Rais Jakaya Kikwete, leo jioni atalihutubia taifa kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akitarajiwa kuzungumzia mambo makubwa manne.
Spika wa Bunge, Anne Makinda aliwaambia wabunge jana asubuhi kuwa Rais Kikwete atalihutubia Bunge kuanzia saa 10.00 jioni na kwamba atafanya hivyo kwa mujibu wa Kanuni ya 30 (1) ambayo inasema: "Rais anaweza kulihutubia Bunge siku yoyote ambayo Bunge linakutana na wakati mwingine wowote kwa mujibu wa Ibara ya 91 ya Katiba."
Hotuba ya Rais Kikwete inatarajiwa kutoa majibu kwa masuala kadhaa kuhusu msimamo na mwelekeo wa taifa yakiwamo mchakato wa Katiba Mpya, hususan marekebisho ya Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2013 ambayo ilipitishwa mkutano uliopita.
Kamati ya Uongozi ya Bunge iliyokutana jana mchana chini ya Spika Makinda, iliridhia muswada huo kuingizwa katika ratiba ya sasa kutokana na kuwasilishwa chini ya hati ya dharura iliyosainiwa na Rais Kikwete, Oktoba 28 mwaka huu.
Kanuni ya 80 (4) ya Kanuni za Bunge
inasema: "Muswada wowote wa Sheria wa Serikali wa dharura hautaingizwa
kwenye shughuli za Bunge bila ya kuwa na hati iliyowekwa saini na Rais
inayoeleza kuwa muswada uliotajwa katika hati hiyo ni wa dharura."
Katika fasili ya 5 na 6 ya Kanuni,
Kamati ya Uongozi ndiyo yenye dhamana ya kuidhinisha muswada wa dharura
na sasa mapendekezo ya Serikali yatapita katika hatua zote tatu za
kusomwa, kujadiliwa kisha kupitishwa kuwa sheria.
Matarajio ya wasomi
Mbali na mchakato wa Katiba Mpya,
baadhi ya wasomi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliohojiwa jana
walisema kwamba Rais Kikwete hawezi kukwepa kuzungumzia mgogoro
unaofukuta ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Wengine wamesema huenda akazungumzia
mambo muhimu kama Operesheni Tokomeza Majangili ambayo siku chache
zilizopita ilizua tafrani bungeni kiasi cha kuanzishwa uchunguzi wa
jinsi ilivyoendeshwa, Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na ushiriki
wa Tanzania katika vita ya kuwaondoa Waasisi wa Kundi la M23 katika
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Gaudence Mpangala alisema kwamba Rais Kikwete anaweza
kuzungumzia Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na mgogoro wa EAC hususan
kutengwa kwa Tanzania na nchi za Uganda, Kenya na Rwanda.
"Hii Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
bado ina utata hata kama Rais aliisaini. Tunakumbuka muswada
ulipopelekwa bungeni ni wabunge wachache tu wa upinzani walioijadili,
lakini wengi walitoka nje na ilizua vurugu kwa vyama vya siasa na asasi
za kiraia."
Aliongeza, "Inawezekana CCM wakagoma
kuijadili wakasema tulishapitisha na kama Rais akiwalazimisha, Bunge
linaweza kuvunjika na kuitishwa tena uchaguzi. Ndiyo maana Rais
analazimika kuhutubia Bunge ili kuweka mambo sawa."
Kauli yake iliungwa mkono na mchambuzi
wa masuala ya siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Emmanuel
Mallya ambaye alisema Rais anaweza kuzungumzia msimamo wa Tanzania kwa
kuzingatia kuwa ni muda mrefu sasa Rwanda, Kenya na Uganda zimekuwa
zikiitenga kwenye mikutano. Alisema Rais pia anaweza kuzungumzia tatizo
la elimu nchini pamoja na mabadiliko ya madaraja ya ufaulu.
Mallya alisema suala la dawa za
kulevya pia linaweza kuzungumzwa na Rais Kikwete hasa ikizingatia kwamba
katika siku za karibuni biashara hiyo imeshamiri na kuharibu sifa ya
nchi.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha
Sayansi ya Tiba Muhimbili, Dk Yahya Kishashu alisema angependa Rais
azungumzie mchakato wa Katiba Mpya katika hotuba yake, hivyo kutegua
kitendawili cha wengi kuhusu mchakato huo.
