Karibuni tena Dodoma Waheshimiwa
Wajumbe wa Bunge Maalum la kutunga Katiba ya nchi yetu. Sote tuna kila
sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu wetu kwa kuendelea kutupa uhai na
afya hadi leo kutuwezesha kuwepo ndani ya ukumbi huu. Tupo humu ili
tuitekeleze kazi waliyotukabidhi Watanzania wenzetu milioni arobaini na
sita (46) ya kuwapatia Katiba mpya. Dhamana hii ni nzito na haistahili
kufanyiwa ajizi.
Tunaendelea na shughuli zetu za Bunge Maalum kwa kuzingatia Kanuni ya 30 (1) inayosema
“Akidi kwa kila kikao cha
Bunge Maalum isipokuwa wakati wa kupitisha uamuzi wa Bunge Maalum
itakuwa ni nusu ya Wajumbe wote wa Bunge Maalum“.
Nimetaarifiwa na Katibu kwamba
wajumbe waliokuja Dodoma kuhudhuria ni zaidi ya robo tatu ya Wajumbe
wote wa Bunge Maalum. Nawashukuruni nyote kwa kuja hapa Dodoma ili
kutimiza wajibu wenu.
Kwa niaba yenu, nawashukuru
Watanzania wenzetu wote ambao kwa mamilioni wamedhihirisha utashi mwema
wa kisiasa kwa kuunga mkono hatua ya Bunge Maalum kuendelea na kazi zake
hadi tuipate Katiba inayopendekezwa ambayo wataipigia kura ya maoni.
Kipekee na kwa niaba yenu, nawashukuru kwa dhati viongozi wetu wa dini
wa madhehebu yote wanaloliombea Taifa hili mafanikio Bunge Maalum,
wakitanguliza utaifa pamoja na amani ya nchi na umoja ndani ya nchi na
siyo ubinafsi na maslahi ya makundi.
Kwa leo sikupenda sana
kuzungumzia hoja mbali mbali zinazotawala magumzo ya mchakato wa Katiba
mpya hapa nchini, magumzo yanayoendeshwa na makundi maalum kwa jazba na
hata matusi. Hata hivyo nalazimika kutoa maelezo ya ufafanuzi kuhusu
upotoshaji mkubwa unaoendeshwa na baadhi ya watu kuhusu Bunge Maalum.
Nikiwa Mwenyekiti wenu ninao wajibu wa kuwafafanulia wananchi kuhusu
uhalali wa shughuli za Bunge Maalum linaloendelea na utaratibu wa
shughuli zetu.
Ni Rasimu ya Tume au la
Wapo wanaodai kuwa eti hapa
Bungeni hatujadili Rasimu ya Tume. Tuhuma hii haina ukweli hata kidogo.
Msingi wa majadiliano yote tangu tumeanza ni Rasimu ya Katiba
iliyowasilishwa na Tume ya Katiba. Utaratibu ni kwamba pale ambapo
wajumbe wanaona panafaa kurekebishwa wanafanya hivyo. Maana ya rasimu ni
andiko ambalo halijajitosheleza bila kupata ithibati ya taasisi ya juu
zaidi. Anayekabidhiwa rasimu anayo haki na mamlaka ya kuirekebisha.
Vinginevyo kujadili rasimu hakuna sababu. Itakuwa ni jambo la ajabu na
lisilo na mantiki yoyote kuwa taasisi iliyopewa mamlaka ya kujadili
Rasimu ikishaijadili iiache ibaki kama ilivyokuwa wakati
ilipowasilishwa!
Je suala ni muundo wa Muungano tu?
Maudhui ya Rasimu yanajumuisha baadhi ya masuala muhimu yafuatayo:
- Kuimarisha Muungano wetu kwa kuleta uwiano bora zaidi wa mamlaka ya Zanzibar na Tanzania Bara ndani ya Muungano
- Kuimarisha haki za binadamu ili kuwawezesha raia wa kawaida kufaidi uhuru wa demokrasia bila ubabe na dhuluma
- Kuzuia wachache kufuja rasilimali za taifa bila kujali maslahi ya wengi na ya vizazi vijavyo.
- Kujenga uwiano sahihi na wenye haki baina ya wanawake na wanaume katika nafasi za uongozi.
- Kubainisha hatua zenye
kuleta matumaini mapya ya maendeleo kwa makundi maalum ya vijana
wakulima wadogo, wafugaji, wafanyakazi wa ngazi za kawaida, walemavu,
wafanya biashara wadogo na wajasiriamali wengine.
- Kuweka msingi imara wa
kutungwa kwa sheria kakamavu za kuzuia ukandamizaji wa raia,
unyonyaji, wizi wa mali ya umma, rushwa, hujuma dhidi ya uchumi na
kuzuia mapato haramu na fedha chafu.
- Kutambua haki za ardhi kwa wakulima, wafugaji na wajasiriamali wengine ili kupunguza migongano na migogoro.
- Kuweka Misingi ya utawala bora inayozingatia uadilifu, sifa stahiki na ufanisi.
