Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kingwangalla (CCM), ametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi katika tukio la vurugu kwenye machimbo ya dhahabu.
Vurugu hizo ziliibuka jana katika machimbo ya dhahabu ya
Mwashina yaliyopo wilayani Nzega, Tabora na Jeshi la Polisi kulazimika
kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wachimbaji wadogo waliokuwa
wakiandamana wakiongozwa na mbunge huyo.
Wananchi hao walikuwa wakiandamana jana kuanzia eneo la
Isunga Ngwanda kuelekea katika machimbo hayo kupinga kitendo cha
serikali kufunga machimbo hayo ambayo wamekuwa wakichimba dhahabu kwa
muda mrefu na kuwasaidia kupata riziki.
Vurugu hizo ambazo zilianza majira ya mchana, zilisababisha watu wengine kadhaa kutiwa mbaroni sambamba na Dk. Kigwangalla.
Dk. Kigwangalla akizungumza na NIPASHE kwa simu muda mfupi
baada ya kutiwa mbaroni, alisema wakiwa katika maandamano hayo polisi
walianza kuwatawanya waandamanaji kwa mabomu ya machozi na yeye
alifanikiwa kutoroka.
Hata hivyo, baadaye polisi walifanikiwa kumkamata na kumuweka
ndani na hadi jana saa 10:45 jioni, mbunge huyo alikuwa bado chini ya
ulinzi wa polisi huku waandamanaji wakiwa wametawanyika.
“Soma facebook yangu, nimenusurika kufa na sasa nimekamatwa
na polisi na kuwekwa ndani…baada ya askari kuwatawanya wananchi kwa
risasi za moto. Nitatoka kwenye mawasiliano sasa hivi,” alisema Dk.
Kigwangala wakati akizungumza na NIPASHE.
Dk. Kigwangalla katika mtando wake wa facebook alisema katika
vurugu hizo kijana mmoja aliyekuwa karibu naye alipigwa risasi baada ya
riasi hiyo kumkosa yeye.
“Nimenusurika kuuawa muda si mrefu. Mungu mkubwa. Askari
kwenye gari ananiambia na bahati yako nimekukosa, nililengwa
kichwa….kijana mmoja aliyekaa mbele yangu amepigwa risasi kwenye paji la
uso, sijui kama amenusurika,” alisema na kuongeza:
“Vijana wamenilinda kwa ujasiri bila hofu. Leo askari
wamenikamata kwa staha. Siwezi kukubali kamwe dhuluma ya mabepari dhidi
ya wanyonge. Niliwaahidi na niliapa kuwatetea.”
Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Bituni Msangi, alisema alijulishwa kuwapo kwa vurugu hizo na Mkuu wa Polisi wa wilaya (OCD).
“Nipo nje ya wilaya, lakini nimepata taarifa kutoka kwa OCD
kwamba kumetokea vurugu ila sijafahamu vurugu hizo zimesababishwa na
nini,” alisema Msangi.
Hata hivyo, taarifa ambazo zililifikia gazeti hili jana
jioni, zilieleza kuwa wachimbaji watano akiwamo mbunge huyo
waliokamatwa sambamba na mbunge huyo wamewekwa katika kituo kikuu cha
polisi wilayani humo.