"Kulikuwa na ushabiki katika Mabaraza
ya Katiba, utakuta wajumbe wanashambuliana kwa maneno na kutukanana
jambo ambalo lisipofanyiwa kazi tunaweza tusifikie malengo," alisema Dk
Kishashu.
Alisema Rais anaweza kutumia nafasi ya
leo kuweka wazi uendeshaji wa mchakato huo ili kuepusha uwezekano wa
maoni ya watu wacheche kupewa nafasi na maoni ya wengi yakapuuzwa.
Hotuba nne za JK bungeni
Hii itakuwa ni mara ya tano kwa Rais Kikwete kuhutubia Bunge tangu alipochaguliwa kuwa Rais, Oktoba, 2005.
Mara ya kwanza ilikuwa Desemba 30,
2005, ikifuatiwa na ile ya Julai 21, 2008 kisha Julai 16, 2010 na hotuba
yake ya mwisho ilikuwa Novemba 18, 2010.
Desemba 30, 2005
Katika hotuba yake ya kwanza Rais
Kikwete aliahidi kuwatumikia Watanzania na kutekeleza ilani ya CCM huku
akiviahidi vyama vya upinzani kwamba Serikali yake itaendeleza mfumo wa
siasa wa demokrasia ya vyama vingi.
Aliwataka Watanzania kuwa na maadili
yatakayotawala shughuli za kisiasa, ambayo hayategemei hiari ya viongozi
wa kisiasa waliopo madarakani na kukemea rushwa katika uchaguzi.
Julai 21, 2008
Hotuba yake ya pili ya mwaka 2008
aliliambia Bunge kwamba Serikali imekamata mali zote za wamiliki wa
kampuni 13 kati ya 22 zilizothibitika kuhusika na uchotaji wa mabilioni
ya shilingi kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Alisema licha ya kuzuiwa hata kwa
magari wanayomiliki watu hao, pasi zao za kusafiria pia zinashikiliwa
ili wasikimbie nje ya nchi.
Aidha, alisema kuwa ameiagiza Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), kufunga akaunti hiyo ambayo alieleza kuwa ilikuwa
na zaidi ya Sh130 bilioni na kuagiza fedha hizo ziwekwe katika Mfuko
Mkuu wa Serikali na zitumike kuongeza ruzuku ya mbolea na dawa za
mifugo.
Baada ya hotuba yake hiyo, Spika wa
Bunge wakati huo, Samuel Sitta alimkumbusha kuwa wahujumu uchumi
hawastahili kuneemeka kwa madai ya haki za binadamu na huku akionekana
kutofurahia Rais kuwaongezea muda watu hao kurejesha fedha hizo.
Julai 16, 2010
Katika hotuba yake ya tatu wakati
akilivunja Bunge la 10 alirudia ahadi alizozitoa mwaka 2005 bungeni
kuhusu amani, utulivu na umoja wa kitaifa na kusisitiza kuwa Serikali
itaendeleza vita dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi, kwa ari mpya,
nguvu mpya na kasi mpya.
Alieleza jinsi nchi ilivyokumbwa na
njaa katika baadhi ya maeneo pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta jambo
ambalo lilipandisha gharama za vitu vingine.
Kuhusu rushwa alisema katika kipindi
cha miaka mitano ya utawala wake, tuhuma nyingi zilichunguzwa na kesi
nyingi zilifikishwa mahakamani.
Pia, alipongeza kuundwa kwa Serikali
ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar mwaka 2009 baada ya viongozi wa CCM na CUF
kuamua kuweka tofauti zao pembeni.
Novemba 18, 2010
Baada ya kuchaguliwa tena kuongoza
nchi, Rais Kikwete alilihutubua Bunge Novemba 18, 2010 na kusema
Serikali yake itakuwa na vipaumbele 13 ambavyo ni umoja, amani na
usalama, kudumisha Muungano, kukuza uchumi na kupunguza umaskini,
mapinduzi ya kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda, kuboresha mazingira ya
uwekezaji na biashara.
Vingine ni kuongeza jitihada za
kuwawezesha kiuchumi wananchi wa makundi yote, kuboresha mipango iliyopo
ya kusaidia wajasiriamali wadogo na wote wanaotaka kujiajiri.
Chanzo:Mwananchi