Mkurugenzi wa ASET, Asha Baraka akimkabidhi Muhidi Gurumo fedha alizochangiwa kwa ajili ya matibabu wakati akiugua |
MUHIDINI Mwalimu Gurumo (sio Maalim kama
ilivyozoeleka kwa wengi) hatunaye baada ya kufariki dunia mchana wa leo
baada ya kuteseka kwa muda mrefu na maradhi mchanganyiko.
Mkongwe huyo ambaye alitangaza kustaafu
muziki Septemba mwaka jana baada ya kuitumikia fani hiyo kwa miaka
karibu 55, amefariki akiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Mzee huyo ameondoka huku akiwa bado
anahitajika katika medani ya muziki kutokana na uzoefu wake katika fani
hiyo aliyoianza akiwa na miaka 21 tu.
Mmiliki wa Blogu hii aliwahi kufanya
mazungumzo na gwiji huyo wakati akijiuguza nyumbani kwake na kupata
historia kamili ya fani yake ya muziki alipoanzia mpaka alipotangaza
kustaafu ambapo nyota wa muziki wa kizazi kipya Naseeb Abdul 'Diamond'
aliamua kumzawadia zawadi wa gari kufuatia kulalama kwamba kwa miaka
yote 55 ya kufanya muziki hana cha kujivunia.
Hapo chini nimeamua kuiweka makala hiyo
kama ilivyo ili umjue kwa undani mwanamuziki huyo ambaye ni vigumu
kusahaulika kwa kipaji alichokuwa amejaliwa na namna alivyokuwa mstari
wa mbele kutetea wanamuziki pamoja na kukumbatia utamaduni wa
Kitanzania.
Taarifa ziliztufikia muda mfupi uliopita
zinasema kuwa Mzee Gurumo atazikwa kesho majira ya saa 7 mchana
kijijini kwake Masaki, Kisarawe mkoani Pwani na msiba kwa sasa upo
Mabibo External.
***
Mzee Gurumo alikuwa mtu wa kujichanganya hapa akiwa na Nyosi El Saadat wa FM Academia |
HUWEZI kuuzungumzia muziki wa Tanzania
hasa miondoko ya dansi, bila kulitaja jina la Muhidin Mwalimu Gurumo
(sio Maalim kama baadhi walivyozoea kumuita).
Hii ni kwa sababu mwanamuziki huyo
mkongwe, maarufu kama 'Kamanda' au 'Mjomba', aliyewahi kutamba na
kuziasisi bendi mbalimbali nchini ameutumia zaidi ya nusu ya umri wake
katika mambo ya muziki, hivyo kuwa na mchango mkubwa katika fani hiyo.
Gurumo alianza fani ya muziki katika
bendi za mitaani miaka ya 1950 akipitia bendi moja baada ya nyingine
hadi Msondo Ngoma, ingawa kwa siku za karibuni amekuwa hapandi jukwaani
mara kwa mara kutokana na afya yake kutetereka kwa maradhi, hata hivyo
aliendelea kuwa mhimili wa bendi hiyo.
Mzee Gurumo akitunukiwa tuzo maalum na Rais Jakaya Kikwete wakati wa uzinduzi wa TBC1 ya Tido Mhando |
Mzee Gurumo akionyesha ukali wake enzi za uhai wake |
Gurumo akiwa nyumbani kwake kipindi akichanganya kwente maradhi yake |
Mzee Gurumo akiwa uwani mwa nyumba yake iliyopo Mabibo mmiliki wa blogu alipomtembea nyumbani kwake mwaka 2012 na kutengeneza makala hii. |
Mzee Gurumo akiwa na tuzo zake |
Mzee Gurumo akiwa sebeleni kwake |
Mzee Gurumo akiwa na mkewe kipenzi. |
Mzee Gurumo akiwa na wanamuziki wenzake wa Msondo wakati maradhi yakichanganya mwilini mwake, lakini damu ya muziki haikumzuia kupanda jukwaani. |
Mbali na mchango wake binafsi kama
mwanamuziki, Gurumo mwenye umri wa miaka 71 amekuwa msaada mkubwa kwa
wanamuziki waliowahi kuibuliwa naye au kufanya naye kazi kutokana na
misimamo yake thabiti ya kulinda na kutetea haki za wanamuziki.
Baadhi ya wanamuziki waliowahi kufanya
naye kazi na Gurumo ni Shaaban Dede 'Super Motisha', Bennovilla Anthony,
Hassan Rehani ‘Bitchuka’ na wengine kadhaa wakiwemo waliotangulia mbele
ya haki kama Suleiman Mbwembwe na Tx Moshi William, wamewahi kukiri
jambo hilo.
