Mtoto, Hamisi Hashimu Liguya (13) wakati akiwasili nchini India kwa matibabu.
Hamisi
aliyekuwa akisumbuliwa na uvimbe mkubwa wa mguu wa kushoto kiasi cha
kushindwa kutembea na kuishia kutambaa amerejea akiwa na matumaini ya
kutimiza ndoto zake.
Mtoto huyo alipatiwa matibabu kwenye
Hospitali ya Ganga, Tamil Nadu, India ametua Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNI) jijini Dar mwishoni mwa wiki iliyopita
akiambatana na baba yake mzazi, Hashim Liguya. Daktari
wa hospitalia hiyo, Raja Sabapathy kwa niaba ya madaktari wenzake
amemwandikia mmoja wa waandishi wetu barua pepe akifurahia kitendo cha
Hamisi kutembea ingawaje kwa msaada wa magongo.
Mtoto Hamisi Hashimu Liguya akiwa na baba yake mzazi hospitalini nchini India.
“Uwezekano
wa Hamisi kupona ulikuwa mdogo, lakini Mungu ametenda miujiza, baada
ya kuukata mguu wake na kumtengenezea wa bandia, tulifurahi kuona
ameuumudu vyema mguu huo,” aliandika Dk. Sabapathy.
Daktari huyo aliongeza kuwa, Hamisi
amekuwa na furaha baada ya kumuondolea uvimbe wa kilo tano katika mguu
wake na kusisitiza kuwa mtoto huyo anahitaji mazoezi ya kila siku ili
kuuzoea mguu wake wa bandia.Hamisi Hashimu Liguya akiwa Hospitali ya Ganga, Tamil Nadu, nchini India kabla ya kukatwa mguu.
Mara
baada ya kutua uwanja wa ndege, Hamisi alisema kuwa ameyafurahia
matibabu aliyoyapata India, kwani hakutegemea kama angeweza kwenda na
kurudi akiwa anatembea na kuwa na matumaini mapya.
“ Nimefurahi sana, naamini sasa nitaweza
kutimiza ndoto zangu kwa kuwa, naweza kutembea,” alisema Hamisi huku
akiwashukuru Watanzania kwa misaada waliyopitia kupitia Global
Publishers na Mtangazaji Hoyce Temu.
Mtoto Hamisi akifanya mazoezi.
Baba
mzazi wa mtoto huyo alitoa shukrani zake za dhati kwa Watanzania wote
waliojitolea kumchangia mtoto wake na kusema kuwa hana cha kuwalipa
zaidi ya kuwaombea dua na kuwataka waendelee na moyo huohuo kwa watu
wengine.
“ Furaha yangu imezidi kikomo, sikuwa na
matumaini ya kumuona mwanangu akitembea tena, nawashukuru Watanzania
kwa wema wao,” alisema baba huyo.
Mtoto Hamisi wakati akipokelewa nchini India.
Watanzania
waliitikia wito wa kumchangia fedha Hamisi baada ya kuhamasishwa na
Kampuni ya Global Publishers wachapishaji wa Magazeti Pendwa Tanzania
na Mtangazaji wa Kipindi cha Mimi na Tanzania, Hoyce Temu. Pia, hamasa nyingine zilitoka kwa Kikundi cha Mkono kwa Mkono ambacho kilionesha jitihada za kumsaidia Hamisi.
Hamisi aliondoka Tanzania, Februari 28,
mwaka huu kwenda India kwa ajili ya matibabu hayo akiwa anasumbuliwa
na ugonjwa ambao kitaalam unajulikana kwa jina la plexiform
neurofibromatusis.