Mradi wa Bandari ya Mbegani – Bagamoyo, mkoani Pwani ndiyo mradi mkubwa wa uwekezaji nchini utakaoifanya wilaya hiyo kuwa na mwonekano mpya.
Aidha,
kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuliingizia taifa kiasi kikubwa
cha fedha na kuzalisha fursa nyingine nyingi za kiuchumi.
Serikali
ya Tanzania na Serikali ya China kupitia Kampuni ya China ya Merchants,
ziliingia mkataba wa makubaliano ya ujenzi wa bandari hiyo kwa
utaratibu wa ubia kati ya sekta ya Umma na sekta Binafsi (PPP).
Ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo, ambao hufanyika kwa kipindi cha miaka mitano mitano.
Kupitia
mradi huo, vipaumbele katika kipindi cha kwanza kuanzia 2011/12 –
2015/16 ni kufungua fursa za kiuchumi na uwekezaji katika sekta za
nishati, usafirishaji na Tehama.kiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara
ya Viwanda na Biashara kwa mwaka 2014/15 bungeni hivi karibuni, Waziri
wa wizara hiyo, Dk Abdallah Kigoda alisema kuwa wizara yake ina mpango
wa kulipa fidia kwa wakazi wa maeneo yaliyofanyiwa uthamini Bagamoyo na
maeneo mengine nchini.
Alieleza kuwa Mradi wa Bandari unahusisha Maendeleo ya Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (SEZ) katika eneo lenye ukubwa wa hekta 9,080 litakalojumuisha shughuli za ujenzi wa barabara, mitandao ya mawasiliano, mifumo ya maji na umeme.
Shughuli
zitakazofanyika katika eneo hilo ni pamoja na viwanda, vituo vya
biashara, vivutio vya utalii, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,
Huduma ya Makazi, Taasisi za Fedha na Makao Makuu ya Mkoa.
Alisema
kukamilika kwa ujenzi wa Bandari ya Mbegani Bagamoyo kutasaidia
kupunguza foleni kwa kiasi kikubwa katika Bandari ya Dar es Salaam na
kuifanya Tanzania kuwa na bandari kubwa na ya kisasa katika Ukanda wa
Afrika Mashariki na Kati.
Dk
Kigoda alisema wataanza uendelezaji wa miundombinu ya msingi kwa Maeneo
Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZ) na Maeneo Maalumu ya
Kiuchumi (SEZ) yaliyolipiwa fidia kama vile Bagamoyo SEZ.
Aliongeza
kuwa kwa mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga Sh7 bilioni kwa ajili ya
kumalizia ulipaji fidia katika eneo la Bagamoyo.
Alifafanua
kwamba mwaka 2013/14, kampuni 31 zilipewa leseni za kujenga viwanda
chini ya Mamlaka ya EPZ na tayari kampuni nane zimeanza uzalishaji.
Kampuni hizo zinatarajiwa kuwekeza mtaji wa jumla ya Dola za Marekani
485 milioni na kuajiri watu 10,276.