"Kama viongozi wa bendi wangekuwa kama
Gurumo katika kupigania na kutetea haki za wasanii, naamini tungekuwa
mbali mno, mjomba (jina jingine la utani la Gurumo) huwa hataki mchezo,"
aliwahi kusema Dede.
Wakati wa mahojiano maalum na yeye
yaliyofanyika hivi karibuni nyumbani kwake Mabibo jijini Dar es Salaam,
Gurumo alisema kwamba kilichokuwa kikimsukuma kuwapigania wanamuziki
wenzake na yeye mwenyewe ni dhamana ya uongozi na hali ya umaskini
aliozaliwa nao.
"Unajua mimi nimezaliwa katika familia
ya kimaskini na kimekulia kwenye umaskini, hivyo nafsi yangu huwa ngumu
kumkandamiza maskini mwenzangu kwani naamini sio haki na dhambi kubwa
kwa Mungu," alisema.
"Japo nilikuwa katika nafasi ya kufanya
hila kwa kuegemea upande wa wamiliki wa bendi, ila kule kutambua kuwa
uongozi niliopewa na wenzagu umetokana na imani yao kwangu, ndio maana
nilikuwa mkali kama pilipili kuwapigania wenzangu," aliongeza.
Gurumo, alisema hata alipokuwa
akishawishiwa na baadhi ya wamiliki wa bendi ili kuwageuka wenzake
ilimradi yeye aongezwe dau lolote analotaka, hakukubali kirahisi na
wakati mwingine kufikia kuamua kuhama iwapo dai lake halisikilizwi.
"Karibu bendi zote nilizopitia misimamo
yangu ilikuwa hivyo na ikitokea uongozi ukawa mbishi kukaidi madai
ninayowasilisha kwao, huwa radhi kuondoka kama nilivyofanya OSS na
kwingine," aliongeza.
Gurumo, alisema kutokana na misimamo
hiyo mikali, alijikuta kila bendi aliyojiunga nayo wanamuziki wenzake
humchangua kuwa kiongozi hadi sasa akielekea kustaafu fani hiyo kutokana
na umri kumtupa mkono na maradhi yanayomsumbua kwa hivi sasa.
Alisema, tabia yake ya kutanguliza
masilahi ya wanamuziki wenzake mbele kwa kiasi fulani yamechangia
kushindwa kujijenga kimaisha kulinganisha na umaarufu wa jina lake na
umri alioutumia katika fani hiyo ya muziki.
Gurumo, alisema katika umri wa zaidi ya
miaka 40 aliyotumia katika muziki hana cha kujivunia zaidi ya kujenga
nyumba yenye vyumba 17 eneo la Mabibo, kujenga nyumba nyingine katika
shamba lake lililopo kijijini kwao Masaki, Kisarawe, mkoani Pwani.
"Nyumba hii kama unavyoiona ambayo
nimewapangisha watu na ninaendelea kuikarabati ndio pekee ya kujivunia,
pia nina shamba nililojenga kibanda kingine huko Masaki, lakini kwa
hadhi yangu nilipaswa kuwa mbali na hapa au vipi?" alisema Gurumo kwa
kuhoji.
Alisema, kwa hadhi yake wala asingekuwa
akipigana vikumbo na mashabiki wake kwenye daladala aendapo kwenye
shughuli zake na hata kwenye kliniki ya matatizo yake kiafya, lakini
hana jinsi kwa vile hana uwezo wa kumiliki hata gari ndogo ya
kutembelea.
"Naamini wengine wanaweza wasiamini,
lakini ukweli ni kwamba sijahi na wala sijui ni lini nitakuwa na usafari
wangu binafsi, natamani lakini tatizo uwezo wa kifedha ndio tatizo,
kama sio kujenga banda hili hapa Mabibo, sijui ingekuwaje," alisema.
Alisema, kinachomfanya awe katika maisha
hayo licha ya umaarufu wake kimuziki, Gurumo alisema mbali na
kuthamini na kujali wengine, lakini ukweli ni kwamba enzi akiutumikia
muziki hakukuwa na masilahi ya kutosha kama wapatavyo vijana wa sasa.
"Huwa natamani miaka irudi nyuma na zama
zile ziwe hivi sasa, ili nami niweze kunufaika na jasho langu katika
muziki," alisema huku tabasamu la uchungu likimtoka usoni mwake.
MJOMBA
Mkongwe huyo aliyejifunza muziki tangu
akiwa Shule ya Msingi Sungwi, iliyopo Kisarawe akiimba na kupiga dramu
katika bendi ya shule, alisema safari yake ya muziki kwa kiasi kikubwa
ilichangiwa na mjomba wake aitwaye Seleman Sultan Wamikole.
