Jeshi la Polisi limelazimika kutumia mabomu ya machozi
kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga) katika Soko Kuu la
Kariakoo.
Hamisha hamisha hiyo yenye baraka za uongozi wa
mkoa zilianza mapema mwezi uliopita kwa lengo la kuondoa biashara zisizo
rasmi katikati ya jiji la Dar es Salaam, pamoja na bodaboda, bidhaa
zimwagwazo chini, mama ntilie na vibanda vya vocha.
Majira ya saa tisa alasiri magari ya polisi
yaliwasili sokoni hapo huku yakiwa na askari polisi na mgambo waliokuwa
wamevaa fulana na kofia za Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa
(Talgwu), zenye rangi ya njano, na kuanza kuwakamata wamachinga hao.
Askari hao waliokuwa katika magari aina ya Land
Rover Defender na Toyota LandCruiser waliuvamia mitaa ya Kongo na
Mchikichini kufanya oparesheni hiyo kabla hawajalazimika kutumia mabomu
ya kutoa machozi ili kuwaondoa walengwa katika eneo hilo.
Hali hiyo ilizua tafrani kwa wateja waliokuwa
wakinunua bidhaa kwenye maduka hayo walioenda kwa ajili ya kupata
mahitaji yao walikimbia hovyo ili kujiokoa kutokana na vurugu hizo.
Maduka mengi ya mtaa huo, kuanzia kituo cha
daladala hadi sokoni, yalilazimika kufungwa kwa hofu ya kupoteza mali
kutokana na vibaka wanaotumia nafasi kama hizo kuiba vitu.
Kazi haikuwa rahisi kwa askari hao kwani
wamachinga kadhaa hawakuwa tayari kuona wakikamatwa au kupoteza mali zao
hivyo kulazimika kupambana kwa kile kilichoonekana kama kuwa radhi
‘kufia mali’ zao. Wamachinga hao waliokaidi amri halali ya jeshi hilo,
walikamatwa na kuingizwa kwenye gari la polisi .
Watu walionekana wakikimbia hovyo na wengine
wakipanda gari lolote bila kujali linaelekea wapi ili mradi waondoke
eneo la tukio kabla hawajapatwa na lolote na kuumia au kuibiwa. “Sisi
tutaenda wapi bwana. Acha wafanye mambo yao wakiondoka tunarudi tena
kuendelea na biashara zetu,” alisema Hamis Jumanne, anayefanya biashara
ya kuuza maji.
Kamanda wa Polisi Mkoa kipolisi wa Ilala, Marietha
Minangi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa zoezi la kuondoa
wamachinga jijini ni endelevu.
chanzo;Mwananchi