Kamati ya nidhamu ya shirikisho la soka duniani FIFA imemfungulia
mashataka mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uruguay Luis Suarez kufuatia
tukio la kumng’ata beki wa timu ya taifa ya Italia Giorgio Chiellini,
wakati wa mchezo wa mzunguuko wa tatu wa kundi la nne ambapo The Azzuri
walikubali kufungwa bao moja kwa sifuri.
Kamati ya nidhamu imethibitisha kumfungulia mashtaka mshambuliaji
huyo mwenye umri wa miaka 26, baada ya kupata ripoti ya mchezo huo ambao
ulichezwa kwenye uwanja wa das Dunas, uliopo mjini Natal.
Hata hivyo kamati hiyo imetoa nafasi kwa Luis Suarez, pamoja na
shirikisho la soka nchini Uruguay kuwasilisha utetezi wao kabla ya
kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Nafasi kwa Suarez pamoja na shirikisho la soka nchini Uruguay
kuwasilisha vielelezo vya ushahidi wa kupinga suala hilo, imetolewa hadi
saa kumi na moja jioni kwa saa za nchini Brazil.
Tayari kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uruguay Oscar Tabarez
ameshajiondoa kwenye ushahidi huo, baada ya kukiri hakuliona tukio hilo
ambalo lilijitokeza katika kipindi cha pili cha mchezo huo.
Tukio la Suarez kumng’ata Chiellini lilitokea dakika kumi kabla ya
mchezo wa Italia na Uruguay haujamalizika, ambapo picha za televisheni
zilionyesha kwa kurudia rudia tukio hilo ambalo linadaiwa huenda
lilikuwa halali kwa mshambuliaji huyo wa klabu ya Liverpool kuonyeshwa
kadi nyekundu.