Mkuu wa mkoa wa Mara, Bw. John Gabriel Tuppa.
MKUU wa mkoa wa Mara, Bw. John Gabriel Tuppa, amefariki dunia ghafla leo majira ya saa 4.30 asubuhi baada ya kuugua kwa muda mfupi ugonjwa wa shinikizo la damu akiwa wilaya ya Tarime mkoani Mara.
Katibu tawala wa mkoa wa Mara, Bw. Benedict Ole Kuyan, amesema kuwa Bw. Tuppa kabla ya kifo chake leo asubuhi akiwa na afya njema alifika katika ofisi ya za mkoa na kumuaga kuwa anakwenda kufunga mafunzo ya mgambo katika kijiji cha Nyamwaga wilayani Tarime.
Amesema kuwa muda mfupi baada ya kufika katika ofisi ya mkuu wa wilaya, alipatwa na tatizo la ugonjwa huo na muda mfupi alikimbizwa hospitali ya Tarime lakini alifariki wakati akipatiwa matibabu.
Katibu tawala huyo amesema mwili wa marehemu unasafarishwa kutoka Tarime kuja hospitali ya Musoma kwa ajili ya kuhifadhiwa wakati taratibu nyingine na maelekezo ya kiserikali yakisubiriwa kutolewa.