SISTER DU ANASWA TENA KWA KOSA LA KUJIUZA, NI BAADA YA KUPEWA MSAMAHA MAALUMU


BAADA Mei mwaka huu kuhukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani kwa kosa la kufanya ukahaba, mkazi wa jijini Dar, Blandina Barton amekamatwa tena kwa kosa hilohilo ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya kumaliza kifungo chake,..

Habari za uhakika zilizopatikana katika Mahakama ya Jiji, Dar es Salaam zinasema kwamba mfungwa huyo alitumikia kifungo chake katika Gereza la Segerea jijini Dar na alipobakiza miezi michache kumaliza alionewa huruma na bibi jela na kutakiwa kumalizia kifungo hicho uraiani.

Inadaiwa kuwa kabla ya kuachiwa, bibi jela alimsihi Blandina kuhakikisha harudii kosa lililompeleka gerezani pindi atakapokuwa akimalizia kifungo chake nje ya gereza.

Blandina akamhakikishia bibi huyo kwamba atakuwa mtu safi kwani amejifunza vya kutosha.

Katika hali ya kushangaza, Jumatano iliyopita Blandina alipandishwa tena katika Mahakama ya Jiji iliyopo Barabara ya Sokoine jijini Dar akiwa amerudia kosa lililompeleka Segerea miezi michache iliyopita.


Imeelezwa mahakamani hapo kwamba, Septemba 24, mwaka huu Blandina na wenzake wanne walinaswa Buguruni usiku wakiwa katika mawindo ya ukahaba.

Bahati mbaya kwa Blandina alipofikishwa mahakamani hapo alikutana na hakimu yuleyule aliyemhukumu kifungo cha miezi sita kwa kosa la ukahaba.


Hakimu huyo, Timothy Lyon alipigwa na butwaa baada ya kumuona Blandina akiwa amesimama mbele yake.


Mtuhumiwa huyo aliyekuwa na wenzake, Husna Amos, Monica Denis, Esther Chizai na Angela Emmanuel wote kwa pamoja walisomewa mashtaka yao na kukana.

 Hakimu Lyon aliwaambia watuhumiwa hao kwamba dhamana iko wazi na kuwataka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili na shilingi laki mbili.

Sharti hilo lilionekana kuwa gumu kwa watuhumiwa wote, hivyo walipandishwa karandinga na kupelekwa Gereza la Segerea mpaka Oktoba 15, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena mahakamani hapo


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...