TAASISI
ya Sayansi ya Afya ya Chuo Kikuu cha Eckernforde Tanga, inatuhumiwa
kuwatapeli wanachuo zaidi ya 115 iliyowadahili na kukaa chuoni hapo
miezi sita kisha kuwafukuza kwa madai kuwa hawana vigezo vinavyotakiwa
na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Hata hivyo, wanachuo hao walifukuzwa baada ya kuwa wamelipa ada, fedha ya chakula, malazi na michango mingine.
Kwa
mujibu wa nyaraka mbalimbali ambazo Tanzania Daima limeziona, chuo hicho
kilitangaza nafasi hizo kupitia gazeti la Mwananchi la Oktoba 31, 2012.
Tangazo
hilo lilisomeka; “Wito wa maombi kwa ajili ya kujiunga na kozi za cheti
na stashahada za sayansi za afya mwaka wa masomo 2012/2013.”
Kwa
mujibu wa tangazo hilo, waombaji wangesoma kozi hiyo kwa miaka miwili
ngazi ya cheti, huku wale ngazi ya stashahada wakisoma kwa miaka mitatu.
Sifa
zilizoainishwa katika tangazo hilo ni kwamba mwanafunzi atakayesajiliwa
ni aliyefaulu masomo manne, likiwemo moja la sayansi.
“Mwombaji
lazima awe na ufaulu wa pasi tatu katika masomo ya sayansi, walau
daraja ‘D’ katika kemia, biolojia na hisabati au kidato cha sita akiwa
na pasi moja daraja ‘E’ katika somo lolote la sayansi,” lilisomeka
tangazo hilo.
Kila fomu
ya kujiunga ilinunuliwa kwa sh 20,000 ambapo fedha hizo zililipwa
kupitia benki ya NBC Tawi la Tanga, akaunti na 0201030006036.
Baada ya
wanachuo hao kudahiliwa kwa sifa zilizoanishwa, walisoma kwa miezi sita
na wakati wakiendelea na masomo, Wizara ya Afya ilileta vigezo tofauti
na vile vilivyokuwa vimeainishwa kwenye tangazo la awali.
Hatua
hiyo ilisababisha wanachuo 115 kuonekana hawana sifa, na hivyo kutakiwa
kuondoka au kufanya mitihani upya ili kuweza kukidhi sifa stahiki.
Badala ya
kufuata masharti ya wizara, Januari 2013, uongozi wa chuo uliwatoa
wasiwasi wanachuo kwa kuwaeleza kuwa hakuna suala la kujisajili kwa mara
nyingine kwa kuwa chuo hicho kipo chini ya Baraza la Elimu ya Ufundi
(NACTE), na kwamba wanatambuliwa.
Licha ya kupewa matumaini hayo, lakini Juni mwaka huo, walionekana hawana sifa na hivyo kuondolewa chuoni hapo kwa mizengwe.
Chanzo
chetu kilidokeza kuwa waliombwa na uongozi wa chuo kutofanya fujo ili
madai yao yashughulikiwe kwa utaratibu, hivyo walipewa hundi kwenda
benki kuchukua fedha.
Hata
hivyo, walipofika benki ya CRDB Tawi la Tanga, walielezwa kuwa hundi
hizo ni feki na waliporejea chuoni, walikuta ulinzi umeimarishwa,
wakalazimishwa kuondoka maneo hayo.
Baada ya
kufanyiwa utapeli huo, wanachuo hao walitoa taarifa kwa Mkuu wa Polisi
wa Wilaya ya Tanga Mjini, wakiomba kuandamana ili wafike kumwona Mkuu wa
Mkoa kumweleza kilio chao.
Licha ya
maandamano hayo, hakuna hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Mkoa wa
Tanga dhidi ya chuo hicho, hali iliyowalazimu kuondoka kurejea majumbani
kwao wakiwa wanadai fedha hadi leo.
Wanachuo hao wanadai fedha walizolipa kwa ajili ya chakula, malazi na vifaaa vya darasani ni sh 1,987,500 kila mmoja.
Pia zipo
gharama za usafiri kwa kila mmoja kutegemeana na mahali alikotoka, fedha
za usumbufu na hivyo kufanya madai yote kwa pamoja kufikia sh
353,069,600.
Mbali na
madai yao kufikishwa kwa mkuu wa mkoa bila kupatiwa ufumbuzi, pia
wanachuo hao wamewahi kumwandikia barua Waziri Mkuu, Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii na Baraza la Elimu ya Ufundi, ingawa hakuna
walikosikilizwa.
Alipotafutwa
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Chuwa Kiango, alitetea kuwa suala
linaloulizwa silo bali kuna tatizo jingine, huku akiomba apewe muda kwa
vile alikuwa akiingia kikaoni.
“Chunguza
upya, muulize aliyekupa taarifa hii, nitakupa maelezo nikitoka kwenye
kikao,” alisema Prof. Kiango ingawa baadaye alipopigiwa simu hakupokea.