“Nilikuwa
nimelala ndani, nilipoamka asubuhi nilikuta mlango umefungwa kwa nje
hata hivyo nilivumilia hadi njaa ilipoanza kuniuma baada ya siku tano
nikaanza kupiga kelele ndipo majirani walipokuja kunifungulia na
kuniambia nyumba imeuzwa” alisema mtoto Erasto Emmanuel pichani juu.
Nyumba iliyouzwa mtoto akiwa ndani.
Mtoto
Groly Emmanuel (9) ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Hatwelo
alisema aliagwa na baba yake ambaye alimwachia shilingi 3,000 lakini
hakumwambia kama nyumba imeuzwa.
Barua ya makubaliano ya kuuziana kiwanja chenye nyumba ndani yake.
Mwanaharakati
wa Haki za Binadamu, Yasin Yuta, alisema majirani waligundua baada ya
kusikia kelele za mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la Erasto Emmanuel
(11) aliyekuwa amefungiwa ndani na kukaa kwa siku tano.
VITENDO vya ukatili dhidi ya watoto
vimeendelea kushika kasi katika baadhi ya maeneo hususani vijijini,
licha ya Serikali na asasi mbalimbali kulipigia kelele ambapo hivi
karibuni Baba mmoja aliamua kuuza nyumba ikiwa na watoto ndani na
kutokomea kusikojulikana na kuwaacha wasijue la kufanya.
Mkasa huo wa ajabu ulitokea katika kijiji
cha Hatwelo, Kata ya Ijombe Mbeya Vijijini ambapo Mkazi huyo
aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Yuta alipouza nyumba yake na
kutokomea yeye na mkewe na kuwaacha watoto wawili wenye umri kati ya
miaka 9 na 11 wakikosa mahala pa kuishi.
Akizungumzia sakata hilo kijijini hapo,
Mwanaharakati wa haki za Binadamu, Yasin Yuta, alisema majirani
waligundua baada ya kusikia kelele za mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina
la Erasto Emmanuel (11) aliyekuwa amefungiwa ndani na kukaa kwa siku
tano.
Alisema baada ya kumfungulia mtoto huyo
ndipo ilipobainika kuwa nyumba hiyo ilikuwa imeshauzwa huku mtoto akiwa
ndani na ndipo mnunuzi alipofunga na kufuli bila kujua kama kuna mtoto
ndani huku watoto wengine wakiwa kwa ndugu zao ambao pia hawakuelezwa
kama nyumba imeuzwa.
Nyumba hiyo iliuzwa kwa Dati Nsagaje kwa
gharama ya shilingi 750,000/= ikiwa ni nyumba mbili pamoja na kiwanja
ambapo mnunuzi huyo alilipa kianzio cha shilingi laki nne biashara
iliyofanyika tangu April 26 mwaka huu na kiasi kilichobaki wakiwa
wameahidiana kulipana Mwezi Mei 15, Mwaka huu.
Wahanga wa tukio hilo ambao ni watoto
walisema hawakuwa na taarifa zozote za kuuzwa kwa nyumba wanayokaa
ambapo walisikia kuwa baba yao ameenda Sumbawanga kumfuata mke wake
ambaye inasemekana aliolewa na mwanaume mwingine.
“Nilikuwa nimelala ndani ambapo nilipoamka
asubuhi nilikuta mlango umefungwa kwa nje hata hivyo nilivumilia hadi
njaa ilipoanza kuniuma baada ya siku tano nikaanza kupiga kelele
ndipomajirani walipokuja kunifungulia na kuniambia nyumba imeuzwa”
alisema mtoto Erasto Emmanuel.
Mtoto mwingine aliyetelekezwa ambaye siku
ya tukio alikuwa ameenda kulala kwa bibi yake Groli Emmanuel (9) ambaye
ni mwanafunzi wa shule ya msingi Hatwelo alisema siku akiwa anaondoka
aliagwa na baba yake ambaye alimwachia shilingi 3000 lakini hakumwambia
kama nyumba imeuzwa.
Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida
na kuonesha kukosa uwajibikaji kwa baadhi ya viongozi wa Serikali ya
Kijiji ambao walishiriki moja kwa moja zoezi hilo huku wakiwa wamesaini
kama mashahidi na kugonga mhuri wa Serikali ya Kijiji walipoulizwa
kuhusiana na sakata hilo hawakuwa na majibu ya kuridhisha.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Hatwelo, Ibrahimu
Mponzi, alisema kitendo alichokifanya muuzaji ni cha kawaida kwa sababu
ameuza mali yake mwenyewe na kwamba wao kama majirani na serikali ya
kijiji hawawezi kuhoji atakako waacha watoto kwa sababu ni mipangilio ya
maisha ya kila mtu.
Mbali na mwenyekiti wa Kijiji kuwa shahidi
wa upande wa mnunuaji akiwa sambamba na watu wengine wanne akiwepo Mkewe
ambaye pia ni Balozi wa nyumba kumi pia waliosaini wengine ni ndugu wa
mnunuaji ili hali muuzaji akiwa hana shahidi hata mmoja.
Na Mbeya Yetu