Katiba Mpya:. Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mh.Peter Msigwa ampongeza JK

                       Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mh.Peter Msigwa. 
Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mh.Peter Msigwa amefanya mkutano hapo jana katika viwanja vya Mwembetogwa, mkoani humo. Mkutano huo ambao ulikuwa wa kufungia mwaka 2013, Msigwa pia aliutumia mkutano huo kwa kuwapongeza baadhi ya mawaziri ambao utendaji kazi wao unaonekana kuwa mzuri, akiwemo Waziri wa Wizara ya Maji na Naibu Wake ,Waziri wa Ujenzi na Waziri wa Mazingira ambao wameonesha msimamo wa kweli katika kuwatumikia wananchi. Katika hatua nyingine mbunge Msigwa amemshukia aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe na kusema kuwa anatafuta umaarufu binafsi kuliko kukijenga chama chake na kuwa hana nia njema na CHADEMA,hivyo amewataka Wanachadema wa jimbo la Iringa mjini kutomsikiliza huku akibainisha kuwa Mwanachama na Kiongozi mzuri ni yule ambae anafanya kazi ya kukijenga chama chake na si kujijenga yeye binafsi. Amesema kuwa iwapo Zitto hatotaka kumsikiliza mwasisi wa Chama hicho, Mzee Mtei wala kuwasikiliza viongozi wa juu wa chama hicho akiwemo mwenyekiti wa katibu mkuu, ni wazi hakitakii mema CHADEMA na wana Chadema hawana budi kumpuuza kiongozi na mwanachama yeyote mwenye lengo la kuua chama. Kuhusu rasimu ya Katiba, Mbunge Msigwa amempongeza Rais Kikwete kuwa ameonyesha ushujaa wa hali ya juu katika kupigania upatikanaji wa katiba mpya, na kuwa iwapo wabunge wa CCM watapinga wao kama Chadema watarudi kwa wananchi kuhamasisha kupiga kura ya kuikataa katiba itakayopendekezwa na wabunge wa CCM. Aidha Msigwa ameongeza kusema kuwa atakuwa mstari wa mbele kuikosoa serikali kama itaonekana kuwa na viongozi dhaifu huku akiwataka watanzania kutathimini yale yote waliyofanya mwaka 2013 na kuwatakia kheri ya mwaka mpya. CHANZO CHA HABARI NA JIACHIE BLOG


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...