Alisema mjomba wake aliyemchukua tangu
akiwa mdogo baada ya baba yake mzazi Mwalimu Mohammed Gurumo, kufariki
na kumuacha katika maisha magumu na ndugu zake wakiwa na mama yao
Mwazani Sultan aliyefariki mwaka 1981.
Alisema kutokana na hali ilivyokuwa
nyumbani kwao, mjomba wake huyo alimchukua na kuja kuishi nae Dar es
Salaam maeneo ya Ilala ambapo moja kwa moja alimwandikisha katika
madrasa ambako alipata fursa ya kuimba kaswida.
Alisema kuwa baadaye alipata hamu ya
muziki hasa kutokana na kuvutiwa na kazi za nyota wa wakati huo, Salum
Abdallah 'SAY' na Luambo Luanzo Makiadi 'Franco'.
Alisema mjomba wake huyo akishirikiana
na mama yake walitambua kiu kubwa aliyokuwa nayo katika sanaa ya muziki
na hivyo wakamruhusu kujiunga jumla ambako alizidi kuiva na baadaye
kufuatwa na bendi mbalimbali.
"Kwa kitendo nilichofanyiwa na mjomba
kwa kunitunza, kunilea na kunisaidia katika harakati zangu za muziki,
ilinifanya nimtungie wimbo maalum nilikuwa OSS miaka ya 1980, wimbo
uliitwa 'Shukrani kwa Mjomba'," alisema Gurumo.
Alisema anaamini kama sio mjomba na mama
yake ambaye hadi leo anamliza akikumbuka alivyofariki, huenda
asingefikia mahala alipo sasa kimuziki.
Mtunzi na muimbaji huyo mahiri nchini,
alisema licha ya kipaji cha kuzaliwa, lakini Salum Abdallah na Franco ni
watu waliochangia kufika kwake hapo alipo kwani enzi zao walimvutia
mno.
"Ni kweli kipaji cha muziki nimezaliwa
nacho na kukirithi kutoka kwa mama yangu Mwazani aliyekuwa kiongozi wa
kundi la ngoma, ila kuvutiwa na Salum Abdallah na Franco ni sababu ya
mimi kufika hapa nilipo, niliwapenda mno wanamuziki hawa," alisema.
SAFARI
Gurumo alisema baada ya kujifunza muziki
kwenye makundi mbalimbali ya mitaani, mwaka 1959 ndipo alipoanza
kutambulika rasmi baada ya kuchukuliwa na bendi ya Kilimanjaro Chacha.
Alisema alijiunga na bendi hiyo kama
muimbaji ingawa pia alikuwa anamudu kupiga dramu chombo alichokuwa
akikipiga katika bendi ya shule na ndani ya bendi hiyo ndipo alipotunga
kibao chake cha kwamba kilichoitwa 'Wakati Nikiingia Bar'.
Hata hivyo Gurumo alisema hakukaa sana
Kilimanjaro Chacha kwani mwaka 1962 alihama na kwenda kujiunga bendi ya
Rufiji Jazz alipokutana na wakali kama Salum Nonde, Mbarouk Khalfan na
wengine.
Alisema alijiunga na bendi hiyo kutokana
na kushawishiwa na safari ambayo Rufiji Jazz ilikuwa ikitarajia kufanya
mkoani Arusha na pia maslahi, hata hivyo miezi michache baadaye
aliiacha bendi hiyo na kuhamia Kilwa Jazz B mwaka 1963.
"Masiahi na ujana ndio ulionifanya
niikache bendi ile na kutua Kilwa Jazz B, ambapo kutokana na kipaji
kikubwa cha uimbaji nilichokuwa nacho, uongozi wa Chama cha Wafanyakazi
(NUTA) uliamua kunichukua na kutua NUTA Jazz mwaka 1964," alisema.
Alisema kuwa alipotua NUTA alitunga
kibao kilichokuja kumpa umaarufu cha kilichoitwa 'Mwangele', kikiwa na
maana 'Mchumba' kwa lugha ya Kingoni na kisha kufuatiwa na nyimbo
nyingine kadhaa.
"Kwa kweli idadi ya nyimbo nilizotunga
nikiwa NUTA sizikumbuki kwa wingi wake, ila baadhi ni kama "Nimuokoe
Nani', 'Kaka Seleman', 'Amina', Msondo Ngoma Na.1-4 na 'Maneno ya
Nyerere'," alisema.
Gurumo alisema baada ya kuipandisha
NUTA iliyokuwa ikifahamika baadaye kwa jina la JUWATA, hasa
alipowachukua wanamuziki nyota kama Bitchuka 'Stereo' na Said Mabera
aliyekuwa akipuliza 'trumpet' katika bendi moja ya Arusha, Shirika la
Teksi (TTTS) lilimfuata ili kuasisi bendi yao.
