Mkuu wa shirikisho la kandanda, FIFA, Sepp Blatter amesema madai ya rushwa katika uchaguzi wa Qatar kuwa mwenyeji wa kombe la dunia 2022 yamechochewa na hisia za ubaguzi wa rangi.
Alisema haya alipokuwa akijibu madai yanayorushiwa baadhi ya wanakamati wa Fifa waliohusika na uchaguzi huo, wanaokabiliwa na tuhuma za rushwa.
"Kuna kimbunga kimeelekezewa Fifa tangu iichague Qatar. Inasikitisha sana kwamba yote yamechochewa na hisia za ubaguzi hasa wa rangi" Sepp BLATTER amenukuliwa kusema.
Blatter ameyasema hayo huko Sao Paulo, Brazil alipokuwa akizungumza na maafisa wa kandanda kutoka Afrika .
Ameahidi Fifa itakabiliana na chochote kinachobeba hata chembe ya kibaguzi.
Hata hivyo Fifa imeamua kufanya uchuguzi wake na imesema italiamulia swala hilo kati ya Septemba na October.
Katika kikao chao huko Sao Paulo, shirikisho la soka barani Afrika (CAF) nalo lilitoa cheche zake kwa vyombo vya habari vya kimataifa hasa magazeti ya Uingereza likisema ndio yaliyoanza kampeni hiyo dhidi ya Qatar na ya kuchafua jina la shirikisho hilo.
Wametaja swala hilo kuwa ni kampeni iliyojaa chuki na udhalalishaji.
Wametishia kuyafungulia kesi magazeti husika.
Wakili mmoja Mmarekani, Michael Garcia, amekuwa akichunguza utaratibu na vipi nchi zinavyochaguliwa kuandaa kombe hilo na atatoa ripoti yake hapo Julai.
Qatar ilishinda Australia, Japan, Korea Kusini na Marekani hapo Dec 2010 ilipochaguliwa na Fifa kama mwenyeji wa kombe la dunia 2022.
Qatar imekana vikali kuhusika na vitendo vyo vyote vya rushwa na kusema kuwa ilishinda kihalali.