Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba akitia saini kitabu
cha maombelezo ya kifo cha Mjumbe wa Tume hiyo Dkt. Sengondo Mvungi
nyumbani kwake Kibamba jijini Dar es Salaam leo.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa taratibu za
kuusafirisha mwili wa Mjumbe wake, Dkt. Sengondo Mvungi aliyefariki
nchini Afrika Kusini zimekamilika na mwili wake unatarajia kuwasili
nchini siku ya Ijumaa, Novemba 15, 2013.
Baada ya kuwasili, mwili huo utahifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Aidha, siku ya Jumamosi, Novemba 16, 2013 kutafanyika Ibada ya
mazishi katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam
kuanzia saa 4:00 asubuhi. Baada ya misa, marehemu ataagwa katika Viwanja
vya Karimjee kuanzia saa 6:30 mchana siku hiyohiyo ya Jumamosi, Novemba
16, 2013.
Aidha, Marehemu Dkt. Mvungi anatarajiwa kusafirishwa siku ya
Jumapili, Novemba 17, 2013 kwenda Kisangara Juu, Wilaya ya Mwanga mkoani
Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika siku ya
Jumatatu, Novemba 18, 2013.
Dkt. Mvungi alifariki jana (Jumanne, Novemba 12, 2013) katika
Hospitali ya Millpark jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini
alikopelekwa kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Kitengo
cha Mifupa Muhimbili (MOI) aliokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani
kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu
waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba
3, 2013.
Wakati huohuo, Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakiongozwa na
Mwenyekiti wake Jaji Joseph Warioba leo (Jumatano, Novemba 13, 2013)
wameungana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete kufika nyumbani kwa marehemu Dkt. Mvungi eneo la
Kibamba jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa pole kwa familia, ndugu
na jamaa wa marehemu Dkt. Mvungi.