"TTTS walinifuata na kunieleza nia yao
ya kutaka kuanzisha bendi na nikakubaliana nao ambapo walinilipa Sh
50,000, nikaondoka Juwata Jazz mwaka 1978 na kuasisi bendi ya Mlimani
Park 'Sikinde' nikiwa na wanamuziki wenzangu wa Juwata na wengine kutoka
Dar International," alisema.
Aliwataja baadhi ya waasisi wa bendi
hiyo iliyokuja kufahamika kama DDC Mlimani Park kabla ya miaka mitatu
iliyopita kurejea jina lake la awali baada ya kutemwa na mwajiri wao,
Shirika la Maendeleo mkoa wa Dar es Salaam, ni Hassani Bitchuka na
marehemu Abel Baltazar aliotoka nao Juwata.
Wengine ni Joseph Mulenga 'Spoiler',
Salum Machaku, Cosmas Chidumule, Hamis Juma 'Maalim Kinyasi', Ibrahim
Mwinchande, Abdallah Gama na George Kessy kabla ya kuongezwa nguvu na
akina Michael Enoch 'Teacher', Joseph Benard na Habib Jeff.
‘KASSIM WA KUTUMIA’
Alisema ndani ya Sikinde, kama kawaida
aliendelea kutamba na utunzi wa nyimbo zilizotwaa umaarufu mkubwa
ukiwemo wa 'Kassim' uliokuwa na sehemu mbili.
Gurumo alisema kibao hicho ni tukio la
kweli lililomhusu rafiki yake aitwaye Kassim aliyekuwa akifanya kazi
katika kampuni ya mizigo uwanja wa ndege (DAHACO), ambaye alikuwa
akisifika enzi hizo kwa ulevi na kusahau familia yake.
"Huu wimbo nilimtungia rafiki yangu
ambaye alikuwa akiendekeza starehe kupita kiasi na kila nilipokuwa
nikimsihi apunguze, alikuwa akinitaka nimuimbe ndipo ataacha ulevi,"
alisema.
Alisema kuwa baada ya hapo, ndipo
alipoamua kutunga 'Kassim namba 1', ambapo mwenyewe (Kassim) alikuwa
akijisikia fahari, ingawa hakuacha ulevi hadi alipopatwa matatizo kazini
na kuchacha ambapo kidogo aliacha pombe na yeye kumtungia Kassim Na.2'.
Gurumo alisema mpaka sasa hajui kama
jamaa yake huyo aliacha pombe na pia hajui kama yu hai au la kwa vile ni
miaka mingi imepita bila kuonana naYe.
"Sijui kama yu hai au la, ila nyimbo
zile zilimhusu yeye katika kumkataza anasa ingawa pia nilikuwa natoa
ujumbe kwa jamii," alisema.
Mkali huyo ambaye ni shabiki wa kutupwa
wa Simba, akiwa ni mmoja wa wanachama wake tangu mwaka 1972 na pia
anayeishabikia Manchester United ya Uingereza, alisema alikaa na Mlimani
Park hadi mwaka 1985 alipojiunga na safari Sound (OSS) akiwa na
Bitchuka.
Alisema alipotua OSS aliwakuta baadhi ya
wanamuziki wake ambao wengi wao walitokea Zaire (sasa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo) wakilala chini na kuushinikiza kuwanunulia
vitanda kama anataka aifanyie kazi bendi hiyo.
Alisema kuwa kwa bahati nzuri, uongozi
ulimsikiliza na kuwanunulia wanamuziki wote vitanda kama alivyotaka na
kuanza kufanya kazi ikiwemo kubadili mtindo wa bendi hiyo wa 'Dukuduku
Yee' na kuwa 'Ndekule'.
Gurumo alifichua kuwa mitindo yote
aliyoasisi katika bendi za NUTA Jazz, Mlimani Park na OSS ya 'Msondo
Ngoma', 'Sikinde Ngoma ya Ukae na 'Ndekule' ni ngoma ya asili ya kabila
lake la Kizaramo ambazo mama yake alikuwa akiimba na kuzicheza enzi
zake.
Alisema jambo hilo la kutumia ngoma za
makabila ya kabila lake, ndilo ambalo hata wanamuziki nyota wa nchi za
Kongo na mataifa mengine ya Afrika Magharibi wamekuwa wakifanya na
kuutangaza muziki wao kimataifa tofauti na ilivyo nchini.
