SUMAYE AICHIMBA MKWARA MZITO CCM, ADAI ATACHUKUA UAMUZI MGUMU

MBIO za urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimezidi kuibua mambo mapya, baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kudai atachukua uamuzi mgumu kama chama chake kitateua mgombea urais asiye na sifa. Akizungumza katika kipindi cha Hapa na Pale, kinachorushwa na Radio Tumaini, mjini Dar es Salaam jana asubuhi, Sumaye alisema kama CCM itafanya mambo ya ajabu kwa kuteua mgombea asiyekubalika wala kuwa na sifa za kiongozi mwadilifu, atafungua ukurasa mpya.

“Nitachukua uamuzi mgumu kama CCM watateua mgombea ambaye hana sifa ya kuwaongoza Watanzania, nitachukua uamuzi mgumu, haiwezekani tukaongozwa na watu wanaotoa fedha nyingi kila kukicha.

“CCM wakifanya mambo ya ajabu kwa kuchukua mtu ambaye ametoa fedha, nitatafuta njia nyingine,” alisema.

Alisema hata siku moja hatakuwa na kinyongo kama atateuliwa mtu safi na mwenye moyo mweupe wa kusaidia Watanzania.

Alipoulizwa swali kama atagombea urais, alisema “Mimi sisemi kama nagombea, nakwambia muda ukifika nitasema tu, kwa wakati huu naomba tuendelee kutulia kwanza.

“Muda ukifika nitaamua nini cha kufanya, unajua unapotaka kuchukua uamuzi huu kuna mambo mazito ambayo unapaswa kuyatafakari kwa undani zaidi.

“Miongoni mwa mambo haya, ni kusaidia Watanzania kutoka walipo ili wapige hatua moja mbele zaidi, kuachana na tabia ya mtu mmoja kujitajirisha kupita kiasi,” alisema Sumaye.

Alisema kama Watanzania wakimhitaji ili awasadie, atakuwa tayari kufanya hivyo.

“Muda ukiwadia na Watanzania wakisema wananihitaji, basi nami nitakuwa tayari kuwasaidia…jukumu hili linahitaji mtu mwenye busara sana,” alisema Sumaye.

Alipoulizwa kuhusiana na hali ya CCM kwa sasa, alisema kuna tofauti kubwa katia ya CCM ya mwaka 1977 na ya sasa ambayo imekuwa ikikumbwa na matukio mengi.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...