hao kuingia ndani ya jengo hilo na kuanza kuwafetulia watu risasi
alikuwa ameshawasili eneo hilo.
Haji ambaye ni mfanyabishara na baba wa watoto
wane wa kike, alisema aliamini kuwa magaidi hao walikuja kumfuata kaka
yake na baadaye familia nzima hivyo aliamua kujitoa muhanga ili kumuokoa
kaka yake na familia yake yote.
Mtoto huyo ambaye baba yake ni Seneta wa Garissa
na aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ulinzi wan chi hiyo, alisema
aliingia kwenye jengo hilo akiwa na bastola ambayo anaimiliki kwa
kufuata sheria zote za Kenya.
Anasema kuwa, alipofika ndani ya jengo hilo aliona
watu wengi wakiwa wameuwawa wakiwa wamelala chini na wengine wakiwa
bado wapo hai huku milio ya risasi ikiendelea kulia kila kona.
Aliungana na watu wengine kama 10 waliokuwa ndani
ya jengo hilo ambao pia walikuwa na silaha ili waone namna ya kusaidia
baadhi ya watu.
“Nimewahi kuona miili ya watu waliokufa lakini
sijawahi kuiona mingi kama ile ikiwamo ya watoto na kinamama
wasiojiweza,” anasema Haji
Anasema katika ghorofa ya juu ambapo watu walikuwa wamehudhuria
shindano la watoto kupika, sakafu, mafuta ya kupikia na vyakula
vilivyokuwa eneo hilo vilikuwa vimefunikwa na damu.
Anasema saa moja tangu magaidi hao wavamie jengo
hilo, huku kikosi cha kupambana na ugaidi kikiwa hakijafika eneo hilo,
kijana huyo na baadhi ya askari polisi waliokuwa wamefanikiwa kuingia
kwenye jengo hilo waliweza kuokoa baadhi ya watu.
Inaelezwa kuwa, kaka yake ambaye jina lake
halikutajwa, alikuwa amejificha kwenye choo kilichopo ghorofa ya kwanza
ya jengo hilo.
Anasema kuwa, waliweza kuokoa watu wengi waliokuwa
wamejificha kwenye maduka yaliyokuwa kwenye jengo hilo pamoja na
watumishi wa benki ya Barclays, ambao pamoja na wateja wao walikuwa
wamejifungia ndani ya ofisi za benki hiyo zilizo ndani ya jengo hilo.
Baada ya kuokoa watu wengi kwenye ngorofa za juu,
alirudi ile ya chini na kugundua kuwa kaka yake ameshasaidiwa pia kutoka
nje ya jengo hilo.
“Nimekasirika kwa kitendo ambacho hawa watu wamefanya na kusingizia kuwa wametekeleza hilo kwa jina la Uislam,” anasema.
“Mimi ni Mkenya mwenye asili ya Kisomali na pia ni
Muislamu, Uislamu hauubiri vurugu, wanafanya kinyume na mafundisho ya
Kiislamu,” anaongeza.
“Sijisikii kama shujaa hata kidogo, yule mtoto wa
kike aliyeonekana kwenye picha akinikimbilia ni shujaa, sidhani kama
nilikuwa na ushujaa kama ule nilivyokuwa na umri kama wake,” anasema.
Katika hatua nyingine, baadhi ya mashirika ya
kimataifa yamesema kuwa, uhalifu huo uliosababisha vifo vya zaidi ya
watu 60 Kenya, umefadhiliwa na fedha zitokanazo na mauzo ya meno ya
ndovu na pembe za faru.
Taarifa hizo zinasema kuwa, magaidi hao
wanategemea fedha hizo kwa ajili ya kununua silaha na kufadhili uhalifu
kama uliofanyika kwenye jengo la Westgate.
Kituo cha Uchunguzi wa Mambo ya Mazingira cha
Afrika Kusini, kinasema kuwa asilimia 40 ya fedha zote zinazotumiwa na
kundi hilo zinatokana na mapato hayo.
Mtu mmoja alinukuliwa akisema kuwa, “Shabaab
wamekuwa wakijishughulisha na kununua na kuuza pembe na meno hayo ili
kupata fedha za kufanikisha shughuli zake” .
Takwimu zaidi zinaonyesha kuwa, kundi hilo kwa mwaka 2011
lilipata dola za Marekani 200,000 mpaka 600,000 kwa mwezi kutokana na
biashara hiyo.
Kwa takwimu za mwaka 2012, kilo moja ya meno ya tembo ilikuwa inauzwa kwa dola 1800 za Marekani.
Taarifa hizo zilifafanua kuwa kwa kawaida tembo mkubwa jino lake moja huwa kati ya kilo 50 mpaka 70.
Zinaeleza kuwa, kikundi hicho hupata faida kubwa
kutokana na biashara hiyo kwani wao hununua jino moja kwa dola 100
kutoka kwa majangili.
Kutokana na hali hiyo, taarifa hizo zinasema kuwa
kikundi hicho hupata fedha nyingi za kununua silaha zozote watakazo,
kuwalipa vizuri wanamgambo wao na kuwawezesha kuwalipa washirika wao
fedha zitakazowafanya waishi maisha ya kifahari watakavyo.
Mapema mwaka huu, Kenya ilisema imeanza uchunguzi juu ya kikundi hicho kujishughulisha na ujangili wa tembo na faru nchini humo.
Ingawa Serikali haijaweza kutoa matokeo ya
uchunguzi huo kama ni kweli kiundi hicho kinahusika au kinahusika kwa
kiwango gani, tafiti za mashirika mengine zinathibitisha kuwa Al Shabaab
wanawatesa Wakenya kwa kutumia rasilimali zilizoko Kenya.
Baadhi ya wananchi wanaomba Serikali kuchukua
hatua kali za kupambana na ujangili kama mojawapo ya njia za kupambana
na matukio ya kigaidi nchini humo.
Vitendo vya kigaidi kwa kiasi kikubwa sio tu
kwamba vinawafanya wananchi kuishi wakiwa na hofu, pia vinachangia
kurudisha nyuma maendeleo kwa wawekezaji kuogopa kuwekeza katika taifa
lisilo na amani.
Aidha ni jambo linaloweza kusababisha wawekezaji
kupungua, hivyo wananchi wengi wameshauri kuimarika kwa ulinzi ikiwemo
kupambana na njia mbalimbali ambazo Al Shabaab wanafanya kuingiza
kipato.