Lakini sina cha kufanya. Ni kweli Recho ameondoka. Hapa nataka nizungumzie kidogo maisha yangu na marehemu Recho.
Marehemu Rachel Haule ‘Recho’ akiwa na mumewe Saguda enzi za uhai wake
Kama inavyokuwa kwa wanadamu wengi kupitia changamoto maishani, Recho
naye alipitia mitihani ya hapa na pale ya kidunia lakini hakuvunjika
moyo. Alipambana kuhakikisha ndoto zake za kuwa mwigizaji mkubwa Bongo
na nje ya Bongo zinatimia.Kabla ya jina lake halijaanza kujulikana katika vyombo vya habari, Recho alikuwa akijaribu kukaa karibu na mastaa wakubwa ili aweze kupata uzoefu na baadaye kusimama mwenyewe kwenye sanaa.
Aliweka kambi ndani ya Kampuni ya RJ chini ya wa uongozi wa Ray na Johari akajielimisha na kupata mwanga wa maisha yake kisanii. Akaanza kuonekana katika sinema chache za kushirikishwa.
Aliuza kwenye sinema kubwakubwa kama Danger Zone, Family Disaster, Long Hope (haijatoka), Mke Mwema, Gentlemen, Cindy, Life to Life, Loreen, Uyoga, Men’s Day Out, Unpredictable na Figo ambayo alicheza na Jennifer Kyaka ‘Odama’.
Tangu hapo akaanza kushirikiana na mastaa wengine kama Jacqueline Wolper na wengine kisha baadaye akakita nanga kwa rafiki yake kipenzi, Odama wakaendelea kufyatua filamu mpya kila mwezi.
Kwa kipindi chote hicho niweke wazi tu, nilikuwa karibu na marehemu.
Niweke wazi pia kuwa nilikuwa bega kwa bega na mchumba wa marehemu, George Saguda. Tulikuwa tukishirikiana mambo mengi kama vijana, naweza kusema walikuwa hawanifichi kitu iwe ni cha kuhusu kazi au binafsi.
Kampani yetu ilikuwa ni ya shida na raha, marehemu na mchumba’ke hawakuwa wakijisikia hata baada ya kuwa maarufu katika jamii.
Ilikuwa ni suala la Recho au Saguda kunipigia simu na kuniambia tukutane, tunakutana kuzungumza, kushauriana huku pia tukinywa na kufurahi.
Ilikuwa ni rahisi Saguda au Recho kuniambia kazi au mipango ya kufanya kazi sehemu kabla ya kumwambia mtu yoyote. Hapa nakiri, kutokana na kazi yangu ya uandishi, kuna wakati nilikutana na changamoto kubwa.
Recho na Saguda walikuwa nami bega kwa bega na kunishauri mambo ya busara.
Naamini hata mimi yapo mengi mazuri ambayo katika kazi yao nimeweza kuwashauri, wao wenyewe wanajua. Tulishaurina kama vijana. Kweli kadiri siku zilivyozidi kusonga mabadiliko kati yetu yalianza kuonekana.
Kama ujuavyo Waswahili, kutokana na ukaribu wangu na Recho, kuna wakati yaliwahi kuibuka manenomaneno juu ya uhusiano wangu naye.
Tuliyapotezea kwani zaidi ya urafiki wa kawaida, hakuna kingine cha ziada kilichoendelea kati yetu.
Nilimheshimu na nitamheshimu Recho. Nilimheshimu na ninamheshimu sana Saguda. Naamini hata kama Saguda alisikia uvumi uliomhusu mchumba’ke na mimi, aliupotezea na kuuona wa kijinga kama nilivyofanya.
Hata baada ya wawili hao kutofanya kazi kwa karibu na RJ ambapo mara nyingi tulikuwa tukikutana kuzungumza, tulikuwa tukikutana kwenye viunga tofauti vya jiji, maisha yakiendelea.
Mwezi mmoja uliopita nilikaa na Saguda kwenye Ukumbi wa Eagle uliopo Sinza-Mapambano, Dar.
Tulikunywa na kufurahi, hatukuzungumzia kabisa ishu ya Recho ambaye muda huo nilikuwa nikijua ni mjamzito aliyebakiza siku chache ajifungue ndiyo maana alikuwa haonekani kwenye viunga vyetu.
Recho ambaye tulikuwa tukiwasiliana mara kwa mara kwa njia ya simu, alipopata taarifa ya kifo cha Adam Kuambiana hivi karibuni, alinipigia simu na kunieleza kwamba hataweza kwenda msibani kutokana na hali yake ya ujauzito.
Nilimwelewa lakini pia alinieleza jinsi marehemu Kuambiana alivyomtabiria jina la mwanaye mtarajiwa.
Hapo ndipo nilipoandika habari katika gazeti hili wiki iliyopita kwenye ukurasa wa tatu iliyokuwa na kichwa cha habari; “Kuambiana alimtabiria mtoto Recho.” Alimtabiria mtoto wa kiume, kweli ikawa hivyo lakini alifariki dunia saa chache baada ya kujifungua kabla ya kufuata yeye.
Wiki iliyopita, Recho alinisisitiza tuonane kwani mara nyingi alikuwa akipanga tuonane bila mafanikio. Alinieleza kuhusu ukimya na usiri wake wa kutangaza ujauzito katika vyombo vya habari kwani alihofia ndugu zake kujua ikiwa bado alikuwa hajaolewa, aliogopa aibu kama mtoto wa kike.
Jumapili iliyopita nilimpigia simu kujua anaendeleaje na lengo likiwa ni kutaka kutimiza ahadi yetu ya kuonana, simu yake haikuwa hewani.
Hata nilipojaribu kupiga tena na tena, hakupatikana. Muda huo ndiyo alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Lugalo, Dar, akajifungua kisha kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipoaga dunia.
Inaniuma sana, lakini mbele yake nyuma yetu. Kwaheri rafiki kipenzi Recho. Pumzika kwa amani!