SUMATRA YASITISHA LESENI ZA MABASI 15 YAENDAYO MIKOANI...

Stendi Kuu ya Mabasi yaendayo mikoani Ubungo, Dar es Salaam.
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imesitisha leseni za usafirishaji kwa mabasi 15 yanayomilikiwa na kampuni tatu nchini.
Taarifa iliyotolewa jana na Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray ilisema wamesitisha leseni za usafirishaji kwa mabasi yanayomilikiwa na kampuni  ya Osaka yenye namba za usajili  T 158 BXG, T 610 ATR, T 572 BXJ, T 994 AGD,  T 607 ATR  na   T 852 AUL.
Alisema Kampuni ya Polepole Classic imesitishiwa leseni ya mabasi yake katika njia ya Moshi-Babati yenye namba za usajili T 898 BKN, T 267 AZL na T 212 BLZ.
Kwa upande wa Kampuni ya Burudani Bus Service, alisema wamesitisha leseni za usafirishaji kwa mabasi yenye namba za usajili T 158 BXG, T 610 ATR, T 572 BXJ, T 994 AGD na T 607 ATR.
Mziray alisema hivi karibuni basi la Osaka lenye namba ya usajili T 819 BYL lililokuwa likiendeshwa na  Emmanuel Semkamba kutokea Arusha kuelekea Dar es Salaam, lilipata ajali maeneo ya Kirinjiko katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Alisema ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu watatu  na majeruhi 33 na  baada ya uchunguzi ilibainika kuwa ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa madereva.
Kwa upande wa Kampuni ya Polepole  lenye namba za usajili T 898 BKN likiendeshwa na Stephano Pangawazi  kutokea Moshi kuelekea Babati, lilipata ajali maeneo ya Kijiji cha Machangarawe katika  Wilaya ya Babati mkoani Manyara na kusababisha 
vifo vya watu watano na majeruhi 32.
Alisema  basi la Burudani  lenye namba za usajili T 610 ATR lililokuwa likiendeshwa na Ruta Kwadahel likitokea Korogwe kuelekea Dar es Salaam, katika barabara ya Arusha- Dar es Salaam lilipata ajali maeneo ya Kijiji cha Taula, Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga na kusababisha  vifo vya watu 12 na majeruhi 93.
Mziray alisema kwa kuzingatia  Kifungu Namba 15 cha Sheria ya SUMATRA na pia Kanuni Namba 22 ya Kanuni za Ufundi na Usalama na Ubora wa Huduma  za Mwaka 2008, Mamlaka hiyo imesitisha  leseni za mabasi hayo mpaka  mabasi yote yakaguliwe na Jeshi la Polisi na kuthibitisha iwapo yanakidhi viwango vya ufundi na usalama, kuwasilisha picha  ya dereva aliyesababisha ajali hiyo pamoja na nakala ya leseni yake ya udereva.
Alisema sharti jingine ni kwa  madereva wa mabasi yaliyotajwa hapo juu wajaribiwe na Jeshi la Polisi kwa lengo la kujiridhisha kama wana sifa za kuendesha mabasi na kuwasilisha kwa maandishi mpango utakaotumiwa na kampuni hizo katika kudhibiti ajali za barabarani zinazosababishwa na madereva wake.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...