Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe. |
Ndugu Wanahabari,
NILIPOKUWA katika ziara ya bara la Ulaya kati ya Oktoba 21 mpaka
Novemba 2 mwaka huu (2013), nilipokea kwa njia ya barua pepe ripoti
inayoitwa "Taarifa ya Siri ya Chadema" ambayo pia ilikuwa imesambazwa
katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
“Taarifa ya Chadema inasema kwamba chama hicho (chama changu)
kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu tangu mwaka 2008 hadi 2010 na
kubaini kuwa mimi napokea fedha kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili
kuivuruga Chadema.
Ripoti hiyo ilinihusisha pia na mwananchi raia wa Ujerumani, Andrea
Cordes ambaye, kwa mujibu wa ripoti hiyo, alinisaidia kupokea na
kuhifadhi kiasi cha dola 250,000 za Marekani kupitia kwenye akaunti yake
binafsi.
Taarifa hii ya kutunga na iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha, imenifadhaisha, kunisikitisha na kunikasirisha.
Taarifa hii iliibuliwa katika kipindi ambacho nilikuwa safarini
kutetea haki za Watanzania na Waafrika ambao utajiri wao wa rasilimali
unafaidiwa na watu wachache waliohifadhi mali katika nchi za nje na pia
kupigania makampuni ya mataifa tajiri yalipe kodi stahiki katika nchi
zetu.
Pengine lengo la ripoti hiyo lilikuwa ni kutaka kunipoteza kutoka
katika nia na dhamira yangu ya dhati ya kutaka Watanzania wafaidike na
utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo waliamua kutoa taarifa
yao unazua maswali mengi kuliko majibu.
Nafahamu kwamba mimi ni mwanasiasa ambaye nimekuwa mlengwa (target)
wa mashambulizi kutoka kwa makundi mbalimbali ya wanasiasa na vikundi
vyao. Kama mwanasiasa, niko tayari kupokea changamoto zozote zinazokuja
na uanasiasa wangu.
Hata hivyo, ambacho sitakubali ni kwa watu kutumia jina langu na
uanasiasa wangu kunichafua mimi binafsi na watu wengine wasiohusika kwa
sababu ya kutaka kutimiza malengo yao ya kidhalimu.
Raia huyo wa Kijerumani tayari amekana kuhifadhi fedha zangu. Kwa
maelezo yake kwa baadhi ya viongozi wa Chadema amekana kuwa na akaunti
inayotajwa na amekana pia kuwepo nchini Ujerumani katika siku na wakati
uliotajwa kwenye ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imemtaja pia mtu kama Dk. Charles Kimei, Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB ikidai kwamba nilikutana naye na alishiriki
kwenye igizo hilo la kunipa fedha.
Niseme mapema kwamba tangu kuzaliwa kwangu sijawahi hata mara moja
kukutana na Dk. Kimei popote pale ndani au nje ya nchi. Kumuingiza mtu
ambaye amejenga jina lake kwenye taaluma ya kibenki kwa sababu tu ya
lengo ovu la kumchafua Zitto Zuberi Kabwe si uungwana bali ni unyama.
Kutokana na uchafuzi huu wa wazi dhidi ya taswira yangu binafsi na
watu wengine walioingizwa kwenye mkumbo huu, nimeandika rasmi kwa Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk.Wilbrod Slaa kumwomba athibitishe kwamba
kinachoitwa Taarifa ya Siri ya Chadema ni kweli ni taarifa ya chama au
kiikanushe ili niweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa
hekaya hiyo.
Cha ajabu, nimepokea ujumbe wa kutishiwa maisha kutoka kwa mtu
anayejiita Theo Mutahaba na kuahidiwa KUPOTEZWA endapo nitaendelea na
jitihada zangu za kupambana na ufisadi na kutafuta haki kwa Watanzania
wote pasipo kujali tofauti zao za kiitikadi, kikanda, kikabila na
kidini.
Natarajia kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote ambao
wamehusika na utungaji na uenezi wa taarifa hii. Nitahakikisha kwamba
wahusika wanatafutwa na kufunguliwa mashitaka stahiki ya upotoshaji na
kuchafuana.
Ni matarajio yangu kwamba wale wenye mapenzi mema na Tanzania, mimi
binafsi na utawala wa sheria, wataelewa nia yangu ya kutafuta haki
katika suala hili.
Nimeamua kujitolea maisha yangu kwa ajili ya Watanzania na kama
alivyopata kusema Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela;
“Struggle Is My Life.”
Forward Ever, Backward Never- Kwame Nkrumah
Zitto Kabwe (Mb)
10/11/2013