Na Hudugu Ng'amilo
Askofu Mkuu
wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Palycarp Kardinali
Pengo amekemea ndoa za jinsi moja na zile za mkataba kwa sababu ni
kinyume cha maadili ya dini zote na zinachangia kuharibu familia.
Akizungumza
katika sikukuu ya mapadri na kubariki mafuta ya krisma katika Kanisa la
Mtakatifu. Joseph, Dar es Salaam, Pengo alisema ndoa za mkataba
zinachangia kwa kiasi kikubwa wanandoa kutokuwa waaminifu na kujiingiza
katika vitendo viovu ambavyo vinazaa familia ambazo hazina maadili.
"Kuna
wanandoa wanaona kukaa na mwenza wake kwa muda wote ni jambo ambalo
halikubaliki, wanajiingiza katika ndoa za mkataba ili waweze kufanya
matendo mengine ambayo hayampendezi Mungu na hapo ndipo wanajenga
familia isiyokuwa na maadili," alisema.
Kuhusu
ushoga, Pengo alisema: "Hatuwezi kuwa na familia imara kama hatutakemea
mazingira haya ya ndoa za jinsi moja na hatuwezi kuzungumzia uhai wa
kuwa na familia bora wakati kuna kikwazo ambacho hakiendani na maadili
ya dini zote."
Kardinali
Pengo pia aliwaonya mapadri wanaotumia fedha za kanisa kwa masilahi
binafsi akiwataka kuacha tabia hiyo mara moja. Alionya kwamba endapo
watabainika, kanisa halitatoa fedha kulipa faini au fidia itakayotokana
na uzembe huo.
Aliwashukuru
waumini wa Dar es Salaam kwa kumpatia zawadi ya Sh43 milioni wakati wa
maadhimisho ya miaka 30 ya uaskofu na kuahidi kuzitumia katika ujenzi wa
Shule ya Msingi Kisiwani iliyopo Mafia.
CHANZO MWANANCHI.