Nahodha wa kivuko cha Korea Kusini kilichozama na kusababisha watu zaidi
ya 300 kutojulikana walipo amekamatwa Jumamosi (19.04.2014) kwa tuhuma
za uzembe na kuwatelekeza watu waliokuwa kwenye shida ya kuhitaji
msaada. Wapelelezi wamemkamata Lee Joon -Seok na wafanyakazi wenzake
wawili mapema leo asubuhi na wote watatu wameshutumiwa kwa kuwatelekeza
mamia ya abiria waliokuwa wamenasa ndani ya chombo hicho na kuhangaika
wenyewe kujiokowa. Mahakama imesema imeamuru kukamatwa kwao ili kuzuwiya
watuhumiwa hao kukimbia au kuharibu ushahidi.
Nahodha huyo mwenye umri wa miaka 68 yuko chini ya uchunguzi kwa kuwa
miongoni mwa watu wa mwanzo kuitelekeza meli hiyo wakati abiria wake
wakiwa bado wako hatarini.Lee amefunguliwa mashtaka ya uzembe na
kushindwa kuhakikisha usalama wa abiria kinyume na sheria za
bahari.Abiria waliambiwa kupitia vipaza sauti kwamba wabakie hapo walipo
licha ya kuwa meli hiyo ilikuwa ikizama upande mmoja.
Nahodha atetea uamuzi wake
Watu 32 imethibitishwa kuwa wamekufa katika janga hilo na wengine 270
hawajulikani walipo wengi wao ni watoto wakiwa katikasafari ya shule ya
upili.
"Naomba radhi kwa wananchi wa Korea Kusini kwa kusababisha janga hili na
nainamisha chini kichwa changu kuomba radhi familia za wahanga" Lee
amewaambia waandishi wa habari wakati akiondoka katika mahakama ya
Wilaya ya Gwangiu Tawi la Mokpo kuelekea gerezani leo asubuhi. Lakini
ametetea uamuzi wake ulioshutumiwa vikali wa kusubiri dakika 30 kabla ya
kuamuru kuchukuliwa kwa hatua za kuondolewa kwa abiria.
"Wakati huo mawimbi yalikuwa makali sana, hali ya bahari ilikuwa ya
baridi,na nilifikiri kwamba iwapo watu wataondoka kwenye kivuko hicho
bila tafakuri inayofaa na ikiwa hawakuvaa majeketi ya uokozi na hata
ingelikuwa wamevaa, wangelisombelewa mbali na maji na kukabiliwa na
matatizo mengine magumu" Lee amesema na kuongeza kwamba meli za uokozi
zilikuwa bado hazikuwasili na pia kulikuwa hakuna meli zozote zile za
uvuvi au mashua nyengine karibu wakati huo.
Watu wengi wangeliweza kuokoka
Wataalamu wamesema watu wengi zaidi wangeliweza kunusurika ingelikuwa
wameondoka kwenda vituo vya uokozi kabla ya meli hiyo kuegemea sana
upande mmoja na maji kuanza kujaa ndani.
Msaidizi wake wa tatu mwenye umri wa miaka 26 ambaye alikuwa na uzoefu
wa miezi sita katu hakuwahi kabla kuongoza meli hiyo kwenye njia hiyo na
ndie aliekuwa kwenye usukani wakati meli hiyo Sewol ilipozama.
Kwa mujibu wa sheria Lee alikuwa akitakiwa awe kwenye sitaha ya meli
ambapo nahodha hutowa amri zake ili kusaidiana na wenzake wakati meli
ikipita kwenye maeneo ya bahari chafu.
Mwendesha mashtaka mwandamizi Yang Jung-jin amewaambia waandishi wa
habari nahodha huyo alikimbia kabla ya abiria.Ukanda wa video uliorushwa
na shirika la habari la Yonhap umemuonyesha Lee akiwa miongoni mwa watu
wa kwanza kuwasili ufukweni kwa kutumia boti ya uokozi.
Yang amesema wafanyakazi hao wenzake wawili waliokamatwa walishindwa
kupunguza kasi ya mwendo wakati kivuko hicho kikiwa karibu na visiwa na
wameshindwa kuchukuwa hatua zinazohitajika kuokowa maisha.
Kulikuwa na abiria 476 na mabaharia kwenye meli hiyo ya tani 6,825
wakiwemo wanafunzi 320 na walimu 15 kutoka Shule ya Upili ya Danwon huko
Ansan karibu na mji mkuu wa Seoul wakati ilipoanza kupinduka na kuzama
ikiwa safarini kutoka Incheon kuelekea kisiwa cha kitalii cha Jeju
kilioko kusini.
Afisa wa
ulinzi wa mwambao Ko Myung-seok amesema meli 176 na ndege 28 leo
zimewekwa kufanya msako kwenye eneo karibu na ilikozama meli hiyo na
kwamba zaidi ya wapiga mbizi 650 wanajaribu kulifikia eneo la ndani ya
meli hiyo iliozama Jumatano.