JWTZ LAPONGEZWA NA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA LADAIWA KUWA NI MOJA YA MAJESHI BORA DUNIANI..

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki moon amemwambia Rais Jakaya Kikwete, kuwa Umoja huo unajivunia mchango na ushiriki wa majeshi ya Tanzania katika Brigedi ya Kimataifa ya Kutuliza Hali (FIB) katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Ban amesema kuwa majeshi ya Tanzania katika DRC, kama ilivyo katika sehemu mbalimbali duniani yanapolinda amani, yamethibitisha ubora wa kufanya kazi.
 
Katibu Mkuu huyo pia amempa Rais Kikwete salamu za rambirambi na pole nyingi, kuomboleza vifo vya wanajeshi tisa waliokuwa wakilinda amani chini ya Umoja wa Mataifa Darfur, Sudan, ambako Julai mwaka huu wanajeshi saba walipoteza maisha.
 
Pia wanajeshi wengine wawili walipoteza maisha Congo. Ban alitoa salamu hizo Ijumaa iliyopita, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa UN mjini New York, Marekani.
 
Rais Kikwete alikuwa mjini New York kuhudhuria Mkutano wa mwaka huu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambalo alilihutubia baadaye Ijumaa hiyo. Rais aliondoka juzi kurejea nyumbani baada ya ziara hiyo ya kikazi.

Nakushukuru kwa uongozi wako na kwa uamuzi wako wa kukubali kushiriki kutafuta suluhisho katika DRC.
 "Ndani ya DRC, Jeshi la Tanzania limethibitisha kuwa jeshi linaloleta tofauti, lenye ubora uliothibitika ndani ya FIB.Tunakushukuru sana kwa kushiriki ulinzi wa amani duniani.

"Lakini pia nataka kuelezea rambirambi zangu na pole nyingi kwako, kutokana na gharama kubwa ya maisha ambayo majeshi ya Tanzania katika Darfur Julai mwaka huu na majuzi katika DRC yamepata. Ni dhahiri kuwa wewe kama kiongozi unaelewa fika maana ya amani ya dunia na faida zake,” alisema Ban.
 
Tanzania ina zaidi ya wanajeshi 2,500 wanaolinda amani Darfur, Sudan, DRC na Lebanon na ni nchi ya sita katika Afrika katika uchangiaji wa wanajeshi na polisi wa kulinda amani duniani.
 
Katika dunia Tanzania inashika nafasi ya 12 kwa kutoa mchango wake katika jukumu hiyo. Baada ya hapo, Ban alitaka kujua mambo kadhaa kutoka kwa Rais Kikwete, ikiwa ni pamoja na uhusiano na majirani hasa Rwanda na kushauri uhusiano huo uboreshwe na hatua zinazochukuliwa kukomesha vitendo vya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Katibu huyo pia aliitakia Tanzania mafanikio katika mchakato wa kupata Katiba mpya. Alimwalika Rais Kikwete kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi Duniani, utakaojadili Mabadiliko ya Tabianchi mwakani wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la UN. Naye Rais Kikwete alimshukuru Ban kwa rambirambi zake kwa Tanzania, baada ya kupoteza wanajeshi wake Sudan na Congo.
 
Baada ya kupokea rambirambi hizo, Rais alisisitiza kuwa Tanzania inayo wajibu wa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika kulinda amani katika sehemu mbali mbali na inaelewa fika athari na hatari za shughuli za kulinda amani duniani.
 
Rais pia alimweleza Katibu Mkuu huyo wa UN kuhusu uhusiano wa Tanzania na Rwanda, akisisitiza kuwa baada ya mkutano wa Kampala, Uganda kati yake na Rais Paul Kagame wa Rwanda, anaamini kuwa sasa uhusiano huo utarejea katika hali yake ya undugu wa kihistoria.
 
Kuhusu mauaji ya albino, Rais Kikwete alisema: “Tumejadili suala hili mara kadhaa huko nyuma Mheshimiwa Katibu Mkuu na kama nilivyopata kukuambia hili ni tatizo ambalo chimbuko lake ni imani za ushirikina na uchawi.

 Ni imani za kijinga tu.
” “Kama unavyojua, tuliendesha kura ya maoni kubaini washiriki wa ujinga huu. Kutokana na kura hiyo, tulikamata watu, wakafikishwa mahakamani na wengine wamehukumiwa kifo. Lakini ni jambo ambalo sasa limepoa sana nchini kwetu.”

-Habari leo


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...