Shule
ya Sekondari ya WAMA-Nakayama inayomilikiwa na Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo (WAMA) imepatiwa msaada wa basi na kampuni ya Ashok Leyland ya
jijini Dar es Salaam.Makabidhiano ya basi hilo yamefanyika leo katika viwanja vya Taasisi hiyo iliyopo wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.Akiongea
mara baada ya makabidhiano hayo Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete
aliwashukuru viongozi wa kampuni hiyo kwa msaada walioutoa na kusema
anaamini msaada huo wameutoa baada ya kuangalia vigezo maalum na
kuwaomba kuzidi kuwa na moyo wa upendo kwao na kwa wadau wengine.Mama
Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alisema Taasisi
ya WAMA inafanya kazi mbalimbali zinazoonekana na jamii moja wapo ikiwa
ni elimu na katika hilo wanashule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama ambayo
ni ya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi iliyoko
wilaya ya Rufiji mkoani Pwani ambayo inawanafunzi 335 wa kidato cha
kwanza hadi cha nne.
“Wenzetu
hawa wametoa basi ambalo litasaidia kutatua changamoto ya usafiri
shuleni kwani wanafunzi kama wanafunzi wanashughuli zao za ndani na nje
ya Shule. Kwa ukubwa wa basi hili tatizo la usafiri litakuwa limepungua
kwa kiasi kikubwa kwakuwa kabla ya kupata basi hili kulikuwa na
lingine dogo”, alisema Mama Kikwete.
Kwa
upande wake Bhimasena Rau ambaye ni Mkurugenzi Mwendeshaji Kimataifa
kutoka kampuni ya Ashok Leyland alimpongeza Mama Kikwete kwa kazi kubwa
anayoifanya ya kuisaidia jamii wakiwemo wanawake na watoto hapa nchini
na kusema kuwa wametoa basi hilo ambalo litasaidia katika kazi za
kijamii.
Taasisi ya WAMA ilianzishwa mwaka 2006 inafanya kazi katika eneo la elimu ya mtoto wa kike, afya, kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuangalia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi