Baada ya kutolewa kwenye fainali za kombe la dunia za mwaka
huu huko nchini Brazil kwa kufungwa bao moja kwa sifuri na timu ya taifa
ya Uruguay, Cesare Prandelli ametangaza kujiuzulu nafasi ya ukocha wa
timu ya taifa ya Italia.
Prandelli, amesema maamuzi ya kujiuzulu aliyachukua mara baada ya
mchezo dhidi ya Uruguay ulipomalizika jana jioni kwa saa za hapa
nyumbani, ambapo amekiri kumfikishia salamu hizo raisi wa chama cha soka
nchini Italia Giancarlo Abete.
Kocha huyo ambae alikichukua kikosi cha Italia mara baada ya fainali
za kombe la dunia za mwaka 2010 zilizounguruma nchini Afrikla kusini,
amesema alikuwa hana budi kuchukua maamuzi ya kujiuzulu kutokana na
kushindwa kufikia lengo alilokuwa amejiwekea.
Amesema anaamini alipoiacha timu ya taifa ya Italia si pabaya sana,
hivyo kocha ajaye ataendeleza mazuri ambayo atayakuta na hatimae kufikia
malengo yanayotarajiwa na mashabiki wa soka nchini humo.
Hata hivyo amekanusha taarifa za kushurutishwa na mtu yoyote kuchukua
maamuzi hayo, na amewataka mashabiki wa soka nchini Italia kutambua
kwamba amefanya hivyo kwa maslahi ya taifa lake.