Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa leo
ataendesha kongamano la kujadili mbinu za kuleta maendeleo endelevu
nchini na Afrika.Kadhalika Rais mstaafu wa Botswana, Festus Mogae ataelezea uzoefu wake katika kuongoza nchi na mapambano ya kukuza na kuboresha uchumi katika kongamano hilo ambapo limeandaliwa na taasisi za Club de Madrid.
Kwa mujibu wa tarifa ya Taasisi ya Uongozi Institute, iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na kusainiwa na Meneja Mawasiliano, Hanna Mtango, kongamano hilo litafanyika kwa siku mbili na kushirikisha viongozi na wasomi mashuhuri.
Mtango alisema katika kongamano hilo kuwa viongozi hao wa vyama na taasisi nyeti barani Afrika, watapendekeza sera zinazotekelezeka kwa kuzingatia mazingira ya Afrika ili kuchochea mabadiliko na kuleta maendeleo.
Alisema kongamano hilo litaendeshwa chini ya uenyekiti wa marais wastaafu na wanachama wa Club de Madrid, ambao ni Mkapa na Mogae wa Botswana.
Madhumuni kubwa la kongamano hilo ni kutoa fursa kwa viongozi wa Afrika kuchambua upungufu na vikwazo vya maendeleo Afrika, ambapo mifumo mbadala itakayofungua ukurasa mpya wa mchakato wa maendeleo, itapendekezwa.
Hanna alisema kongamano hilo litahusisha viongozii kadhaa wa kiserikali, sekta binafsi na vyama vya kijamii wapatao 80 na mkutano huo utaongozwa na majadiliano yenye ujumbe wa mabadiliko na kupata uzoefu kutoka kwa viongozi wa Afrika katika kuongoza nchi na mapambano ya kukuza na kuboresha uchumi.
CHANZO NI HABALI LEO