Marehemu Julius Nyaisangah.
Na Brighton MasaluALIYEKUWA mtangazaji nguli Bongo, marehemu Julius Nyaisangah aliwahi kutoa kali baada ya kusoma taarifa ya siku mbili zilizopita.
Akizungumza na mwandishi wetu siku ya kuuaga mwili wa marehemu Nyaisangah, mmoja wa aliyekuwa mtangazaji mwenzake ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, Mhe. Betty Mkwassa, alisema Nyaisangah alifanya kioja hicho wakati wakiwa Kituo cha ITV/Radio One mwaka 2003, jambo lililosababisha kupewa adhabu.
Akifafanua kwa undani zaidi, Mkwassa ambaye pia alijizolea umaarufu mkubwa sana kwa uhodari wa kusoma taarifa ya habari, alisema kwa kawaida mtangazaji kabla ya ku soma taarifa ya habari ni lazima aipitie kwanza kwenye karatasi na kwenye kioo maalum cha kusomea taarifa ya habari nusu saa kabla lakini siku hiyo hakufanya hivyo.
Alipitia taarifa ya habari kwa dakika kumi tu kabla ya kuingia studio ambapo hakuisoma ile ya kwenye kioo na kujikuta akisoma taarifa ya siku hiyo iliyoandikwa kwenye karatasi lakini matukio ya picha yakionekana ya taarifa ya habari ya siku mbili kabla.
“Unajua hali hiyo ilisababishwa na yeye kujiamini kupita kiasi, hivyo siku zingine hakuwa akisoma kabisa kabla ya kuingia studio, alishtuka baadaye na kujikuta akisimamisha kabisa kusoma taarifa hiyo.
“Wakafanya marekebisho, ndipo akaendelea. Alijilaumu sana, aliomba msamaha kwa dhati kabisa lakini aliapa kutorudia tena. Hata hivyo, pamoja na kuomba radhi kwa kosa hilo, uongozi ulimuadhibu japo sikumbuki vizuri ni adhabu gani alipewa,” alisema Mkwassa.