"Hata Wakongo na wanamuziki wa kimataifa
kutoka nchi kama Senegal, Cameroon, Nigeria na Chad wamekuwa wakibuni
muziki wao kwa kutumia ngoma za makabila yao, bahati mbaya vijana wengi
wameshindwa kuumiza vichwa nao kubuni kazi zao na kuishia kunakili kazi
za wenzao bila kujua wanawasaidia kuwatangazia, kwa kulikwepa hilo ndio
maana nilikuwa nakubuni miondoko ya kabila langu la Kizaramo," alisema.
Gurumo, alisema sio jambo baya
wanamuziki wa Tanzania kuiga kazi za wenzao, kitu alichodai ni vigumu
kukikwepa, lakini alidai ni vema kama wangekuwa wakibuni vionjo
vitakavyowatofautisha na wanamuziki hao wanaowaiga.
Alisema kwa muono wake ukiondoa Msondo
na Sikinde zinazopiga muziki unaotambulika kama dansi la Tanzania,
karibu bendi zote zinapiga muziki kwa kuwaiga wakongo, hata kwa zile
bendi ambazo zilikuwa zikiaminika kuwa ni kilelezo rahisi kuitambulisha
Tanzania kimataifa.
ULEVI
Gurumo hafichi kitu juu ya ujana wake
kwa kueleza mbali na 'ubitozi' aliokuwa nao, pia alikuwa 'gangwe' enzi
zake na pia aligeuzwa mtumwa wa pombe kutokana na kuwa mlevi
aliyepitiliza.
Alisema, alikuwa anakata kilaji isivyo
kawaida jambo ambalo lilikuwa likimfanya akorofishane na mama yake mzazi
aliyetishia kumuachia 'laana' kama angeendelea kuendekeza ulevi.
"Kwa wanaonijua sidhani kama hili ni
jipya, nilikuwa mlevi haswaa, kiasi mama alishindwa kunivumilia na
kutishia kuniachia laana kama nisingesikilia wito wake wa kuachana na
pombe," alisema.
Alisema, baada ya kushindana na
'shetani' kwa muda mrefu akikorofishana hata na mkewe, Pili bint Said
Kitwana, hatimaye aliachana na ulevi mwaka 1982, miezi michache tangu
mama yake mzazi kufariki.
"Ilikuwa ni kazi ngumu kuachana na
pombe, lakini kwa heshima ya mama niliacha, pia shinikizo la mke wangu
kipenzi ambaye ninampenda na kumsifia kwa uvumilivu wake, niliacha miezi
michache baada ya mama kufariki na hadi leo situmii hiyo kitu,"
alisema.
Gurumo, alisema binafsi anajutia masuala
ya ulevi akidai ni kati ya mambo yaliyochangia kumkosesha kufanya mambo
ya maendeleo pamoja na kuihatarisha ndoa yake, kama mkewe
asingekumvumilia kwa miaka 20 tangu walipooana mwaka 1962.
"Naamini ulevi uliopitiliza kwa hakika
ni mbaya kama vijana wa sasa mnavyosema kwamba 'ulevi ni noma', nusura
ndoa yangu ivunjike kwa ajili ya kuendekeza hii kitu, hata nilipotangaza
kuachana na pombe si mke wangu wala marafiki zangu waliokuwa wakiamini
hadi walipoona siku zikienda bila kupiga kilaji," alisema Gurumo.
Gurumo alisema hakuna kitu anachofurahia
maishani mwake kama siku alipooana na mkewe, aliyezaa nae watoto wanne,
Mariam aliyemzaa mwaka 1981, Mwalimu, 28, Omar na Mwazani pamoja na
alipoachana na pombe.
"Hivyo ndivyo vinavyonifurahisha hadi
leo, nilipomuoa mke wangu na nilipoacha pombe, ila kwa huzuni ni kifo
cha mama yangu, huwezi kuamini hadi leo huwa nikikumbuka natokwa machozi
kwa namna mama alivyokuwa anikipenda na tulivyokuwa tunapendana na
kuishi kwa upendo na furaha," alisema.
Gurumo, alisema maisha yake yamekuwa
mikononi mwa mama yake kutokana na baba yake kufariki mwaka 1948 wakati
akiwa na miaka nane tu, ndio maana amekuwa akimkumbuka kila mara
marehemu mama yake.
BITCHUKA
Gurumo anayekula vyakula vyote halali na
vyenye manufaa kwa afya yake na kunywa juisi na soda, alisema hakuna
tukio lisilofutika kichwani mwake kama siku alipoamua kumsimamisha kazi
'swahiba' wake, Hassani Rehani Bitchuka.
Alisema, alifanya uamuzi huo aliouita
kuwa mgumu kuwahi kukutana nao maishani kama mwanamuziki mwaka 2005,
baada ya Bitchuka kugoma kushiriki kwenye onyesho la pamoja kati ya
Msondo Ngoma na African Stars 'Twanga Pepeta'.
