JEMBA ABANIKWA KAMA KUKU .... NI BAADA YA KUTUHUMIWA KUIBA BODABODA MAFINGA

Anavyoonekana majereha ya mgongoni
 
Sehemu ya miguu yake
Ezekiel Kaganga (29) mkazi wa Mjimwema Mafinga, wilayani Mufindi mkoani Iringa amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Mufindi mjini Mafinga baada ya kubanikwa kwenye moto kama kuku akituhumiwa kuiba pikipiki (bodaboda).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi amewataja watu wawili wakihusishwa na tukio hilo la kinyama.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni ni Alex Ludago (28) na Steven Michael (29) wote wakazi wa MET mjini Mafinga.
Akisimulia jinsi tukio lilivyokuwa katika wodi namba tano ambako amelazwa Kaganga alisema anafahamiana na watuhumiwa hao na kabla ya tukio hilo Januari 7, mwaka huu walikuwa pamoja wakinywa bia katika moja ya maduka ya kuuzia pombe mjini Mafinga.
Alisema Januari 8 mwaka huu alipokea taarifa katika duka hilo la pombe lililopo katika eneo la mashine ya mpunga kwamba kuna pikipiki ilipotea katika mazingira ya kutatanisha baada ya yeye kuondoka katika eneo hilo siku iliyopita.
Katika majibu yake kwa mmoja wa watuhumiwa hao alisema hajui lolote kuhusu kupotea kwa pikipiki hiyo.
 “Jamaa hao hawakuridhishwa na majibu yangu na Ijumaa ya Januari 12 alikamatwa na Polisi akihusishwa na tukio hilo na akatoka Januari 17,” alisema.
Alisema baada ya kutoka Polisi alikaa siku tatu uraiani na ndipo alipokamatwa na vijana hao na kupelekwa katika msitu wa Lumwago nje kidogo ya mji wa Mafinga.
Katika msitu huo alifungwa kamba, kupigwa viboko na baadaye alining’inizwa juu ya mti huku moto ukiwa umechomwa chini yake.
“Nilibanikwa kama kuku, moto ukiwa chini mie nikiwa nimefungwa juu ya miti; niliachwa hapo kwa siku mbili,” alisema.
Alisema baada ya siku mbili alihamishwa kutoka katika msitu huo na kupelekwa eneo la machijio mapya na kumwagiwa mafuta ya taa ili achomwe na moto na kundi la watu wanaokadiriwa kuwa saba.
“Nikiwa mahututi walinichukua na kunipeleka kituo cha Polisi kabla sijaletwa hapa hospitalini nako endelea kupata matibabu,” alisema.
Aliyata maeneo ambayo ameungua sana kuwa ni mgongoni, makalioni, mikononi, ubavuni, miguuni na shingoni.
Kaka wa Kaganga, Aizaki Kaganga alisema “mdogo wangu anaendelea kupata matibabu, na hali yake sio mbaya sana japokuwa hawezi kutembea.”
Alisema alipokea taarifa ya kupotea kwa mdogo wake  kuhusishwa na tukio hilo na akawaahidi watuhumiwa wamsubiri  arudi kutoka safarini Arusha ili alipe pikipiki hiyo.
“Hata hivyo vijana hao hawakuwa na subira hiyo na badala yake wakamfanyia unyama waliofanya,” alisema.
Kamanda Mungi alisema jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo pamoja na kuwasaka watuhumiwa wengine waliohusika na tukio hilo.
Akifarijiwa na kaka yake
Imechotwa: Matukio daima blog
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...