Jamaa za abiria wa ndege hiyo wamekumbwa na majonzi makubwa.
Mamlaka
ya usalama wa safari za baharini nchini Australia imesema kuwa
operesheni ya kuitafuta ndege ya shirika la Malaysia iliyotoweka
imesitishwa kutokana na hali mbaya ya hewa na mawimbi makali baharini.
Taarifa
zinasema kuwa upepo mkali pamoja na mvua kubwa inayonyesha katika eneo
hilo ina maana kuwa ndege hazitoweza kupaa kwa usalama. Mawimbi makali
yameilazimisha meli ya jeshi la wanamaji wa Australia kuondoka katika
eneo ambalo mabaki yanayodhaniwa kuwa ya ndege hiyo yalionekana hapo
jana Jumatatu.
Dr
Erik van Sebille, ambaye ni mtaalam wa maswala ya Baharini katika chuo
kikuu cha New South Wales mjini Sydney, amefanya utafiti katika eneo
hilo la kusini mwa Bahari Hindi kutambua ni wapi na vipi vifusi
vinasafirishwa na mawimbi ya bahari. Anasema itakuwa vigumu sana kupata
mabaki ya ndege hiyo.
" Ni eneo lisiloweza kukalika duniani, acha niseme. Upepo unaovuma ni
mkali sana, mawimbi ni makubwa, ni mojawepo wa mawimbi makubwa zaidi
baharini. Unapofika katika eneo hili la kusini, unaanza kuhisi athari za
eneo la Antactica kwenye bahari. Hapa tunazungumzia dhoruba kali kali
sana hususan wakati huu tunapoingia majira ya kupukutika," anasema Dr.
Erik van Sebille.
Kadhalika amesema kuwa vifusi vilivyoenekana hapo jana tayari vimekwishaondolewa katika eneo hilo na mawimbi makali.
"Haitakuwa
rahisi kabisa kupata kijisanduku cha kunasa habari. Mawimbi ya eneo
hili ni makali na kwa hiyo vifusi ambavyo wametambua kwa sasa huenda
vimehamishwa katika kipindi cha majuma mawili au matatu tangu ndege hiyo
ianguka-na huenda vimesafiri kilomita alfu moja tayari. Na hii
inaifanya vigumu kurejelea utafutaji kwa sababu bahari inabadilika sana
hapa-ina vurugu ukipenda."
Hapo
awali naibu waziri wa mashauri ya nchi za Kigeni wa China Xie
Hangsheng, aliitaka serikali ya Malaysia kutoka ushahidi unaoelezea kuwa
ndege hiyo ilianguka katika eneo la Kusini mwa bahari Hindi. Ndege hiyo
ilitoweka kwenye mtambo wa Radar zaidi ya majuma mawili yaliyopita