Mtuhumiwa wa kutoa ushahidi wa uongo wa kumteka aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha madaktari, Dk Steven Ulimboka, Joshua Muhindi akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana, mara baada ya kulipiwa faini ya Sh 1,000. |
Raia wa Kenya, Joshua Muhindi, aliyekuwa akikabiliwa na shitaka la kutoa maelezo ya uongo kituo cha Polisi Oysterbay, kwamba alimteka nyara Dk. Steven Ulimboka, amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh. 1,000 (buku).
Hukumu hiyo ilitolewa jana chini ya kifungu cha sheria ya 121 ya mwaka 2002 kinachosema mtu atakayetoa taarifa za uongo kwa umma atapewa adhabu ya kifungo cha miezi sita jela au faini ya Sh. 1,000.
Hukumu hiyo ilitolewa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Hakimu Aloyce Katemana baada ya mshitakiwa huyo kukiri kosa hilo lililokuwa likimkabili.
Awali, kesi hiyo ilipelekwa mahakamani hapo kwa ajili ya mshtakiwa huyo kusomewa maelezo ya awali. Kabla hajasomewa, alikumbushiwa makosa yake na Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka. Mshtakiwa alikubali.
Katika maelezo ya awali, Kweka alidai kuwa mshtakiwa huyo alitoka Kenya na kuingia nchini kwa kupitia mpaka wa Namanga, uliopo mkoani Arusha.
Alidai alipoingia Dar es Salaam, alifikia katika eneo la Kawe na kwenda kwenye Kanisa la Ufufuo na Uzima, mbele ya Mchungaji, Joseph Marwa, na kutubu kuwa yeye ni miongoni mwa watu waliomtesa Dk. Ulimboka na kumtupa katika msitu wa Mabwepande.
Mshtakiwa hakuwa na hela hiyo na mwandishi wa habari wa Radio Times, aliyefahamika kwa jina la Chipangula Nandale, aliamua kumlipia faini hiyo ya Sh. 1000.
Agosti 6, mwaka huu, mshitakiwa alifutiwa mashtaka mawili, likiwamo la kutaka kumsababishia kifo Dk. Steven Ulimboka. Alikamatwa tena na kusomewa shtaka jipya la kutoa maelezo ya uongo.
CHANZO: NIPASHE