"Bitchuka aligoma kushiriki onyesho hilo
kwa madai asingeweza kufanya onyesho na watoto, kitu ambacho kiliwaudhi
wanamuziki wenzake na wote waliniangalia mimi kama kiongozi wao
nitafanya nini kwa kosa alilofanya 'swahiba' wangu ambaye tumekuwa
katika 'udugu' tangu nilipomchukua toka Arusha mwaka 1973," alisema.
Alisema, hata hivyo alilazimika kusimama
kidete kama kiongozi kwa kuweka kando 'uswahiba' wake kwa Bitchuka, ili
kuinusuru Msondo na kuitisha kikao nilichotangaza kumtimua kundini,
jambo ambalo anadai hadi leo humpa tabu kubwa kutokana na uhusiano
aliokuwa nao na Bitchuka kwa mjda mrefu.
"Kwa kweli jinamizi la tukio lile hadi
leo huniwewesesha, lakini tayari nilishazungumza na Bitchuka na
kunielewa, pia unajua wakati mwingine ukiwa kiongozi unapaswa kufanya
maamuzi magumu bila kutarajiwa," alisema.
Alipoulizwa juu ya msanii gani kwa sasa
anayemuona kama ndiye mrithi atakayeendeleza gurudumu la muziki wa dansi
nchini, Gurumo bila kificho alimtaja Husseni Jumbe mmiliki wa bendi ya
Talent.
"Kwangu namuona Jumbe kama ndiye tumaini
pekee la maendeleo ya muziki wa dansi kutokana na kipaji kikubwa
alichonacho akitunga, kuimba, kupanga muziki na kujaliwa sauti ya
kipekee," alisema.
Kuhusu muziki wa kizazi kipya, alisema
upo juu kwa vile unatangazwa mno na vyombo vya habari, ila haoni kama ni
muziki wenye nguvu unaoweza kuufunika muziki wa dansi.
"Promo ndio inayoubeba muziki huu, kitu
kinachowalemaza wasanii wake kushindwa kuwa wabunifu na kujiona wamefika
mbali, wakati wana kazi kubwa hususani ya kujifunza kupiga ala
mbalimbali ili wapige muziki wao utakaokubalika kimataifa tofauti na
sasa wakitegemea kila kitu kifanywe studio," alisema.
Hata hivyo alikiri wanaoufanya muziki
huo na taarabu wamekuwa na mafanikio makubwa kimaisha kwa vile soko
limewapokea vema, jambo ambalo hata yeye hupata wivu akifikiria
anapowaona vijana wakiendesha magari wakati yeye akitembea kwa miguu
licha ya muda mrefu aliotumia kwenye fani hiyo ya muziki.
SWAHIBA WA JK
Gurumo, alisema fani yake ya muziki
imemsaidia kufahamiana na wengi wakiwemo viongozi mbalimbali wa ndani na
nje ya nchi, huku akimtaja Rais Jakaya Kikwete kwamba ni mmoja wa
viongozi 'rafiki' zake.
Alisema, urafiki huo ndio anaoamini
ulimfanya Rais Kikwete kuvunja shughuli zake na kumtembelea hospitalini
kumjulia hali alipolazwa kwa mara ya kwanza kutokana na maradhi
yanayomsumbua.
Gurumo, alisema kitendo cha Rais Kikwete
kuacha kazi zake kwendsa kumjulia hali na kumsaidia katika matibabu
yake kumemfariji mno, kwa vile katika kulazwa kwake na hata sasa
akiendelea kujiuguza nyumbani hakuna kiongozi yeyote wa serikali
wakiwemo wa Wizara wa Habari na Utamaduni, kuwahi kwenda kumjulia hali.
"Huwezi amini ni yeye na mkewe, Mama
Salma ndio waliokuja kunijulia hali hospitalini, akianza mwenyewe kisha
mkewe kitu ambacho kinanifariji hadi leo nikiamini Rais Kikwete
anatujali na kututhamini wasanii," alisema.
Aliongeza kuwa, ukiondoa kufarijika
kwake kutembelewa hospitalini na Rais Kikwete na mkewe, Mama Salma, pia
kitendo kilichofanya na Mkurugenzi wa ASET, Asha Baraka cha kuandaa
onyesho maalum kwa ajili ya kumchangia ni kitu ambacho kitabaki kichwani
mwake na kumpongeza mwanamama huyo maaraufu kama 'Iron Lady'.
