Mkuu
wa kitengo cha kuzuia na kupambana na madawa ya kulevya Mkoa wa Arusha
Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Aben Mgode akiwaonyesha waandishi wa
habari misokoto 5000 pamoja na baadhi ya magunia 16 ya madawa ya kulevya
aina ya bangi yaliyokamatwa kutokana na misako mbalimbali iliyofanyika
mkoani hapa. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
………………………………………………………………………
……………..
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Watu saba
wakiwemo wanawake wawili wamekamatwa na misokoto 5000 ya madawa ya
kulevya aina ya bangi pamoja na mirungi kilo 47. Tukio hilo lilitokea
mwishoni mwa wiki iliyopita katika eneo la Mti mmoja lililopo wilaya ya
Monduli.
Mafanikio
hayo yalitokana na msako shtukizi uliofanywa na jeshi la polisi Mkoani
hapa kuanzia saa 12:00 asubuhi mpaka saa 10:00 jioni baada ya kufanya
upekuzi katika magari mbalimbali na kupata madawa hayo ambayo yalikuwa
yanasafirishwa na watuhumiwa hao kupitia magari ya abiria yaliyokuwa
yakielekea Manyara, Singida, Dodoma na Mwanza.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisi kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas watuhumiwa
hao walikuwa wanayahifadhi madawa hayo kwenye mifuko ya “plastic” ili
yasitoe harufu na kisha kuweka kwenye mabegi.
Aliwataja
watuhumiwa hao kuwa ni pamoja na Godwina Munisi (31) Mkazi wa Sombetini
, Mwajuma Kingu (48) Mkazi wa Mbauda, Fidelis Joseph (48) Mkazi wa
Ngarenaro, Selemani Ally (34) Mkazi wa Olmatejoo, Omari Ally (25) Mkazi
wa Babati Mkoani Manyara Kasimu Ayubu (39) Mkazi wa Tarakea Rombo Mkoani
Kilimanjaro na Yasini Talian (40) Mkazi wa Ngarenaro.
Kamanda Sabas alisema kwamba watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Wakati huo huo
katika msako unaoendelea wilayani Longido, jumla ya magunia 16 ya
madawa ya kulevya aina ya bangi yamepatikana katika eneo la kijiji cha
Leboo baada ya askari Polisi kufanya msako na kufanikiwa kupata magunia
hayo 16 yaliyokuwa yanasafirishwa .
Kamanda
Sabas alisema kwamba, askari hao walikuwa wanafanya msako usiku na mara
baada ya watuhumiwa hao kugundua kuwa wanafuatiliwa walitelekeza
magunia hayo 16 na kukimbia. Inasemekana kwamba
watuhumiwa hao walikuwa wanatumia wanyama aina ya Punda kusafirishia
madawa hayo ambapo magunia yalikuwa yamefungwa mawili mawili.
Hata
hivyo Jeshi la Polisi Mkoani hapa bado linaendelea kuwatafuta
watuhumiwa hao ili wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili