MBUNGE wa Urambo Magharibi, Prof. Juma Kapuya (CCM), ambaye pia ni
Waziri wa Ulinzi wa zamani, jana alijikuta katika wakati mgumu wa
kuumbuliwa na mbunge mwenzake wa Temeke, Abbas Mtemvu (CCM), wakati
wawili hao wakibishania uuzwaji tata wa Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam
(UDA).
Hatua hiyo ilijitokeza wakati Mtemvu akichangia hotuba ya bajeti ya
Wizara ya Fedha na Uchumi kwa mwaka wa fedha 2014/2015, na kuungana na
wabunge wenzake kadhaa waliotangulia kuchangia, akidai UDA imeuzwa
kifisadi bila wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam kushirikishwa.
Wakati Mtemvu akiendelea kujenga hoja yake, Prof. Kapuya aliomba
kumpa taarifa, akimweleza kuwa mbunge kujishughulisha na uwekezaji si
dhambi na kwamba UDA imeuzwa kihalali wala hakuna ufisadi kama
inavyodaiwa, isipokuwa mbunge huyo anatumika kuwashawishi wabunge
kupinga suala hilo. Baada ya Prof. Kapuya kuketi, Mtemvu aliendelea kuchangia akidai kuwa
haipokei taarifa ya mbunge mwenzake kwa sababu yeye ni miongoni mwa
walioshirikia kuiuza UDA kifisadi akitumia nafasi yake ya uwaziri.
“Yaani mtu mzima unasimama hapa unasema kwamba UDA iliuzwa kihalali
wakati wewe ulitumia nafasi yako ya uwaziri kushiriki ufisadi huo?”
Alihoji Mtemvu na kuongeza kuwa yeye hatumiki bali Prof. Kapuya ndiye
anazunguka hotelini Dodoma kuwashawishi wabunge watetee uuzwaji wa UDA
na kutamba kuwa video kamera zipo zikimuonyesha akifanya hivyo.
Wakati Mtemvu akieleza hivyo, wabunge wengi walimshangilia kwa nguvu,
hususani wale wa kutoka Mkoa wa Dar es Salaam, ingawa Naibu Spika, Job
Ndugai, aliingilia kati na kumtaka ajielekeze kwenye hoja badala ya
kuendeleza mashambulizi binafsi.
Mkulo afunguka
Waziri wa Fedha na Uchumi wa zamani, Mustafa Mkulo amevunja ukimya na
kutoa siri ya uuzaji wa kiwanja cha Shirika Hodhi la Mali za Serikali
(CHC). Kiwanja hicho ambacho Mkulo alidaiwa kukiuza kifisadi ni kile kilichopo Barabara ya Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Akijibu tuhuma hizo kwa mara ya kwanza, Mkulo alisema kiwanja hicho
kimeuzwa kama ilivyouzwa UDA ambayo hadi sasa ipo kwenye mzozo mkubwa
unaoligawa Bunge.
Alisema yeye wala wizara yake, hawakuhusika na uuzwaji wa kiwanja
hicho ambacho kwa mara ya kwanza alitajwa bungeni kuwa mhusika mkuu na
mwizi namba moja. Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha na Uchumi kwa mwaka wa
fedha 2014/2015, Mkulo alisema waliohusika na uuzwaji wa kiwanja hicho
ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya CHC, Prof. Khamis Mahigi na aliyekuwa
Mkurugenzi wa shirika hilo, Methusela Mbanjo.
“Aprili mwaka 2012, nilituhumiwa kuuza kiwanja hicho, leo nataka
kutoa ufafanuzi kwa sababu nimepata nafasi, mimi sikuuza wala
sikushiriki mchakato wa kuuza kiwanja. “Bodi ya CHC iliandikia Wizara ya Fedha barua ya kuomba kibali cha
kuuza kiwanja chao, barua hiyo haikwenda wizarani isipokuwa ilikwenda
kwa Msajili wa Hazina, ambaye baada ya uchambuzi wa kina akatoa ushauri
kwa Katibu Mkuu naye akatoa mapendekezo yake kwa Waziri wa Fedha nini
kifanyike.
“Mapendekezo ya msajili yalionyesha udhaifu kwenye maombi ya CHC
ambapo baada ya kuona upungufu huo, nikiwa waziri nikaagiza bodi ifuate
taratibu, kanuni na sheria kisha ilete upya kwa sababu hiyo ni mali ya
serikali. “Baada ya siku chache wizara ikapata taarifa kwamba CHC ilikuwa
imeshapokea nusu ya gharama ya mauzo ya kiwanja kile, kwa maana kwamba
bodi ilikuwa imeshauza kiwanja na barua kwamba waziri atoe kibali
ilikuwa ni geresha,” alisema Mkulo ambaye ni mbunge wa Kilosa (CCM).
Mkulo alisema kuthibitisha kwamba hakuhusika na uuzwaji wa kiwanja
hicho, mkataba wake ulisainiwa miezi mitano baada ya yeye kuondoka
hazina. Alisema karatasi na nyaraka zote zilizotumwa kwenye magazeti zilikuwa feki, lakini zilitoka CHC.
Mkulo alisema wabunge waliomlipua bungeni walikuwa wakipita na nyaraka hizo huku wakimtuhumu kuwa yeye ni mwizi namba moja.
“Kiwanja hiki kiliuzwa na wenyewe kama ilivyouzwa UDA, ila hii ni mbaya zaidi ya UDA.
“Nikisema niyaseme yote hapa wabunge wenzangu mtatapika, wakati ule
yanatokea bungeni mimi nilikuwa Washington DC kwenye mkutano wa Benki ya
Dunia, niliomba nafasi kutoa utetezi wangu humu bungeni, lakini kwa
bahati mbaya sikupata hadi nilipoondoka Hazina,” alisema.
Mkulo alisema kuwa aliona ayaseme hayo jana kwani yeye ni Muislamu,
marehemu baba yake alikuwa sheikh na babu yake alikuwa chifu, na hivyo
anataka afe kwa heshima kwa kusema ukweli.