"Kwa kweli sikutarajia kama Asha Baraka
angeweza kufanya kitendo kile ambacho ni wazi ninaonyesha ni jinsi gani
anavyothamini na kujali mchango katika muziki. Nadhani watu wengine
wanapaswa kuiga mfano wake, ni mtu ambaye ameonyesha mapenzi kwangu na
kujali mchango wangu katika muziki, namshukuru na kumpongeza," alisema.
Gurumo, anayechizishwa na rangi nyekundu
na nyeupe na ambaye anapenda kutumia muda wake za ziada kujishughulisha
na mambo ya Kilimo kwenye shamba lake lililopo Masaki, alisema katika
maisha yake kisanii amewahi kupata tuzo mbili tu zote za mwaka 2008.
Alisema tuzo hizo ni ile ya Kili Music
Award kama Mwanamuiki Mkongwe na ile ya Hall of Fame, huku aliyekuwa
mdau mkubwa wa muziki nchini aliyekuwa akifanya shughuli zake Umangani,
Is'haka Kibene alimtengenezea na kumpa tuzo maalum kumtambua kama
'Kamanda wa Muziki wa Tanzania.
UBUNIFU
Gurumo, aliyeanza kuonekana tena kwenye
jukwaa la bendi yake ya Msondo baada ya kuwa nje kwa wiki kadhaa
kutokana na kulazwa hospitalini, alisema muziki wa Tanzania umepiga
hatua kubwa kimaendeleo, ingawa alikiri kwamba kukosekana kwa ubunifu
miongoni mwa wananamuziki na wasanii wake ni tatizo linaloukwaza
usitambe nje.
Alisema, hata muziki wa kizazi kipya
(bongofleva) ambao umekuwa ukitajwa kama wenye maendeleo makubwa kwa
wasanii wake, alisema unashindwa kutamba kimataifa kwa sababu wasanii
hao hawaumizi vichwa kubuni vitu vipya.
Mkongwe huyo alisema tatizo la wasanii
kupenda kuiga kazi za wenzao wa nje na kuzifanya zao kwa kuziimba
kiswahili, ndilo linalowafanya wasitambe kimataifa na kutaka kuwepo kwa
mabadiliko kuanzia sasa.
Alisema suala la kuiga kazi za nje
halijaanza sasa, bali kitamboi kirefu akikiri hata wao (wakongwe)
walikuwa wakifanya hivyo, ila alisema ubunifu wa ziada ndio uliowafanya
waonekane mahiri katika soko la kimataifa.
"Kuiga ni jambo lisilokwepeka, lakini ni
wajibu wa wasanii wa sasa kuumiza vichwa na kubuni vitu vipya ambavyo
vitawatofautisha na wanaowaiga. Sio Bongofleva wala dansi kote wamelemaa
kwa kuiga kazi za wenzao," alisema.
Alisema cha ajabu hata bendi za zamani
ukiondoa Msondo Ngoma na Mlimani Park, zote hushindana kupiga muziki wa
kikongo bila kujua wanasaidia kuutangaza muziki wa nchi hiyo na
kuzidumaza bendi zao tofauti na Msondo na Sikinde.
Aliongeza anahisi bendi hizo zimeamua
kuingia kwenye mkumbo huo kutokana na upepo wa soko ulivyo, japo alisema
kimezifanya bendi husika zisiwasisimue mashabiki wake kama ilivyokuwa
miaka ya nyuma.
KUSTAAFU
Gurumo, alisema hana muda mrefu kabla ya
kutangaza kustaafu fani ya muziki kutokana na hali yake ya kiafya na
umri mkubwa alionao akitaka kuwapisha wanamuziki wenye damnu changa
kuendelea gurudumu la fani hiyo.
Alisema, ingawa hajajua ni lini atafanya
hivyo ila hadhani kama utamalizika mwaka huu wa 2012 kabla ya kutimiza
azma hiyo na kudai atakapostaafu atajikita kwenye kuwasaidia vijana
chipukizi.
Gurumo, alisema mipango yake ni
kuanzisha chuo cha muziki anachotaka kukijenga Masaki, Kisarawe iwapo
atapata mtu wa kumsaidia kufanikisha hilo kwa lengo la kutaka kuendeleza
vipaji na kuudumisha muziki wa Tanzania.
"Sina muda mrefu kabla ya kustaafu rasmi
muziki, sitajiweka kando kabisa na ndoto zangu ni kutaka kujenga chuo
cha muziki katika shamba langu lililopo Masaki, lakini natatizwa na hali
ya kiuchumi, hivyo kama serikali au mtu yeyote mwenye uwezo kifedha
akinisaidia nitafurahi kwa vile nataka kuendeleza muziki wetu," alisema.
Alisema, anaamini vijana wanapaswa
kujifunza mengi kutoka kwake na kwa wakongwe wengine ili kuufanya muziki
wa Tanzania uendelea kudumu hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya
kidunia.
