WAKATI mshindi wa jumla wa tuzo ya Mchezaji
Bora wa Mwaka 2011 wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania
(Taswa) Shomari Kapombe akizaliwa mwaka 1994, katika kijiji cha Kishozi,
Kagera alizaliwa mtoto wa kike ambaye hakudhaniwa iwapo siku moja
angefika mbali kimtazamo, kiakili, kifikra na katika masuala ya
ulimbwende.
Mtoto huyu alipewa jina la Biera lenye uhalisia wa
kabila la Wahaya na baba yake ambaye alifariki baada ya yeye kutimiza
umri wa mwaka mmoja. Alianza kulelewa na mama yake Amina Bukoko katika
mji wa Tabora wakati huo mama yake akiwa na umri wa miaka 21 tu.
Huyu ni Happiness Watimanywa aliyetawazwa kuwa Miss Tanzania Septemba 21, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 19.
Mwanaspoti lilimtafuta mrembo huyu na kufanya mahojiano naye kama ifuatavyo...
Mwanaspoti lilimtafuta mrembo huyu na kufanya mahojiano naye kama ifuatavyo...
Mwanaspoti: Wewe ni msomi na mrembo, unadhani urembo hasa ni nini?
Happiness: Kama unataka kuwa
mrembo si lazima uvutie tu machoni mwa watu, kuna vitu vingi. Kwanza
unapaswa kuwa mrembo wa umbo na sura hata hivyo uwe na vigezo vyote kwa
kuitwa mrembo. Pili ni tabia, unapaswa kuwa mrembo wa roho na nafsi
(inner beauty) huwezi kuwa mrembo kisha ukafanya vitu vilivyo tofauti na
urembo wako. Pia vilevile uweze kutambua udhaifu ulionao na
kuurekebisha.
Mwanaspoti: Ni makosa gani ambayo
unahisi yalifanywa na warembo waliowahi kutwaa taji la Miss Tanzania na
umejipanga vipi kuyarekebisha na matarajio yako ni nini katika
kuibadili sekta ya urembo nchini?
Happiness: Sidhani kama kuna
makosa yaliyofanywa na warembo waliopita, ila kuna baadhi ya vitu
ambavyo Watanzania wanasahau kwamba mrembo naye ni binadamu. Kuna vitu
atavifanya ambavyo huenda vinaweza kuonekana kuwa na utofauti, ni kama
binadamu wa aina nyingine. Lakini kikubwa ni kutekeleza masuala ya
kijamii na yeye mwenyewe anavyoishi katika jamii. Kujijengea uwezo wa
kufikiri ni nini utaifanyia jamii, si kuishia kuvaa taji ila ni zaidi ya
ulimbwende.
Mwanaspoti: Umewahi kutembelea vivutio mbalimbali hapa nchini na je umejipanga vipi katika kuhamasisha utalii wa ndani?
Happiness: Nina mipango mingi na
mizuri kuhusu hilo. Kwanza mimi nimekuwa mtalii mzuri na nilianza utalii
wa ndani nikiwa mdogo kabla sijaingia katika masuala ya ulimbwende.
Nimewahi kutembelea Mikumi, Serengeti, Manyara na nimewahi kufika katika
kilele cha Mlima Kilimanjaro. Nilikwea mlima huo mwaka 2011 na
kufanikiwa kufika katika kilele cha Uhuru, nikiwa huko nilishuhudia
mambo mengi sana na nilipata uzoefu mkubwa. Nimewahi kushuhudia mengi na
Tanzania imebarikiwa vitu vingi. Nimeshawahi kuona simba anapanda mti
nadhani ni uzoefu tosha, nimepanga kuhamasisha utalii wa ndani na
kukaribisha wageni kutembelea nchi yetu.
Mwanaspoti: Ukiwa Miss Tanzania
2013, pia ulililetea sifa taifa kwa kuongoza katika somo la Uhasibu kati
ya nchi 150, hebu tuambie ilikuwaje na vipi bado unaendelea na somo
hilo?
Happiness: Nilikuwa nikilipenda
somo la Uhasibu tangu nikiwa kidato cha kwanza licha ya kufanya vizuri
katika somo la hisabati tangu shule ya msingi. Kwanza tulikuwa na
mitihani ya IGCSE; mitihani hii tuliifanya kawaida sana ila kwa kuwa
nilikuwa mdadisi sana hasa nisipomwelewa mwalimu wangu ilinisaidia
kuweza kufanya vizuri. Hata hivyo alama zangu darasani zilikuwa ni
kuanzia 90 mpaka 100 sikushuka chini ya hapo.
Nakumbuka niliitwa katika shule niliyokuwa
nikisoma St Costantine International School, Arusha wakati wa mahafali
ya kidato cha nne na kupewa habari hiyo njema, nilifurahi sana. Mtihani
niliufanya mwaka 2009 na majibu nilipewa 2010. Lakini kidato cha tano na
sita nilisoma masomo yaliyo nje ya mchepuo yaani Jiografia, Historia na
Uhasibu, sikuhitaji masomo ya mchepuo