Mtoto wa mwandishi na mtangazaji wa kituo cha ITV,Ufoo Saro,Alvis
Anthery akitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza la marehemu Bibi yake
Anastazia Saro aliyezuikwa jana katika makaburi ya kanisa la Urara
wilayani Hai.
Umati wa waombolezaji waliojitikeza katika kuaga mwili wa marehemu
Anastazia Saro aliyezikwa katika makaburi ya kanisa la Urara wilayani
Hai.
Msemaji wa familia ya Saro,Allelio Swai akitoa maelezo ya familia
wakati wa ibada ya kumuombea marehemu Anastazia Saro.
Jeneza lililobeba mwili wa marehemu Anastazia Saro likiwekwa kaburini.
Mkuu wa jimbo la Hai,Aminirabi Swai akiongoza ibada ya maziko katika
makaburi ya kanisa hilo na kisha kuweka shada la maua katika kaburi la
marehemu Anastazia Saro.
mwakilishi wa serikali katika maziko ya marehemu Anastazia Saro ,mkuu
wa wilaya ya Hai Novatus Makunga akiweka shada la Maua katika kaburi.
Mtoto Alvis Anthery akiweka shada la maua katika kaburi la Bibi yake
marehemu Anastazia Saro.(picha na Dixon Busagaga)
Na Dixon Busagaga waglobu ya jamii Moshi
VILIO,simanzi na hali ya huzuni jana vimetawala kwa mamia ya wakazi wa
kijiji cha Shari, Machame wilayani Hai waliojitokeza kuuaga mwili wa
marehemu ,Anastazia Saro (56),mama mzazi wa Mwanadishi na Mtangazaji
wa Kituo cha Televisheni cha ITV,Ufoo Saro.
Wakazi hao wakiwemo wale waliotoka maeneo mbalimbali ya miji ya
Moshi,Arusha na Dar es Salaam baadhi yao walionekana wakiangua vilio
huku wengine wakipoteza fahamu muda mfupi baada ya jeneza lililobeba
mwili wa marehemu kuingizwa kanisani.
Hali ilikuwa ya Simanzi zaidi wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa
waombolezaji wakipita mbele ya jeneza ambapo ililazimika kuwepo na
watu maalumu ambao walikuwa na jukumu la kutoa huduma ya kwanza kwa
baadhi ya ndugu walioshindwa kujuzuia.
Hali kama hiyo ili rejea kwa mara nyingine tena pale msemaji wa
familia Allelio Swai akitoa maelezo ya namna marehemu alivyo uawa na
hali aliyokutwa nayo mara baada ya kufanyiwa uchunguzi na madaktari.
Akitoa maelezo ya wasifu wa marehemu aliyefanyiwa ibada ya mazishi
katika Kanisa la Urara lililopo chini ya Jimbo la Hai la Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),Swai alisema marehemu Anastazia
Saro alifikwa na mauti hayo baada ya
kupigwa risasi na mkwewe Anthery Mushi ambaye alikwenda nyumbani kwa
mama huyo eneo la Kibamba CCM,nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Alisema taarifa ya madaktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
(MNH), inaonyesha,Anastazia Saro alifariki dunia baada ya kushambuliwa
kwa risasi tano katika mwili wake.
Swai aliomba kufanyika maombi kwa ajili ya Ufoo aliyelazwa katika
hosptali ya Muhimbili ambako anapatiwa matibabu baada ya kufanyiwa
upasuaji mkubwa hali iliyolazimu madaktari kumpa muda mrefu wa
mapumziko.
“ Ufoo taarifa ya madaktari inaonesha alichanika utumbo mkubwa na
kiasi utumbo mdogo,lakini tunashukuru hali ya Ufoo inaendelea
kuimarika ,lakini maombi yenu yanahitajika ili aweze kurejea katika
hali yake ya zamani ,na aweze kulitumikia taifa kwa kuhabarisha
“alisema Swai.
Kwa upande wake,baba mdogo wa Ufoo Saro, mzee Eshikaeli Saro,
akizungumza katika ibada ya mazishi kanisani hapo,alisema familia na
kanisa imepoteza mtu aliyekuwa kiungo muhimu kati ya jamii na kanisa.
“Mama alikuwa ndiye mpambaji wa madhabahu ya kanisa ,na alihakikisha
kanisa linakuwa katika hali ya usafi kabla ya ibada na hata pale
wanakwaya walipokuwa na mazoezi ya kutwa hapa kanisani alihakikisha
wanapata chakula”alisema Saro.
Alitoa shukrani kwa Mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Dk.Regnald
Mengi,mkurugenzi mtendaji wa ITV na Redio One, Joyce Mhavile pamoja na
wafanyakazi wote wa makampuni hayo kwa kuifanya familia hiyo iweze
kumfikisha marehemu Machame na kuzikwa.
Marehemu Anastazia Saro, aliuawa baada ya mkwewe kufika nyumbani kwake
Kibamba CCM akiwa na mzazi mwenzie Ufoo kwa lengo la kusuluhishwa kile
kinachodaiwa ni ugomvi uliokuwa ukifukuta kati ya wawili hao.
Tukio hilo lilitokea alfajiri ya Jumapili ya Oktoba 13 mwaka huu,
huku mwanae Ufoo Saro ambaye ni Mwandishi na Mtangazaji wa ITV,
akijeruhiwa vibaya kwa risasi mbili baada ya kutokea ugomvi kati
yakena mzazi mwenzie Anthery Mushi ambaye hata hivyo na yeye alijiua
kwa kujipiga risasi baada ya tukio hilo.
Picha zote kwa hisani ya Michuzi Blog