FAMILIA
Muhidini Mwalimu Gurumo, alizaliwa mnamo
mwaka 1940 katika kijiji cha Masaki, Kisarawe akiwa ni mtoto wa pili
kati ya watatu wa mzee Mwalimu Mohammed Gurumo.
Baba yake alifariki wakati Gurumo akiwa
na miaka nane tu na hivyo maisha yake ya utotoni kuwa chini ya mama yake
mzazi kabla ya kuchukuliwa na mjomba wake aliyemsaidia kuingia kwennye
muziki.
Gurumo, alifanikiwa kufunga ndoa na
mkewe, Pili bint Said Kitwana na kubahatika kuzaa nae watoto wanne,
ambapo ni mmoja tu aitwae Mariam ndiye aliyerithi kipaji chake cha
muziki akiimba kundi moja la taarabu lililopo Temeke.
Mkongwe huyo anayemtaja Said Mabera
'Dokta' kama mmoja wa wanamuziki viongozi anayemzimia, alisema katika
maisha yake ya ndoa hakuna anachokifurahia kama kudumu kwa ndoa yake na
mkewe ambayo imetimiza miaka 50 mwaka huu.
Alisema, kama sio uvumilivu wa mkewe,
huenda ndoa hiyo ingevunjika kitambo kutokana na ukweli ukiondoa ulevi
na kazi yake ya sanaa, pia ukorofi aliokuwa nao uliochangiwa na ujana ni
kati ya mambo yaliyotaka kuivunja ndoa yake.
"Sio siri najivunia kuwa na mke
mvumilivu kama huyu, kuna mambo niliyomfanyia kwa muda mrefu ndani ya
ndoa yetu, lakini alinivumilia hadi leo tukiingia mwaka wa 50 tangu
tuoane mwaka 1962," alisema.
Aliongeza, kuwa anaamini ndoa yao
ilikuwa mipango ya Mungu ndio maana wamedumu na kuzeeka pamoja wakiwa
ndio kwanza wanapendana kama wameoana jana, jambo ambalo linamfanya kila
mara kumshukuru Mungu.
MKEWE
Pili Bint Said Kitwana, alikiri kwamba
ndani ya uhusiano wa kimapenzi hadi kuja kuoana na Gurumo alipitia
katika misukosuko mingi, lakini anashukuru Mungu alijaliwa uvumilivu na
kuidumisha hadi leo.
Mama huyo alisema ugomvi wake mkubwa na
mumewe ilikuwa ni tabia yake ya ulevi, hali iliyomfanya mara kwa mara
kukwaruzana nae akimsihi aache.
Alisema, kuna wakati mumewe alikuwa
akiondoka nyumbani Ijumaa kwenda kwenye maonyesho na asionekane hadi
Jumatatu akiletwa na rafiki zake akiwa 'bwii', kitu kilichokuwa
kikimuuma.
"Tatizo kubwa baina yangu na Gurumo ilikuwa suala la ulevi, hata alipokuja kuacha sikuamini," alisema.
Aliongeza, jingine ni tabia ya kuwa na
'kuchakachua nje', na kumfanya aumie roho hasa wanawake zake wa nje
kumfuata na kumtukana na hata wakati mwingine kutaka kupigana nao hasa
anapoamua kuambatana nae kwenye maonyesho.
Alisema, ukiondoa matatizo hayo, Gurumo
ni mume bora, mpole, mkarimu na baba anayejali familia mwenye mapenzi
ya dhati, ndio maana aliamua kumvumilia hadi leo na kutoa wito kwa
wanandoa wengine kuvumiliana katika ndoa zao ili kuzifanya zidumu kama
ilivyo kwao.
Pia, alisema kitu kinachomfurahisha kwa
Gurumo ni tabia ya kutochagua chakula cha kula, akidai hula chakula
chochote isipokuwa 'kitimoto'.
Mama huyo alisema kwa namna mumewe
alivyojitolea ndani ya taifa hili kupitia fani yake ya muziki ni vema
serikali ikamkumbuka kwa kumsaidia angali akiwa hai, badala ya kusubiri
aje afe ndipo wajitokeze kumwagia sifa lukuki.
"Naiomba serikali imsaidie mzee huyu,
huwa naumia roho tunapokuwa tukipelekana klinini jinsi abiria ndani ya
daladala wanavyotushangaa, najua ni kutokana na jina kubwa la Gurumo na
hali aliyonayo kimaisha," alisema.
Aliongeza, ingelikuwa ni amri yake
angependa kuona Gurumo akipumzika masuala ya muziki baada ya kuutumikia
kwa zaidi ya miaka 50.