- Kuwezesha kutungwa kwa
sheria bora zaidi zitakazosimamia chaguzi zilizo za haki na huru
zaidi pamoja na kuwepo Tume za Uchaguzi zilizoboreshwa.
Zaidi ya hivyo, yapo mapungufu
katika Rasimu iliyopo kwa kuachwa masuala ya kuwezesha Serikali za
mitaa; kutoa maelekezo kuhusu masuala ya matumizi ya ardhi na rasilimali
nyingine za Taifa. Nini kinatuzuia kuiboresha Rasimu kwa kuyaongeza
mambo haya ndani ya Katiba kwa faida ya Taifa?
Yote haya ni masuala muhimu
ambayo yamo ndani ya rasimu na wakati wake wa kuyaweka sawa ndiyo huu.
Pamoja na umuhimu wake suala la muundo wa Muungano si suala la
kutulazimisha tuyaahirishe mazuri yote yaliyomo katika Rasimu
tuliyopewa.
Uhalali wa Shughuli za Bunge Maalum
Pamoja na uhalali wa kisheria wa
Bunge hili Maalum kuendelea kufanya kazi zake, linao pia uhalali wa
kisiasa kutokana na sifa za uwakilishi wetu na pia maudhui yaliyomo
ndani ya Rasimu. Kutofautiana maoni hakuwapi hadhi tofauti baadhi ya
wajumbe kujiona wao wana uhalali zaidi mbele ya wananchi kuliko wenzao.
Ndiyo maana utaratibu umewekwa wa kupiga kura na wa maridhiano.
Utamaduni mpya unaoanza kujengwa na baadhi ya viongozi wa jamii wa
kususia mijadala halali na kwenda nje kuelezea hoja za upande mmoja
hauna nafasi katika Tanzania jamii isiyotaka fujo na utengano.
Wajumbe wa Bunge Maalum
wanaoendelea na kazi mjini Dodoma ni wateule wa Rais kwa niaba ya
wananchi kwa kazi ya kutunga Katiba. Kazi hii haiwezi kusitishwa kwa
sababu tu wajumbe wachache wameisusia. Tutazingatia matakwa ya sheria
katika kufikia hatma ya mchakato wa Katiba.
Mabadiliko ya Kanuni
Kama nilivyoeleza hapo mwanzo,
Rasimu ina jumla ya sura kumi na saba (17) zenye mambo mengi yenye
maslahi kwa Watanzania wote. Kwa muda tuliopewa wa siku sitini (60)
isingewezekana kuikamilisha kazi tuliyopewa ndani ya muda. Ikumbukwe
kwamba kwa Kanuni zilivyo, kila sura mbili zinahitaji siku tisa
kuzifanyia kazi. Kwa njia hiyo, ingetuchukua siku takriban mia moja
thelathini (130) ili kuikamilisha kazi hii! Pendekezo la msingi hapa ni
kwamba Kamati zetu kumi na mbili (12) zizingatie na kuzijadili sura kumi
na tano (15) za Rasimu na pia zikamilishe uandishi wa sura mbili
zilizojadiliwa awali na ikibidi ziongeze sura ambazo zitadhihirika kuwa
ni muhimu. Naamini mtiririko huu utatuwezesha kuwa na mpangilio bora
zaidi wa sura na ibara katika Katiba mpya. Tusingependa na wala
isingefaa kuomba tena muda wa ziada wa kazi ya Katiba ndio maana
tunafanya mabadiliko ya Kanuni. Kamati ya Uongozi iliyoketi Dar es
Salaam tarehe 28 Julai 2014 imependekeza yafanywe mabadiliko ya Kanuni
za Bunge Maalum kuwezesha kazi ikamilike ndani ya muda tuliopewa. Kwa
hiyo nitawaomba tuyatafakari mapendekezo ya mabadiliko ya Kanuni na
hatimaye kuyapitisha ili ratiba ya kazi zetu iende sawa. Nitawaomba
muikubali ratiba iliyogawanywa leo na pia mkubali kuzibadilisha Kanuni
kwa lengo nililolieleza hapa.
HITIMISHO
Pamoja na maoni ya kila namna
yanayoendelezwa kujadili mchakato wa Katiba nje ya Bunge hili, ni muhimu
wahusika wapunguze jazba, chuki na upotoshaji. Bunge Maalum lisaidiwe
kwa mawazo chanya ili limalize kazi yake.
Sisi tuliomo humu katika Bunge
Maalum tuna wajibu wa kuifanya kazi yetu kwa umakini na kwa uadilifu ili
kazi yetu iwe bora. Tujadiliane kwa uungwana. Tofauti za mawazo
zisitufanye tuingize chuki na maneno yasiyofaa. Katika mabadiliko ya
Kanuni nashukuru sasa Kiti kimepewa mamlaka ya kushughulikia utovu wa
nidhamu ndani ya wakati. Lakini ninaamini haitakuwa lazima kwangu mimi
au Makamu Mwenyekiti kutumia nguvu za mamlaka yetu ila tu pale
itakapobidi.
Nawatakia nyote Mkutano wenye mafanikio kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
MUNGU IBARIKI TANZANIA!
Samuel Sitta – MB
MWENYEKITI BUNGE MAALUM LA KATIBA