‘Sijavuruga ndoa ya Vicky Kamata’
Dar es Salaam. Suala
la kukwama kufungwa kwa ndoa ya Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Vicky
Kamata limechukua sura mpya baada ya mzazi mwenza wa mchumba wa mbunge
huyo, kukanusha taarifa kwamba alikwenda Dodoma kwa lengo la kuomba
msaada kwa viongozi wa Bunge.
Kauli ya mama huyo imezidisha utata
katika sakata la kukwama kufungwa kwa ndoa hiyo iliyokuwa ifanyike
Jumamosi baada ya kutokea habari kuwa mwanamke mmoja alikwenda bungeni
mjini Dodoma kutaka kuonana na Spika kwa lengo la kuomba Bunge limsaidie
kupata haki yake kabla ya harusi hiyo kufungwa na hivyo kusababisha
harusi kutofanyika.
Kamata, ambaye alijizolea umaarufu
kutokana na wimbo wake wa “Wanawake na Maendeleo” na baadaye kuingia
bungeni katika uchaguzi wa mwaka 2010, alikuwa afunge ndoa na mtu
aitwaye Charles Gardiner Jumamosi iliyopita jijini Dar es Salaam, lakini
haikufanyika kutokana na mbunge huyo kuwa mgonjwa kiasi cha kulazwa
hospitali maeneo ya Tabata.
Jana, Kinavi Dadi, ambaye ni mzazi mwenza wa Gardiner, alikanusha kufunga safari hadi Dodoma kwa lengo hilo.
“Ni kweli kwamba Charles ni baba watoto
wangu, lakini sijawahi kwenda Dodoma na wala sifahamu chochote kuhusu
safari hiyo. Nadhani inatosha,” alisema mama huyo na hakutaka mazungumzo
zaidi.
Baadaye kidogo mmoja wa ndugu wa Kinavi,
ambaye aliomba asitajwe jina lake gazetini, alikiri ndugu yao kufunga
ndoa na Gardiner Juni 2004 na kujaliwa kupata watoto wawili, lakini
walitofautiana na baadaye ndoa yao kuvunjwa mwaka 2012.
“Ni kweli kwamba dada yetu alifunga ndoa
na Charles, lakini pia ni kweli kwamba walipeana takala halali two
years ago (miaka miwili iliyopita), kwa hiyo taarifa kwamba eti amezuia
ndoa isifungwe, siyo za kweli na wala huko Dodoma hajawahi kwenda,”
alisema.
Alisema taarifa kwamba aliyepata kuwa
mke wa Gardiner alikwenda Dodoma kuomba msaada wa Bunge zimewaumiza sana
kama familia kutokana ukweli kwamba Kinavi ndiye anayefahamika kuwa mke
wa kwanza.
“Ndugu yetu analia sana kutokana na
kuumizwa na wale wanaomchafua. Sisi katika familia tumelelewa kwa
maadili hivyo Kinavi siyo mtu wa kuzuia ndoa ya Gardiner maana
walishatengana, mawasiliano yaliyopo ni yale yanayohusu watoto ambao
wana haki ya wazazi wote wawili. Hatujui waliozitangaza hizo habari
walikuwa na malengo gani,” alisisitiza.
Bungeni Dodoma
Wakati hayo yakiendelea, habari kutoka
bungeni Dodoma zinasema mwanamke aliyedaiwa kuwa mke wa Gardiner ni
‘feki’ na alikuwa wa kutengenezwa na baadhi ya wabunge kwa lengo la
kumtibulia Kamata.
Mpango huo unadaiwa kuwahusisha wabunge
wanawake wanne; watatu kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) na mmoja kutoka
Chadema ambao awali waliapa kwamba ndoa ya mbunge mwenzao isingefungwa.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, waandishi
wa Mwananchi waliopo Dodoma walimsaka mwanamama huyo bila mafanikio na
baadaye waliambiwa kwamba haikuwa rahisi kumwona kwani hakuwa halisi.
Kundi la wabunge hao ndilo lilimwingiza
mwanamke huyo katika viwanja vya Bunge kwa lengo la kumkutanisha na
viongozi wa taasisi hiyo, lakini mpango huo ulishindikana.
Mwishoni mwa wiki, Naibu Spika Job
Ndugai alisema anakumbuka kwamba alipewa taarifa za kuwapo kwa mwanamke
anayemtafuta, lakini hadi alipoondoka kwenda jimboni kwake Kongwa hakuwa
ameonana naye.
“Walioniambia ni wabunge fulani na
walikuwa kama wanafanya utani, lakini hadi naondoka kuja huku Kongwa,
maana niko vijijini kwa sasa, sikubahatika kuonana naye kwa hiyo
simfahamu kwa jina, wala sura yake, wala anakotoka sikufahamu,”alisema
Ndugai.
Juzi Kamata aliliambia gazeti hili
kwamba naye alisikia taarifa za kuwapo kwa mwanamke huyo mjini Dodoma,
lakini hakuweza kufahamu ni nani kutokana na kwamba alikuwa bado
amelazwa hospitalini.
Mbunge huyo alilazwa kwa siku sita
katika Hospitali ya Tabata General, iliyopo Segerea, Dar es Salaam na
aliruhusiwa juzi. Anatarajia kwenda Dodoma wakati wowote.
Mapenzi ya Mungu
Mbunge huyo juzi alizungumzia kutofungwa kwa ndoa yake na kusema anaamini kilichotokea “ni mapenzi ya Mungu”.
Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake,
Sinza jijini Dar es Salaam, Kamata alisema ingawa ndoa hiyo
haijafungwa, moyo wake una amani kwa kuwa alimwomba Mungu kuhusu suala
hilo kwa muda mrefu na hicho ndicho Mungu alichojibu.
“Hii ni mipango ya Mungu. Wakati wa
maandalizi ya ndoa tulikuwa na timu ya wanamaombi. Tuliomba sana na
baada ya kuiombea ndoa, tuliomba mapenzi yake yatimizwe. Kwa hiyo haya
ni mapenzi yake,” alisema.
Kamata alisema licha ya kuwa tukio la
kutokufungwa kwa ndoa hiyo kuwa zito na ambalo lingeweza kumjeruhi moyo,
amekuwa na amani tofauti na ndugu, jamaa na marafiki zake wengi
walivyodhani.
“Mimi mwenyewe nilikuwa najishangaa,
mbona nina amani. Nashangaa tarehe 24 inapita hivi hivi, na ikathibitika
ndoa haijafungwa, lakini bado nina amani,” alisema.
Aliongeza kuwa anaamini kutokufungwa kwa
ndoa yake kuna sababu ambazo Mungu mwenyewe anazijua na wala hawezi
kumlaumu mtu au kulaani chochote kilichoingilia kati kufungwa kwa ndoa
hiyo.
“Naamini ni mipango ya Mungu, yeye ana
makusudi yake. Huwezi kujua ndoa ingefungwa nini kingetokea, lakini nina
amani moyoni na maisha yanasonga mbele,” alisema.
Kuhusu maandalizi ya harusi, alisema
mipango mingi ilishafanyika na baadhi ya fedha zililipwa, lakini
majadiliano yanafanyika kama waliokwishalipwa wanaweza kurudisha angalau
nusu ya fedha.
Alisema baadhi ya fedha zilishalipwa kwa mpambaji, mpishi na mavazi ya harusi lakini ukumbi na vinywaji havikuwa vimelipiwa.