Stori: WAANDISHI WETU
HAKUNA neno
zuri la kusema zaidi ya Mungu mkubwa! Ule mtafaruku ndani ya ndoa ya
mwimba Injili mahiri Bongo, Flora na mumewe, Emmanuel Mbasha umedaiwa
kumalizika kwa wawili hao kupatana, Risasi Jumamosi linakuwa nambari
wani kukuhabarisha.
Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika, wawili hao walikalishwa kikao cha upatanishi mapema wiki hii kilichokuwa chini ya familia.
MANENO YA CHANZO
“Kikao
cha familia kilikaa, Mbasha aliitwa akafika, Flora naye aliitwa
akatokea, mazungumzo yalikuwa marefu lakini kimsingi waliamua kuweka
kando mtafaruku wao na kuijenga upya ndoa yao,” kilisema chanzo.
Chanzo
kiliongeza kuwa katika kikao hicho cha mwanzoni mwa wiki hii, miongoni
mwa adidu za rejea ilikuwa kutokumbushia vikao vilivyopita ambapo
hakukupatikana muafaka.
VIKAO VILIVYOPITA
Katika
vikao vilivyopita, wahusika wakuu walikuwa wazazi wa Mbasha (mzee Maneno
Mbasha, Zulfa Maneno), ndugu wa Flora na Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo
na Uzima, Josephat Gwajima.
VIKAO VYA BAADAYE
Kwa
mujibu wa chanzo, vikao vilivyofuata, wawili hao wakawa tayari kila
mmoja ametema nyongo yake pembeni na kufikia makubaliano kwamba, ndoa
yao isimame tena wakitumia maandiko kwenye Biblia kutoka kitabu cha
Waebrania yanayosema: Ndoa na iheshimiwe na watu wote na malazi yawe
safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu
WAKORINTHO YAFUNGA KAZI
Kwa
mujibu wa chanzo hicho, maneno mengine ya Biblia yaliyotumika kwenye
kikao hicho mpaka wawili hao wakaamua kurudiana ni 1 Wakorintho 7:1-10
ambapo maandiko yanasema:
Lakini
kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe na kila
mwanamke awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake vivyo
hivyo mke na ampe mumewe haki yake.
Flora Mbasha akiwa kwenye picha ya pamoja na mumewe, Emmanuel Mbasha.
Mke hana
amri juu ya mwili wake bali mumewe vivyo hivyo mume hana amri juu ya
mwili wake bali mkewe. Msinyimane, isipokuwa mmepatana kwa muda ili
mpate faragha kwa kusali, mkajiane tena shetani asije akawajaribu kwa
kutokuwa na kiasi kwenu.
Lakini
wale waliokwisha kuoana nawaagiza, wala hapo si mimi, ila Bwana (Mungu),
mke asiachane na mumewe, lakini ikiwa ameachana naye na akae asiolewe
au apatane na mumewe, tena mume asimwache mkewe.
KIKAO CHA JUMAMOSI KUMALIZIA
Chanzo
kilisema kuwa, kikao cha mwisho ambacho kitamalizia kuweka mambo sawa
ili wawili hao waanze ngwe ya pili ya ndoa yao ambayo inaaminika itakuwa
ya mwisho mpaka kifo kiwatenganishe, kinatarajiwa kufanyika leo jijini
Dar es Salaam mahali ambapo hapakutajwa.
MWANASHERIA ATAJWA
Mwanasheria
wa Flora aliyejulikana kwa jina moja la Ado ametajwa kusimamia kikao
hicho ili wawili hao waanze maisha mapya baada ya safari fupi ya
mvurugano uliowafanya kuwa mbalimbali.
AONGEA NA RISASI JUMAMOSI
Juzi,
Risasi Jumamosi lilimsaka mwanasheria huyo kwa njia ya simu yake ya
mkononi ili kumsikia anasemaje kuhusu kutajwa kwenye usuluhishi wa ndoa
hiyo ambapo alipopatikana alisema:
“Niko
Arusha, Ijumaa nitarudi Dar. Kuhusu kikao cha usuluhishi siwezi
kukwambia lakini suala la kuwapatanisha nalifahamu, nawaomba na ninyi
msaidie kufanikisha jambo hilo zuri.”
VIPI KUHUSU KESI YA MADAI YA KUBAKA?
Hata
hivyo, Wakili Ado hakutaka kugusia kuhusu kesi ya Mbasha iliyopo
Mahakama ya Wilaya ya Ilala ambapo anadaiwa kumbaka shemejiye mara mbili
(jina tunalo) ambayo kwa mujibu wa mahakama, upelelezi umekamilika na
itasikilizwa Julai 17, mwaka huu.
KWA UPANDE WAKE FLORA
Risasi Jumamosi lilimwendea hewani, Flora ili kumsikia anasemaje kuhusu kuwepo kwa upatanishi kati yake na mumewe, Emmanuel.
Huyu
hapa: “Ongea na wakili wangu atakwambia kila kitu.” Ambapo majibu ya
wakili yalikuwa: ”Ninachojua mimi ni kwamba Flora ameshamsamehe mumewe
na yuko tayari kuanza ukurasa mpya.”
MBASHA SASA
Kwa upande wake, Mbasha alipozungumza na gazeti hili juzi alisema kurejea upya kwa ndoa yake ni jambo la kuupendeza moyo wake.
“Mimi sina neno nipo tayari, nimeshasamehe yaliyotokea, Flora ni mke wangu jamani, nampenda sana kutoka moyoni.”CHANZO GPL