Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
ameuliza maswali saba ya msingi kwa wajumbe wa Bunge la Katiba
wanaopinga Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume yake akitaka wawajibu
wananchi ili kutuliza kiu yao.
Jaji
Warioba ambaye tangu awasilishe Rasimu ya Katiba Desemba 30, mwaka jana
amegeuka kuwa adui kwa watu wanaotaka muundo wa serikali mbili,
aliuliza maswali hayo jana katika uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa
Taasisi ya Twaweza kuhusu mchakato wa Katiba.
Akizungumza
kwa ukali, Jaji Warioba alisema: "Kwanza, jibuni kwa nini mnapinga
muundo wa Muungano wakati walioupendekeza ni wananchi?
"Sheria
inasema uwepo wa Muungano na mapendekezo katika rasimu hayasemi
Muungano usiwepo. Kumbukeni kuwa wananchi walitakiwa kutoa mapendekezo
ya namna ya kuboresha Muungano."
Katika
swali lake la pili, Warioba alisema kwa nini Tanganyika imevaa koti la
Muungano? Kwa kuwa katika ukusanyaji wa maoni wananchi walieleza kuwa
Serikali ya Muungano ya sasa siyo ya Muungano, ni ya Tanganyika.
Katika
swali la tatu alisema wajumbe hao wanatakiwa kujibu maelezo ya wananchi
ambao waliieleza tume hiyo kuwa Katiba imevunjwa na madaraka ya rais
yamechukuliwa na sasa kuna marais wawili katika nchi moja.
"Tume
inapewa lawama kubwa, wajibuni wananchi hii tume ilitumwa na nani
kukusanya maoni ya wananchi? Waambieni ilikusanya maoni hayo kwa kutumia
sheria ipi zaidi ya ile ya Mabadiliko ya Katiba?" alisema Jaji Warioba
katika swali lake la nne.
Katika
swali lake la tano, Warioba aliwataka wajumbe hao kutoa sababu za
kumtuhumu kuwa amependekeza muundo wa serikali tatu kwa sababu yeye
pamoja na (Joseph Butiku) walikuwa wajumbe wa Tume ya Jaji Kisanga na
Jaji Nyalali ambazo nazo zilipendekeza muundo wa serikali tatu, kitu
ambacho alisema si kweli na hawakuwahi kuwa mjumbe wa tume hizo.
Pia,
aliwataka wajumbe hao kujibu swali la sita, kwa nini hawataki
kuzungumzia yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na badala yake wanageuza
rasimu hiyo kuwa imeandikwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Katika
swali lake la saba, aliwataka wajumbe kujibu kwa nini wanaishutumu Tume
ya Mabadiliko ya Katiba kuwa imeingiza maoni yake, wakati ilikusanya
maoni hayo kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba?
Alisema
badala ya kujadili hoja za msingi, wajumbe wa Bunge hilo wamekuwa
wakitoa lugha za kejeli na matusi kwa baadhi ya watu (akiwamo na yeye),
kitendo ambacho alisema si sahihi na kinaweza kuligawa taifa kwa sababu
yaliyomo katika Rasimu ya Katiba yametokana na maoni ya wananchi.
Katika
uzinduzi huo walikuwepo baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo ambao ni Dk
Hamisi Kigwangalla aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana, Julius Mtatiro, Maria Sarungi na aliyekuwa mjumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole