MHE. LOWASSA AANIKA UTAJIRI WAKE


Waziri Mkuu wa zamani na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akizungumza
wakati wa mahojiano na waandishi wa gazeti hili mjini Dodoma. Picha na
Edwin Mjwahuzi
**********
 
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema madai kwamba yeye
ni tajiri hayana ukweli wowote. Amesema yeye ni mfugaji na anamiliki
ng’ombe zaidi ya 800 katika Jimbo la Monduli, mkoani Arusha.


Lowassa alisema hayo katika mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake wiki iliyopita mjini Dodoma.
 “Haya madai hayana hata chembe ya ukweli hata
kidogo, isipokuwa mimi nadhani wananitakia mema kwa sababu ukiona jumba
zuri wanasema la Lowassa, gari nzuri la Lowassa, kitu chochote kizuri
wanasema cha Lowassa,” alisema na kuongeza:
“Wamesema uongo mwingi sana, mimi nasema tu
nilichopata nimepata na sina utajiri kiasi hicho, lakini si mbadhirifu
wa haki zangu ninazopata kama mshahara na haki nyingine.”
Alipotakiwa kutaja mali anazomiliki, Lowassa alisema: “Mimi ni mfugaji, nina ng’ombe zaidi ya 800 jimboni kwangu Monduli.”
Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli, alisema
madai kwamba anamiliki utajiri uliopindukia yalianza kabla hajajiuzulu
uwaziri mkuu na ilielezwa kuwa “maduka fulani” ni yake.
Alibainisha kuwa hata kampuni ya Alphatel ambayo
wanamiliki kwenye familia yake iliwahi kuhusishwa na jengo kubwa
lililojengwa na mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia wilayani Kinondoni, Dar
es Salaam likiitwa Alpha.
“Ikaonekana ni jengo langu, kule Mbezi kuna rafiki
yangu mmoja walienda watu wakasema hii nyumba ya Lowassa. Yule bwana
alitoka na bastola akawakimbiza. Mimi sina nyumba maeneo hayo,” alisema
Lowassa.
Bomu la ajira
Akitaja njia za kutegua ‘bomu la ajira’ kwa vijana
ambalo amekuwa akisema liko mbioni kupasuka, Lowassa alitaja maeneo
mawili ambayo yanapaswa kutazamwa ili kuzalisha ajira nyingi mpya.
Alitaja kilimo akisema kinachukua watu wengi
nchini. Alisema kinapaswa kutengenezewa mazingira ili vijana wanaomaliza
chuo kikuu wawe tayari kuishi kwenye mazingira ya kilimo.
Alitoa  mfano wa Misri kuwa mwanafunzi anapomaliza
chuo kikuu hupelekwa Mto Nile na hupewa ekari tatu za kulima mizabibu,
trekta na vyombo vingine na mkopo ambao huanza kuulipa baada ya miaka
mitatu.
 
“Tangu akiwa chuo (mwanafunzi) anajua ajira yake ni kilimo na
kwamba atapewa mazingira ya kufanya kilimo, si cha jembe la mkono ila
kilimo cha kisasa, anakopeshwa na anawezeshwa,” alisema.
Kwa hapa nchini, alisema Serikali ingefanya uamuzi
mgumu wa kutenga maeneo kama Kigoma, ichukue eneo la ekari milioni 10
ipandwe michikikichi (mawese) na kuwakabidhi vijana na baada ya miaka
minne watakuwa wamepata mawese kwa ajili ya chakula na kuuza nje.
Alitaja eneo jingine ni Serikali kuanzisha viwanda ili ajira ziendelee.
“Tunaweza na sisi tukajenga kwa makusudi viwanda
vya nguo ambavyo vinachukua ajira ya watu wengi au viwanda vingine
tutakavyoona vinafaa vinavyochukua ajira ya watu wengi. Naliweka suala
hili hadharani tulijadili,” alisema.
Lowassa, ambaye amekuwa akitajwa miongoni mwa
wanasiasa wanaotaka kuwania urais, alisema: “Kama mabepari wanaendeleza
sera za kijamaa kuokoa ajira zao na sisi tuendeleze sera hizo hizo
kuokoa ajira za watu wetu. Utaniambia Serikali itatoa wapi fedha, jibu
langu rahisi sana, tuna gesi. Mungu ametubariki.
“Tuna uhakika wa kupata trilioni 50 cubic metre.
Unaweza kukopa kutokana na gesi uliyonayo ardhini na tukifanya hivyo
tutakuwa tumetengeneza ajira nyingi za vijana.”
Alisema duniani kote vyama vya siasa vinapotaka
kuingia madarakani huangalia masilahi ya watu wake, jambo gani la msingi
ambalo chama kikiingia madarakani kitayafanya, likiwamo hili la ajira
ambalo lipo karibu katika kila nchi na kila chama kinachoingia
madarakani hulizungumzia.
“Labda niseme mfano mmoja, Mwalimu (Julius)
Nyerere alipokuwa anaanzisha elimu ya kujitegemea mwaka 1967 alikuwa
anaangalia ajira,” alisema.
Kwa nini analiita bomu? “Mimi sisemi tu ni bomu
ila nasema ni bomu linalotarajia kulipuka wakati wowote, lakini ni bomu
ambalo tunahitaji kulishughulikia. Lengo langu la kupiga kelele ni
kuitaka jamii ishughulikie jambo hili.”
Alieleza kufurahishwa na matokeo ya kelele zake za
ajira, kuwa ziliamsha wizara hadi kutoa takwimu na kila wizara
ikatakiwa kuangalia kwenye eneo lake inatengeneza ajira kiasi gani.
Afya yake je?
Yamekuwapo madai kuwa afya yake inatetereka na
kuwa alilazimika kwenda Ujerumani kutibiwa. Alipoulizwa alisema… “Hili
ni kama lile la utajiri.”
 
“Watu wanapenda kunitakia afya mbaya. Kwani wewe unaionaje?
Wanatunga tu naumwa, nikifanya mazoezi nikapungua kidogo wanasema huyu
amepata stroke (kiharusi) amepelekwa Ujerumani. Lakini nataka
nikuhakikishie kuwa afya yangu ni nzuri sana, namshukuru Mwenyezi Mungu
ambaye ananipigania afya njema.
Lakini kwa nini amekuwa akionekana kwa TB Joshua
Nigeria?… “Kila mtu ana uhuru wa kuamini na kushirikiana na imani
anayofikiri inafaa. Namuona TB Joshua kama muumini na mwombaji mzuri
ninayekubaliana naye katika vitu vingi, kwa hiyo nasikia faraja kwenda
kwa TB Joshua na ninataka kuwahimiza watu wanaotaka kwenda, waende, ni
mwombaji mzuri sana.”
 
MWANANCHI


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...