KAMA
ilivyotegemewa na kushauriwa na watu wengi, uongozi wa klabu ya Simba
chini ya rais Evans Aveva umemsainisha mkataba wa mwaka mmoja kocha mkuu
wa klabu hiyo, Mcroatia, Zdravko Logarusic.
Loga
amesaini mkataba huo leo makau makuu ya klabu ya Simba, mtaa wa
Msimbazi, Kariokoo jijini Dar es salaam na kueleza kuwa kikosi chake
kitakuwa bora msimu ujao, huku lengo kubwa likiwa ni kutwaa ubingwa.
Kitendo
cha kupewa kandarasi ya mwaka mmoja kimemfurahisa Logarusic na kuahidi
mambo mazuri kwa mashabiki na wanachama wa Simba katika mikikimikiki ya
ligi kuu msimuawa 2014/2015 unaotarajia kuanza septemba 20 mwaka huu.
Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange `Kaburu` ndiye aliongoza zoezi la kumsainisha Loga kandarasi hiyo.
Kaburu
alieleza kuwa uongozi umeamua kumpa majukumu kocha huyo na msalaba
uliopo mbele yake ni kuhakikisha Simba inarudisha heshima kwa kutwaa
ubingwa wa ligi kuu bara.
Kwa
upande wa kocha msaidizi, Suleiman Abdallah Matola `Veron`, Kaburu
alisema kocha huyo tayari alishasaini mkataba wa miaka miwili tangu
mwezi desema mwaka jana, hivyo hakuna mabadiliko.
Awali
kulikuwa na taarifa za uongozi wa Simba kumtimua Loga, lakini uongozi
umeamua kumbakisha kwa kueleza kuwa wameridhishwa na utendaji wa kazi
yake.
Kocha
huyo wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya alijiunga na Simba desemba mwaka
jana na mechi ya kwanza kuiongozo Simba ilikuwa ile ya Nani Mtani Jembe
ambapo alishinda mabao 3-2.
Hata
hivyo alipoanza kushiriki ligi kuu mzunguka wa pili baada ya kurithi
mikoba ya Abdallah Kibadeni, Loga alimaliza msimu kwa kushika nafasi ya
nne.
Mcroatia huyo anasifika kwa kuwa na msimamo mkali hasa suala la nidhamu kwa wachezaji.
Mara kadhaa wachezaji walidai kocha huyo ni mkali mno na kuna wakati anashindwa kuwatetea badala yake anawakalipia.
Lakini kwa tamadauni za wachezaji wa Tanzania, nidhamu ya mpira ni ndogo na kocha anayewasimamia sana anaonekana kuwa mbaya.