Dar es Salaam. Umoja wa Ulaya (EU), umelaani vikali kufungiwa kwa magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kwa madai ya kuandika habari zenye taswira ya uchochezi.
Taarifa ya kulaani uamuzi huo, ilitolewa leo jijini Dar es Salaam na msemaji wa Umoja huo, Tom Vens. Taarifa hiyo pia iliungwa mkono na mabalozi wa Canada, Norway na Uswisi.
Serikali iliidhinisha kufungiwa kwa magazeti hayo Septemba 27 mwaka huu, huku Mwananchi likifungiwa kwa siku 14 na Mtanzania siku 90.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, mbali na kushtushwa kufungiwa kwa magazeti hayo, pia EU imeshangazwa na uamuzi wa Serikali kuzuia habari kuwekwa katika mtandao wa gazeti la Mwananchi, pamoja na kuzuia Gazeti la Rai kutoa habari zake kila siku.
“Ni wajibu wa vyombo vya habari kutekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria na kujitahidi kufuata maadili,” inaeleza taarifa hiyo na kuongeza;
“Uhuru wa Habari na uhuru wa kujieleza ni haki ya msingi kwa watu na utekelezaji wake unahitaji uangalifu na uwiano sawa katika matumizi ya sheria zinazoongoza vyombo vya habari,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa inaeleza kuwa, haki ya kisasa ya sheria ya habari na vyombo vya habari inatakiwa kuboreshwa ili kuwa na uwazi zaidi.
“Ikumbukwe, Oktoba 2010, mapendekezo ya EU kuhusu chaguzi huru yalieleza kuwepo na sheria za vyombo vya habari zinazoendana na wakati wa sasa, kwa kuzingatia maoni ya wadau. Pia ilipendekeza utaratibu bora wa kutatua migogoro na malalamiko,” ilieleza taarifa hiyo.
Inaeleza kuwa ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania unazidishwa na dhamira ya pamoja ya uhuru wa kimsingi, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza na habari.
“Vyombo vya habari vina jukumu muhimu la kuuhabarisha umma kama njia mojawapo ya kukuza maadili na haki za binadamu. Jukumu la vyombo vya habari pia ni kuendelea kuimarisha mchakato wa demokrasia,” inaeleza.
EU unatoa wito juu ya mamlaka kufanya jitihada za kulinda uhuru wa kujieleza na kukuza haki ya kupata habari.