Watu 25 wamethibitika kufa mkoani Dar es Salaam
nchini kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kwa siku tatu
mfululizo kuanzia Ijumaa hadi Jumapili iliyopita.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,
Sadik Meck Sadik amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo akisema watu
wengine 14 wanadaiwa kufa, lakini hawajathibitishwa na polisi.
Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam wenye wilaya
tatu, amesema watu 11 wamekufa katika wilaya ya Ilala, huku wengine
wawili hawajaonekana mpaka sasa.
Taarifa kutoka wilaya ya Temeke imesema watu
saba wamethibitishwa kufa kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua
kubwa iliyonyesha.
Pia kuna taarifa za watu 21 kufariki dunia katika wilaya ya Kinondoni, japo hawajathibitishwa.
Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam Bwana Sadik
amesema miundombinu ya barabara na madaraja imeanza kurejeshwa baada ya
kuharibiwa na mafuriko na kusababisha mkoa wa Dar es Salaam kukosa
mawasiliano ya ndani na pia kukosa mawasiliano na mikoa jirani.