ONESHO LA WAPIGA ALA/VYOMBO VYA MUZIKI KUFANYIKA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM SIKU YA IJUMAA

Action Music Tanzania inayofuraha ya kukualika kuhudhuria onesho la muziki litakalofanyika siku ya Ijumaa ya tarehe saba mwezi wa tatu (07.03.2014) kwenye idara ya sanaa na sanaa za maonesho (FPA) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia saa kumi na mbili na nusu jioni hadi saa mbili usiku (12:30-2:00), Kiingilio ni bure.
Onesho hilo limeandaliwa na AMTZ litawahusisha wanamuziki kutoka kwenye taasisi mbalimbali ambao wameshiriki mafunzo maalumu ya muziki kwa muda wa wiki mbili ambayo yamefanyika kwenye Idara ya Sanaa na Sanaa za Maonesho ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (FPA), kuanzia Februari 24 mwaka huu. Pia wakati wa onesho kutakuwa na zoezi la kuchangia mfuko wa AMTZ ambapo wageni wataombwa kuchangia kiasi chochote cha fedha ili kuijengea uwezo asasi wa kuendelea kutoa mafunzo ya namna hiyo kwa watu wengine.  
AMTZ ni asasi isiyo ya kiserikali inayoundwa na walimu wa muziki kutoka katika taasisi mbalimbali za elimu ya muziki nchini na imesajiliwa na BASATA na kupata kibali cha kutoa mafunzo ya muziki ya muda mfupi. AMTZ imekuwa ikitoa mafunzo ya muziki kwa wanamuziki wa aina zote kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuandaa, kucheza na kufundisha muziki kwa kutumia mbinu mpya na za kitaalamu ili kuambukiza elimu ya muziki kwa wanamuziki wengine na hatimaye kuboresha ustawi wa muziki kwa ujumla wake nchini.
Kufika kwako katika onesho hilo utakuwa ni mchango mkubwa sana kwa wanamuziki wetu, asasi yetu na muziki kwa ujumla wake. Natanguliza shukran zangu za dhati na karibu sana

Contact:
Mandolin Kahindi
Executive Secretary
Action Music Tanzania


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...