BABU aliyefunga ndoa mwaka 2011 akiwa na umri wa miaka 94,
Mathias Kisokota mkazi wa Kitongoji cha Isunta, Namanyere wilayani Nkasi ambaye
kwa sasa ana umri wa miaka 97, amehamia na mkewe katika Mji wa Mpulungu mwambao
wa Ziwa Tanganyika nchi jirani ya Zambia miezi sita iliyopita kwa lengo la
kufanya tambiko la kumwezesha mkewe mwenye umri wa miaka 83 kupata mtoto wa
uzeeni.
Mke wa mzee huyo, Uria Mwamanzi ni mwenyeji wa nchi jirani
ya Zambia alizaliwa na kukulia katika Mji wa Mpulungu mwambao mwa Ziwa Tanganyika
ambapo kwa mujibu wa wajukuu zao ndiko babu yao alipokutana naye na kuwa na
mahusiano hadi walipofunga ndoa miaka mitatu iliyopita.
Wanandoa hao ambao waliacha gumzo kubwa baada ya kufunga
pingu za maisha katika Kanisa
Katoliki la Mtakatifu Anthony, alasiri ya Juni
18, 2011 mjini Namanyere Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi.
Akizungumza na mwandishi wa habari kwa njia ya simu kutoka
katika Mji wa Namanyere jana, Salvatory Adolf (19), mjukuu wa wazee hao kutoka
kwa mtoto wao kitindamimba mwenye umri wa miaka 40 sasa, alisema babu yake
amemsindikiza mkewe huyo ili kwenda kutambikia mizimu ya kwao.
“Bibi hakuwa na raha mara kwa mara alikuwa akitamani kurudi
nchini kwao Zambia kuwasalimia nduguze pia akiwa huku alikuwa akiugua mara kwa
mara hivyo babu aliona bora amsindikize bibi akatambike kwa mizimu ya babu zake
nchini humo,” alisema.
Hata hivyo, hakutaka kueleza kwa undani juu ya kiu ya babu
yake ya kutaka kupata mtoto, habari ambazo zinazungumzwa na watu wa karibu
waliopo ndani ya familia ya wanandoa hao.
Miongoni mwao, Agnes ambaye ni mtoto wa mwisho wa Mzee
Kisokota akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu kutoka mjini
Namanyere, Nkasi alisema baba yake amekuwa na hamu hadi sasa ya kupata mtoto
katika ndoa yake changa. “Anasali sana akiomba kila siku apate mtoto katika
ndoa yake.
Bado ana matumaini makubwa ….. nikianza kukusimulia
tutakesha, tena anasema siku akijaliwa mtoto katika ndoa yake hiyo atajawa na
furaha kubwa na kufanya sherehe ya aina yake… amemsindikiza bibi (mkewe) Zambia
kusalimia ndugu zake pia kutambika kwa kuwa baba ana hamu ya mtoto atatumia
fursa hii nae kutambikia kwa wakwe zake ili mkewe huyo ashike mimba,“ alieleza
Agnes.
Hali hiyo inakuja licha ya ukweli kwamba, umri wa mke wa
Mzee Kisokoto kuzaa umeshapitiliza, lakini kwa pamoja wamedaiwa kuamini kwa
Mungu hakuna kisichowezekana hivyo anaweza kutenda miujiza kwa kuwapa baraka ya
mtoto wa ndoa yao ya uzeeni.
Mjukuu huyo alipoulizwa juu ya ziara hiyo kuhusisha pia
kusaka mtoto kutoka kwa `mizimu’ ya ukoo wa mke wa babu yake, hakuwa na majibu
ya moja kwa moja.
“Bibi alipoondoka alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya mwili
lakini tangu atambike nchini Zambia inadaiwa amepona kabisa na sasa wanaishi
raha mustarehe na babu… ila watarudi huku kwetu baadae mwaka huu …”, alisema.
Katika safari ya wazee hao, Adolf anasema bibi na babu yake
walisindikizwa na Claudio Mathias (21), kaka wa mjukuu huyo na kwamba kaka huyo
amesharejea nchini.
Wanandoa hao kwa mujibu wa wajukuu zao kabla ya kufunga ndoa
katika Kanisa Katoliki Jimbo la Sumbawanga mjini Namanyere miaka mitatu
iliyopita walikuwa wakiishi ‘kinyumba’ kila mmoja wao akibahatika kuwa na
watoto katika mahusiano yake ya awali.
Kwa pamoja wana wajukuu zaidi ya 30 na vitukuu zaidi ya 40
wengi wao wakiishi nchi jirani ya Zambia. Mzee Kisokoto alifiwa na mke wa